Sina ugomvi na hakimu aliyetoa adhabu ya kufungwa miaka nane au kulipa faini ya shilingi milioni nane kwa aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) David Mataka. Wala sina ugomvi na hukumu husika wala maslahi binafsi–––kama mtu ambaye nimesoma sheria–––kwa vile, najua lilipo tatizo. Najua wengi watakuwa wameshangaa hata kulaumu kama siyo kukata tamaa na kukasirika. Wapo waliosema hakimu alikuwa amekatiwa kitu kidogo au kikubwa jambo ambalo ni aibu kwa vile wahusika walishindwa kujua sheria zinasemaje. Na siyo kila kesi lazima iwepo rushwa au ushawishi. Hakimu hufukia uamuzi wa kesi kwa kuzingatia sheria, ushahidi, hata utetezi mbali na mengine.
Kwa mfano, kama mshitakiwa alitenda kosa kweli tena mbele ya jaji au hakimu, kama ushahidi utakosekana, kupungua, kukosa kurithisha mahakama au kuvurugwa, hakuna shaka ataachiwa tu hata kama jaji au hakimu alishuhudia vinginevyo hakimu au jaji aamue kuwa shahidi jambo ambalo ni gumu sana. Mfano, kama kesi husika, inabidi tujiulize. Sheria inasemaje? Je mfumo wetu ni wa kifisadi hivi kiasi cha kuendelea kuwa na sheria za hovyo zenye kutetea na kulinda ufisadi hivi? Haya ni maswali muhimu hasa ikizingatiwa kuwa hakimu huwa hatungi sheria bali kutafsiri sheria na kutenda haki kwa mujibu wa sheria na kesi. Hivyo, kitu cha kwanza naweza kusema kuwa wale wanaodhani mahakimu wanapewa au kulishwa kitu wanawaonea. Badala ya kulaumu mahakimu ambao mikono yao imefungwa na sheria, walaumu sheria na waliozitunga bila kuangalia mazingira na wakati.
Kwa mfano, sheria nyingi tulizo nazo zina asili yake kwenye sheria za kikoloni ambazo lengo lake ilikuwa ni kuwezesha na kulinda ukoloni. Wakati sheria hizi za kikoloni zikitungwa, watendaji wakuu wa serikali ya kikoloni walikuwa wazungu. Na lengo na ukoloni ilikuwa ni kubia makoloni yao. Hivyo, kulinda watendaji wake ambao wote walikuwa ni wazungu, wakoloni walitunga sheria zenye kutoa adhabu nyepesi kwa makosa yaliyotendwa na wazungu ambao wakati huo ndio walikuwa wakubwa. Ndiyo maana sheria zinazohusiana na ujambazi na wizi ulioweza kutendwa na watu wa kawaida au waswahili yalipata adhabu kubwa wakati yale yaliyotendwa na wazungu au wakubwa kama vile wizi wa mali ya umma zilipokea adhabu nyepesi hasa faini kama ilivyotokea hivi karibuni kwenye kesi tajwa hapo juu. Kwa spirit ya sheria za Kikoloni, Mataka ni tabaka la wakubwa. Hivyo, hapaswi kufungwa bali kutozwa faini. Hii ndiyo mantiki ya kutuhumiwa kusababisha serikali hasara ya shilingi bilioni 71 kutozwa shilingi milioni nane tu. Huu si mzaha wala utani bali matusi kwa watanzania ambao–––kwa takriban miaka 60–––wamekuwa wakitembea kifua mbele na kutangaza kuwa wako huru wakati si kweli kama wataendelea na sheria za kijambazi na kiwizi kama hizi ambazo kisheria zimepakwa sukari wakati ni sumu ili kukidhi vigezo vya utawala bora unaotambuliwa na wezi wa magharibi. Je kwa mchezo na mzaha huu, nini kitamzuia kila mwenye fursa kuiba akijua atachomoka bila madhara bali mafedha lukuki? Je taifa zima tunaweza kuwa mataahira hivi kiasi cha kutunga sheria za kusikinisha walio wengi ili kutajirisha wezi wachache? Je ni wangapi watakaa kwenye nafasi za juu milele? Kuna haja ya kubadilika tena haraka. Fīat jūstitia ruat cælum, acha haki itendeke hata kama mbingu zitaanguka. Hii maana yake ni kwamba, tusiogope kutenda haki kwa vile tunawagusa wakubwa au wateule. Tanzania ni kubwa na muhimu kuliko watu binafsi.
Leo, sitaki kusema mengi hasa ikizingatiwa kuwa ninachoongelea siyo somo jepesi. Hakuna watu wajuaji kama waandishi wa habari na wanasheria. Japo mimi ninavyo vyote ukiachia mambo mengine, naomba nisisitize kuwa nitatumia fursa hii kuishauri serikali iache kupoteza muda kutumia sheria za kikoloni huku ikiwaaminisha wananchi kuwa wako huru. Pia ifahamu kuwa hawa watu wanaoibiwa kwa kutumia sheria za kikoloni na kijambazi, wanaweza kuamua siku moja pakachimbika bila jembe iwe ni kwa kura au fujo hasa umaskini na ukosefu wa ajira vinapozidi kushamiri huku wakishuhudia wezi wakubwa wakipigwa faini ya vijesenti wakati wamezamisha mabilioni. Nakumbuka mheshimiwa Rais aliwahi kumuonya IGP kuwa ujambazi ukiendelea hatavumilia. Je kama IGP anapewa onyo kuhusu ujambazi wa bunduki, kwanini nasi tusimkumbushe mheshimiwa Rais kuwa hata majambazi wa kalamu ni hatari tena kuliko hawa wa silaha kwa vile kumilki silaha ni kinyume cha sheria wakati kumilki kalamu ambayo nayo pia ni sheria ni halali.
Tumalizie kwa kuwaomba watanzania wasikubali kuendelea kuwa na sheria za kijambazi wakati mwisho wa siku wao ndiyo waathirika wakuu. Kwani, kama nilivyosema hapo juu, serikali haina shamba wala mradi zaidi ya kodi za wananchi na raslimali zao ambazo sheria hizi tulizorithi toka kwa wakoloni kiasi cha kuibiwa na kunufaisha wezi wachache wenye madaraka ambao hawana cha kuogopa kwa vile sheria zinawamotisha na kuwalinda wanapouibia umma nao wakiwamo. Kwani, wengi wao wanapodondoka hujikuta pabaya. Kazi ya kubadili sheria hizi si ya bunge wala serikali tu bali wananchi pia.
Chanzo: Raia Mwema Kesho.
No comments:
Post a Comment