Japo sina mpango wa kujadili suala ambalo liko kwenye mikono ya vyombo vya upelelezi na utoaji haki, kwani ni kinyume cha sheria. Hata hivyo, nina kila sababu ya kutumia suala hili kujifunza hata kufundisha wengine kama ambavyo niko tayari kufundishwa nao. Hivi karibuni, tuliona picha za aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya akiburuzwa mahakamni, pingu mkononi, kichwa chini na aibu isiyo kifani. Hayo ndo maisha. Hata hivyo, kuna somo ambalo watanzania hawawezi kuepuka kujifunza. Hili si jingine bali ukweli kuwa mwanzo wa utawala wa awamu ya sita kufanya mambo tofauti kama njia ya uboreshaji uwajibikaji kwa viongozi wa umma inafungua ukurasa mpya wa uwajibikaji wa umma na watanzania kwa ujumla.
Hakuna ugomvi kuwa Hayati Dk John Pombe Magufuli rais wa awamu ya tano alipendwa sana na wanyonge tokana na kuwapigania na kupambana na uoza pale alipoweza. Pamoja na nia yake njema na thabiti, baadhi ya wateule wake walimuingiza mkenge kwa kuwanyanyasa wanyonge hao hao huku wakijitahidi kumfurahisha ima kwa unafiki, kujipendekeza ua kung’ata na kupuliza. Hapa ndipo sakata zima la nani aliwahudumia wanyonge vizuri au vibaya na kuwatumia kujihudumia badala ya kuwahudumia–––kama ilivyodaiwa kwenye sakata la Sabaya–––linapochomoza likiacha maswali mengi kuliko majibu huku umma ukingojea kuona wengine kama yeye wakichuliwa hatua za kisheria ili kutenda haki na kuleta tabia ya uwajibikaji kwa umma.
Hakuna ubishi kuwa Hayati Magufuli ataingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama kiongozi si aliyepigania wanyonge tu bali pia aliyewateua vijana wengi kwenye nafasi za juu tena wengine hata bila sifa stahiki. Leo tutaangalia namna baadhi ya vijana walivyomtumia Magufuli kujifanyia mambo walivyotaka tokana na ukosefu wa uzoefu, ujinga, ulimbukeni na ujana ukiachia mbali ulevi wa madaraka. Wakazi wa mkoa wa Dar wanajua fika jinsi mmojawapo wa vijana hawa wapya kwenye ngazi za juu–––aliyekabiliwa na tuhuma za kughushi elimu na kutumia majina bandia na kunyamaziwa na Magufuli–––alivyoendesha mkoa kama mali yake au ya baba yake kama siyo mama yake. Tunajua aliwahi kusema maneno mazuri juu ya rais SSH wakati wa mchakato wa katiba mpya iliyouawa. Hata hivyo, hii haimpi kinga ya kushtakiwa pale alipokosea. Waliwaangusha waliowateua na pia hawakujua mwanzo wala mwisho wa mamlaka yao ukiachia mbali ubabe, ubinafsi na upogo na upofu wa kutoona mbali. Mfano, mteule huyu alifikia mahali hata kuvamia studio, kutesa, kunyanyasa hata kudhalilisha mawaziri. Rejea kisa cha kutumbuliwa Nape Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Katibu baada ya kuhoji uchavu wa mteule huyu aliyesifika kwa akujipendekeza kwa hata kumuabudia Magufuli jambo ambalo naye alipenda na kumvumilia hadi arobaini zake zilipoisha na akamtumbua. Rejea kutishiwa kuuawa kwa bastola kwa Nnauye kwa sababu ya kutaka kujua uoza wa kijana huyu ambaye kwa sasa si mteule bali mkulima mwenye kumilki mali ambayo sijui kama anaweza kuitolea maelezo ukiachia mbali kuwa na muhanga wengi. Je hawa walioteswa na kuhujumiwa chini ya kijana huyu wako tayari kujitokeza ili serikali ichukue hatua kama ilivyofanya kwa Sabaya? Hapa hujagusia waliokimbilia kwenye siasa wakaukwaa ubunge. Hata hivyo, historia yao haiwezi kufutika wala kukimbiwa. Lazima nao walipie madhambi yao ili haki ionekane inatendeka sawa kwa kila mtanzania.
Kama azma ya serikali ya awamu ya sit ani kutenda haki na kurekebisha mapungufu yaliyotokea kwenye utawala uliopita, tunaamini haitaishia kwa Sabaya bali kuanzia kwake. Magufuli alikuwa binadamu ambaye asingeweza kila kitu. Ndiyo maana wahusika walimzidi kete na kufanya mambo yao na kujineemesha bila yeye kujua. Hata baba wa taifa haya yalimtokea. Kwani si wote waliokuwa wakiimba ujamaa walikuwa wajamaa kama yeye. Hivyo, tusione aibu wala kuogopa kufichua uoza uliotendekeka chini yake sawa na ambavyo utatokea chini ya utawala huu. Mfano mzuri ni toka kwenye utawala Hayati Benjamin Mkapa aliyekiri wazi kuwa baadhi ya watendaji aliowaamini walimuangusha na kumhujumu sawa na hawa waliomuhujumu Magufuli. Watu hawa wanajulikana. Vitendo, ukwasi hata uovu wao vinafahamika kwa watanzania wengi. Hivyo, ni wakati muafaka kutenda haki na kuwashulikia kwa mujibu wa sheria ili liwe funzo kwa wengine. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amejitofautisha na uonevu hana haja ya kusita kuwachukulia hatua ili asionekane anatumia sheria kibaguzi na kiupendeleo.
Ukiachia huyu wa Dar, yupo mwingine wa Arusha ambaye naye alijigeuza muung mtu akinyanyasa, kuvunja sheria na kujifanyi alivyotaka asijue cheo ni dhamana. Hawa si watu wa kufumbia macho wala kuvimilia. Lazima walipie madhambi yao kama kweli tumedhamiria kutoa haki na kufanya mabadiliko yenye lengo la kuleta mabadiliko yanayolenga kuheshimu mamlaka kama dhamana ya umma. Sheria ya Tanzania iko wazi kuwa hakuna aliyeko juu ya sheria. Hivyo, wahusika wanapaswa kushughulikiwa kisheria ili kuweka mambo sawa na kuondoa dhana kuwa sheria inatumia kibaguzi na kwa upendeleo.
Tumalizie kwa kumtaka rais SSH kutenda haki sawa kwa wote. Wote wanaofahamika kuwa walitumia madaraka vibaya ima kwa faida binafsi kiasi cha kutokea kuwa matajiri wenye utajiri usio na maelezo au kuwaumiza wengine lazima washughulikiwe bila ubaguzi wala upendeleo. Tanzania ni ya wote kama ambavyo rais SSH amekuwa akisisitiza mbali na kuwaamuru wateule wake kuwaheshimu wananchi ambao kimsingi, ndio wenye madaraka waliyokasimu kwa viongozi ukiachia mbali kuwa viongozi wote wa umma wanaendesha maisha yao na kulipa mishahara yao tokana na kodi za wananchi wa kawaida wanaopaswa kuwatumikia na si kuwatumia kama ilivyo kwenye kadhia tajwa.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment