Wanawake wakimshangilia rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan alinifurahisha na kunikumbusha kitu kimoja pale aliposema, akihutubia wanawake kule Dodoma kuwa wanawake wana nguvu kuliko wanaume. Kwani wamejaliwa nguvu aina tatu yaani busara vichwani, ustahimilivu nyoyoni na vifuani na mtumboni kupitia kutengeneza na kuzalisha binadamu wote. Hapa kuna busara na somo kubwa tu. SSH aliendelea kusema kuwa wanawake siyo viumbe dhaifu bali wenye nguvu kuliko wanaume. Alitolea mfano kwa kumnukuu mke wa zamani wa Marekani, Eleanor Roosevelt aliyesema kuwa mwanamke ni kama jani la chai. Ukitaka kujua nguvu yake muweke kwenye maji moto. Atazalisha rangi mpaka uchoke. Alizidi kunogesha busara kuwa wanawake walijaliwa nguvu tofauti na wanaume ambao wamejaliwa misuli ya kunyanyua vitu hata kuviangamiza ikilinganishwa na wanawake waliojaliwa nguvu ya kuvitengeneza hivyo vitu hata watu.
Hata hivyo, wakati wanawake wanajitutumua wana nguvu kuliko wanaume kutokana na wanavyotumia nguvu zao constructively, kuna tatizo. Je ni wanawake wote wanajitambua na kuitambua nguvu waliyojaliwa? Je hata wanaojitambua na kuitambua, wanaitumia nguvu husika vilivyo na vizuri? Je wanawaathiri wenzao kujitambua na kuitambua nguvu yao na kuitumia kujenga mitandao yao ili kuweza kujikomboa toka kwenye mfumo kandamizi dume? Je wao wanajiandaaje kuwa sehemu ya suluhu na si tatizo? Je kwa kuendelea kutegemea kutendwa kwa kupendelewa ndo wanajikomboa au kuendeleza ukandamizaji?
Kuna jambo moja nataka niliseme hapa. Kama wanawake watajitambua na kuitambua nguvu yao na kuamua kuifanyia kazi na kuitumia bila kutegemea kuomba kupendelewa au kutambuliwa, wanaweza kufanya mapinduzi makubwa si ya kijinsia tu bali hata katika nyanja zote za maisha. Nakumbuka wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia. Baada ya kuona vita haikomi na wababe wa vita wanaendelea kuumiza na kuua watu wengi, wanawake waliogoma kutoa unyumba kwa waume zao hadi iletwe amani baada ya kuchoshwa na vita na walifanikiwa. Nchini Kenya hata Marekani silaha hii iliwahi kutumika na kuleta mafanikio. Hivyo, jambo ambalo unaweza kuliona kuwa dogo, likitumika vizuri, linaweza kufanya makubwa. Hapa sitaki niulizwe itakuwaje siku akina baba nao wakiamua kugomea suala hili. Hata hivyo, wana mbinu nyingi za kufanikisha mambo yao.
Baada ya kuonyesha na kutoa mifano kuonyesha nguvu walizo nazo wanawake, naomba nijikite kwenye nini wafanye ili kujikomboa. Kimsingi, kikwazo cha kwanza cha wanawake si mfumo dume bali wao wenyewe. Ni wao wenyewe kwa vile wanaupa mamlaka na nafasi mfumo dume kuwajengea utambulisho. Hii maana yake ni nini? Nitatoa mfano wa mashindano ya urembo. Licha ya kuandaliwa na wanawake, wanawake hutegemea hadhira ya wanaume kutoa vigezo vya urembo wao badala ya wao kuja na vigezo vyao wenyewe. Hii si mara yangu ya kwanza kutaka mashindano ya Miss Tanzania yaandaliwe na wanawke peke yao bila hata mwanamme mmoja. Kuendelea kuruhusu wanaume waandae na kutawala mashindano haya ni kuruhusu yaendelee kuonekana kama ya kihuni, kimalaya na yasiyo na maana. Kumekuwepo na tuhuma nyingi za rushwa ya ngono. Kuondoa uoza huu, ni kwa wanawake kuandaa mashindano yao wenyewe hasa ikizingatiwa hata kwenye ngazi ya familia, mama huwa ndiye anawaandaa mabinti zake kuwa warembo na si baba.
Kikwazo namba mbili kwa akina mama ni ile hali ya kuruhusu mfumo dume uwapendelee. Rejea kuwekwa katika sheria mfano viti maalum bungeni. Unapomruhusu mtu kukupendelea, jua anaweza hata kukuonea. Kama tutachukulia kuwa mfumo dume ni adui wa maendeleo na usawa wa akina mama si Tanzania tu bali dunia nzima, tutakubaliana kuwa mfumo huu hauwezi kuwapa nguvu wale unaowanyonya na kuwanyanyasa na kuwanyonya hata kuwagawana ili uendelee kuwatumia kwa faida yake. Wanachopaswa wahanga kufanya si kungoja kupendelewa au kupewa bali kunyakua kile wanachoona wamenyang’anywa. Je wanawezaje kunyakua hicho wanachotaka ambacho ni madaraka? Jibu ni rahisi kuwa–––kama watajipanga vizuri na kutumia namba kubwa waliyo nayo kama mojawapo ya nguvu–––wataingia madarakani tena bila kupambana wala kuandamana. Wakijipanga vizuri, watawahamasisha wanawake kuwapigia kura wagombea wanawake na kuwashinda wanaume. Hili halina ubishi. Kwani wanaowasaidia wanawake kushinda kwenye nafasi nyingi za uongozi ni wapiga kura ambao wengi wao ni wanawake. La pili wanalopaswa kufanya wanawake ni kuhakikisha wanawake wanahamasishwa kushiriki chaguzi na kuchagua wanawake wenzao ili waweze kutetea haki zao.
Mbinu au mkakati mwingine kwa akina mama kujikomboa na kuleta maendeleo na usawa, ni kuacha kulalamikalalamika na kutoa matamko bali kuanza kufanyia kazi umoja wao ili kuutumia kutatua matatizo ambayo yanawakumba na kuwaunganisha kama wanawake. Wakati wa kuachana na maneno na kuanza vitendo ni sasa kwa wanawake. Pia waelewe kuwa kuna wanaume ambao watawaunga mkono tokana na kujua wazi kuwa nao watakuwa wanufaika. Mfano, watu wengi walioko katika ndoa, bila shaka watasaidia wake zao, ukiachia mbali watoto wa kike hata wa kiume kusaidia mama, dada, shangazi na wanawake wengine wakijua fika kuwa ukimuendeleza mwanamke umeliendeleza taifa kwa ujumla. Mifano tunayo mingi toka nchi za Scandinavia ambazo zimewapa mamlaka wanawake nao wakayatumia vilivyo na vizuri.
Tumalizie kwa kuwataka wanawake wapokee changamoto waliyo nayo na kuifanyia kazi badala ya kulalamika, kutegemea kuwezeshwa na kupendelewa na wanaume. Bila kufanya hivyo, kelele zote za kumpa nguvu mwanamke na mtoto wa kike ni kupoteza muda. Nani alitegemea kuwa mashoga na wengine wangeweza kupambana na kupata ‘haki’ zao pamoja na wanachofanya kutokubalika kwenye mataifa mengi? Kama wanawake walivyounga na kudai haki za kupiga kura, usawa na mambo meingine mengi waliyofanikisha, wanapaswa kutumia wingi wao, kujenga mitandao, umoja na kusaidiana badala ya kupigana vita na kuwafaidisha maadui zao. Rais SSH ametoa changamoto. Basi wanawake watumie fursa hii kujikomboa. Kwani, hawatakombolewa na yeyote isipokuwa wao wenyewe.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment