The Chant of Savant

Thursday 5 August 2021

Kwa sera za sasa Tanzania ina haki ya kutonufaika na diaspora

Mpendwa Rais Samia Suluhu Hassan,
Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sema “Kazi Iendelee” na kweli inaendelea.
Baada ya kukuamkua, naomba nikupe ya moyoni kuhusiana na somo tajwa hapo juu.
        Naamini, kama mtanzania na kiongozi wa nchi, unajua kuwa Tanzania hainufaiki na raia wake wanaoishi ughaibuni almaaruf diaspora tofauti na nchi nyingine zinazofaidika baada ya kuwawekea mazingira wezeshi kama vile kuwaruhusu kuwa na uraia pacha. Wakati wa vita baridi kati ya Marekani na uliokuwa Umoja wa Kisovieti wa Kisoshalisti wa Urusi, Tanzania ilipiga marufuku uraia pacha kwa kuogopa kutumika kupenyezwa maadui na kuivuruga hasa kipindi ikijenga siasa za Ujamaa ambazo hadi leo zimetuletea heshima na utulivu ukiachia mbali mshikamono na amani. 
Kama ulivyofanya maamuzi magumu kuruhusu chanjo na kuchukua tahadhari zidi ya Ukovi-19, liangalie hili la uraia pacha chonde chonde.
        Hata hivyo, baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin na mfumo mzima wa kijamaa chini ya USSR ambapo dunia nzima iko chini ya himaya moja ya kipebari, kuna haja gani ya kuendelea kuwa na katazo na sheria kama hizi? Tunaogopa nini kama siyo kile waingereza huita the fear of the unknown au woga wa kisichoeleweka? Tangu kuanguka kwa ukomunisti, dunia imebadilika sana. Kwa mfano, Tanzania ukiondoa Visiwani, hatukuwa na televisheni, vyama vingi wala uhuru wa habari. Sasa tunavyo tena kuliko hata wale waliokuwa navyo kabla yetu. Sasa tunashirikiana hadi na Israel taifa ambalo tulikuwa tumeliwekea vikwazo. Kimsingi, tumefungua milango ya nje na kufunga ya ndani kwa hasara yetu.
        Mheshimiwa Rais, vitisho vya zama zile havipo tena. Hivyo, kuendelea na ukale huu tunajipotezea furs ana watu wetu. Mfano, wapo wanaoleta madai yasiyo na mashiko kuwa uraia pacha unaweza kuondoa uzalendo. Hiki ni kituko. Kwani mafisadi wetu wengi  walioumiza umma wa watu wetu kwa kuwaibia wana uraia pacha? Wengine wanadhani kuwa tukiruhusu uraia pacha tutaibiwa. Ala! Sisi ni nani na tuna nini ikilinganishwa na nchi tajiri? Kwanini nchi tajiri zinaruhusu watu toka nchi maskini kama Tanzania kuwa na uraia wao na bado wakabaki na uraia wan chi zao za asili? Je tunawazuia kwa sababu za maana zaidi ya ukale na roho mbaya kuwa wanaweza kuwa tishio kisiasa au kwa sababu za maana? Nitagusia kidogo hapa chini.
        Kwanza, kama  kweli tutataka kufaidika na diaspora wetu, tubadili sheria na mazoea ya hasara.Turuhusu uraia pacha. Hoja kuwa uraia pacha unaondoa uzalendo ni woga usio na mashiko na zimepitwa na wakati. Wakati wa kuhofia kupandikiziwa mashushu umeishakwisha. Siasa za sasa siyo sawa na zile za zama zile za ubepari na ukomunisti au chama kimoja na mapinduzi ya kijeshi. Tuwe wakweli kuwa uraia kwa watanzania weusi unakataliwa kwa hofu kuwa wakija wataweza kugombea nafasi za kisiasa. Mbona tunao wengi waliokuwa na uraia pacha tena wakawa hata viongozi? Nani anaweza kutwambia sababu ya aliyekuwa waziri wa fedha wa awamu ya kwanza marehemu Amir Jamal kufia na kuzikwa Kanada kama hakuwa na uraia pacha? Je ni waasia wangapi hupeleka wake zao kuzalia nje ili wawe na uraia pacha na wanaendelea kutesa nchini?
        Pili, mbali na hao juu, inashangaza tunavyoruhusu matapeli wengi toka nchi za kigeni kuja na kufungua makanisa na kuwaibia watu wetu wajinga na waliokata tamaa na kuishia kuwa matajiri wa kutupwa kwao ambako wananunua mali nyingi ikiwemo ardhi na nyingine tunazowanyima diaspora wetu. Je huu si ubaguzi wa kujibagua wenyewe? Utakuta kuwa hata matapeli hawa wa kiroho wanatumia mwanya wa madhehebu ya dini kutolipa kodi kutofanya hivi huku wakiwahujumu watu wetu na nchi yetu kwenda kutajirisha kwao. Fanya uchunguzi uone yapo madhehebu mangapi yanamilkiwa na wageni wakati mkiwanyima haki watanzania wenye uraia pacha kufaidika na taifa lao ambalo mawazo mgando yameruhusu kuibiwa na matapeli kwa kisingizio cha dini.
        Tatu, je kwanini watanzania wanachukua uraia wa nchi nyingine hasa kwa wale wasiojua kuwa wanaweza kuwa permanent residents? Wengi ni kwa sababu za maisha kama vile ajira, masomo na manufaa mengine. Mfano, mtanzania akiamua kusomea hapa Kanada akiwa si raia au mkazi wa kudumu, atalipia gharama za masomo mara tatu kuliko Mkanada au mkazi wa kudumu wa hapa. Mojawapo ya sehemu diaspora wanaweza kusaidia Tanzania ni kwenye taaluma. Mfano, mtu kama mimi ambaye nategemea kupata shahada yangu ya uzamivu hivi karibuni, naweza kufundisha kwenye chuo chochote au kutoa ushauri kwa serikali kwenye maeneo niliyobobea bila kinyongo. 
           Kwa wasomi wa viwango vya juu siyo shida sana. Kwani, ukizenguliwa Tanzania, nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini zinakuchukua chap chap na kwenu wanakosa. Wapo wenye mitaji wanaoweza kuwekeza kama watatengenezewa mazingira mazuri. Wengine huchukua uraia au ukazi wa kudumu ili kusomesha watoto wao. Na wakishamaliza, watoto hawa wanaweza kuajiriwa au kujiajiri nchini kama watajengewa mazingira mazuri. Si wote wanajua sheria kuwa ukifika uwanja wa ndege unaweza kuukana na kuendelea na maisha. Hata hivyo, wengi wanaogopa kupoteza haki za watoto wao waliozaliwa ughaibuni.
        Nne, kwa mujibu wa mtandao wa brookings.edu, nchi kama vile Lesotho, Gambia, na Sudan ya Kusini hutegemea pesa toka kwa diaspora kwa kiwango cha asilimia  hutegemea fedha toka kwa diaspora wao kwa kiwango kikubwa  cha  21%, 15% na 35% cha pato la taifa mtawalia wakati Tanzania hatunufaiki tokana na sera na msimamo wa kizamani. Kwa nchi kama Ethiopia, Kenya na Nigeria, diaspora ni kitega uchumi na chanzo kikubwa cha mapato kwa mataifa haya. Badala ya kutwishana kodi zisizokubalika kama za uzalendo usiokuwepo, kwanini tusiwatambua diaspora wetu ili kuwamotisha wawekeze kwao?
        Kwa heshima, nimalizie kwa kuwaombea watanzania wenzangu ambao, ima tokana na kutojua kuwa unaweza kuwa na ukazi wa kudumu na kubaki na uraia wako ukafaidi nchi mbili au kulazimika kuchukua uraia wa nje kufikiriwa kuruhusiwa uraia pacha. Uzalendo wa mtu hautegemei idadi ya uraia bali mapenzi na tabia ya mtu. Kuepuka kuendelea kukosa fedha za diaspora wetu na kuwapunguzia hofu hata kudhulumiwa–––kwa wale wasiojua sheria kuwa unaweza kuukana uwanja wa ndege na kufanya vitu vyao­­ko–––waruhusu wawe na uraia pacha wachangie kwenye pato la taifa lao ukiachia mbali kuwa wao ni chanzo kizuri cha mapato.
Chanzo: Raia Mwema.

No comments: