Mheshimiwa rais Samia Suluhu Hassan (SSH) Hayati John Pombe Magufuli alipotakiwa kuwashughulikia watangulizi wake waliokuwa wakishutumiwa kutenda ufisadi na vitendo vya hovyo–––kwa kujua uzito wa kazi ya urais na kuwaheshimu hata kuwaokoa wahusika–––alisema hakuwa madarakani kufukua makaburi. Kifupi ni kwamba, Magufuli alikataa kuwachunguza na hatimaye kuwashitaki watangulizi wake kama waliomshinikiza walitaka afanye ima kwa nia nzuri au mtego.
Mheshimiwa rais, leo, mheshimiwa rais naomba uniazima sikio lako niongelee kile nitakachokiita dhana mpya. Hii si nyingine ni kuonekana au kudhania kuwa serikali yako inapamba makaburi. Je hii maana yake ni nini? Ni ile hali ya wale waliohusika na kashfa ambao wakati wa mtangulizi wako walipotea kuanza kujitokeza na madai ya ajabu ajabu. Kwanza, hawa siyo makaburi kwa maana ile ya watangulizi wako bali ni makaburi kwa vile ni kashfa za kifisadi sawa na nyingine.
Mheshimiwa rais, nafahamu baada ya kifo cha mtangulizi wako, wengi wa wale aliokuwa amewaweka ndani tokana na kashfa mbali mbali wamesherehekea na kuona kama kuna neema itawashukia. Kwanza, tusiwaache washerehekee. Kazi ya kuwapatiliza iendelee kwa jina la Jamhuri ya Muungono wa Tanzania. Pili, siamini kuwa utawaacha waone kama mtangulizi wako ndiye alikuwa kikwazo badala ya ukweli kuwa walichofanya ni kinyume cha sheria. Tatu, naamini serikali yako haitawapa kile wanachokita–––to get away with murder, kwa kimombo. Nne, siamini kuwa utafumbia macho kashfa hizi na kuwaachia wahusika ili waende kutanua kwa kutumbua fedha walizoibia umma. Tano, naamini unajua ninachomaanisha. Na sita, hutafukua wala kupamba makaburi.
Mheshimiwa rais, kwa vile lengo la makala hii ni kuongelea dhana ya kupamba makaburi, ngoja nizame kidogo kwenye dhana yenyewe. Kwanza, nini maana ya dhana nzima ya kupamba makaburi? Katika mila nyingi na sehemu mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania, kuna utamaduni wa kujengea makaburi na kuyapamba kwa marumaru hata maua ili kuonyesha, heshima, kumbukizi na upendo wa marehemu. Hili si jambo baya ingawa makaburi yote yana uoza ndani. Hata hivyo, makaburi yanayoongelewa kwenye dhana hii ni tofauti na makaburi ya kawaida. Yanayoongelewa si makaburi bali kashfa zinazonuka na zenye uchafu unaonuka kuliko hata makaburi yaliyo na miili ya wapendwa wetu. Haya makaburi yana damu na jasho la watanzania. Hivvyo, haya si makaburi ya kupambwa wala kusameheka. Hii ni kutokana ukweli kuwa waliowaua ‘marehemu’–––yaani fedha na mali za umma–––wanajulikana na hawastahili msamaha wala huruma yoyote. Utawahurumiaje watu wenye akili na tabia za kinyama na wenye unyama wa kupita hata wanyama wenyewe? Utawasameheje watu wenye kutenda unyama kuliko hata wanyama wenyewe? Hivyo, kashfa husika siyo za kusamehe wala kuacha zitokomee kwenye kaburi la sahau.
Mheshimiwa rais, leo tutaongelea kashfa yenye kunuka sana iliyovuma iliyojulikana kama Lugumi ambapo Said Lugumi alituhumiwa kuibia serikali jumla ya shilingi bilioni 34 (Nipashe, Septemba 16, 2016) pale alipopewa tenda ya kufunga mashine ya kuchukulia alama za vidole nchini bila kufanya hivyo. Wakati wa kipindi chote cha mtangulizi wako, huyu bwana hakusikika wala kufurukuta. Hata hivyo, baada ya msiba wa Magufuli, Lugumi ameibuka upya. Hivi karibuni alikaririwa akifsi nyumba ‘zake akisema “mambo yalikuwa yanafanyika kwa nguvu tu, ndiyo maana kuna vitu vyangu vingi vilichukuliwa kwenye nyumba hizo, hasa nyumba ya Upanga ambayo ndiyo ilikuwa ofisi yangu” Mwananchi (Aprili, 15, 2021). Hapa inapaswa tujiulize maswali tena rahisi.
Je ilikuwaje Lugumi akakaa kimya muda wote Magufuli alipokuwa madarakani? Je nani alitumia nguvu kuchukua vitu vyake naye alichukua hatua gani? Je kwanini alikaa kimya muda wote huu hadi anaibuka baada ya miaka kama mitano hivi? Je hapa kuna kinachofichwa au kutaka kutupiga changa la macho? Je hizi nyumba anazodai ni zake kwa vipi wakati alishitakiwa kwa kosa ambalo mahakama haijatoka hukumu? Ilikuwaje mhusika akakabiliwa na tuhuma za kuhujumu uchumi bila kukamatwa na kuwekwa ndani–––tena bila ya dhamana–––hasa ikizingatiwa kuwa kesi za namna hii hazina dhamana? Je hapa kuna kitu kinafichwa na ukweli ni upi? Je hizi nyumba zingeuzwa kwenye mnada ulioshindwa angeweza kuzidai? Jibu analo Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambaye alikaririwa akisema kuwa mtu aliyekwamisha mnada wa nyumba za Lugumi, marehemu Dk Luis Shika “aliwekwa na Lugumi ili kukwamisha mnada. Ingawa sina facts (vielelezo) kuthibitisha hilo, lakini alichokuwa anafanya kinatufanya tuamini hivyo.” Je kama polisi walijua mchezo mzima, kwanini hawakuwakamata wahusika na kufichua njama zao? Je kwanini mamlaka hazimhoji Mambosasa na jeshi lake kutoa ushahidi ili kumaliza kadhia hii?
Mheshimiwa, bado kuna kesi nyingine nyingi ambazo hazijafutwa. Mojawapo ni ile ya wizi wa fedha za EPA. Hii kesi ilivutia watu wengi tokana na namna ilivyolidhoofisha taifa kwa kuwaibia wanyonge. Nayo naomba uitupie macho kuwa sehemu ya makaburi ambayo hayapaswi kupambwa bali wahusika kupewa zawadi ya maovu yao. Sitaijadili kashfa hii kwa kina kwa vile bado iko mbele ya vyombo vya kutoa haki. Ila, kwa kudokezea, tu, naomba nimalize kwa kusema yafuatayo:
Kwanza, usiruhusu serikali yako kupamba makaburi kama ilivyoelezwa kwa mfano wa kashfa ya Lugumi. Pili, naomba ufanye uchunguzi wa kina ili umma ujulishwe ukweli ni upi kwenye kesi ambazo zinazua utata ni kwanini watuhumiwa wanaibuka na madai ya ajabu ajabu kana kwamba walionewa baada ya kufariki kwa mtangulizi wako ambaye tunaamini unaendelea kumuenzi kwa vitendo na ukweli na siyo maneno matupu. Tatu, kwa wale wenye ushahidi kama vile alivyo Mambosasa, waitwe mbele ya mamlaka husika wawasilishe ushahidi wao ili kusaidia kuufikia ukweli wa mambo. Nne, mfano, swali la kujiuliza ni–––kama kweli hapakuwa na namna–––ilikuwaje mali za Lugumi zikose wanunuzi? Tano, je Lugumi ni zaidi ya huyu tunayemjua hasa ikizingatiwa mazingira yaliyotumika kumpatia tenda kubwa na nyeti kama hii bila kukidhi vigezo? Sita, je ni akina nani wako nyuma ya Lugumi? Saba, je nyuma ya Lugumi kuna nani na wangapi?
No comments:
Post a Comment