The Chant of Savant

Thursday 19 August 2021

Je Huu Ndiyo Mwanzo wa Mwishi wa Gwajima?

Kama kuna watu wameonyesha uzalendo na kuweka mbali maslahi binafsi, si mwingine bali Daktari wa kweli Doroth Gwajima waziri wa Afya. Tunapongeza kwa hili na kumpa shime asiyumbe bali kuendelea kuitendea haki ofisi yake na hadhi yake bila kujali mambo ya kifamilia na ya kibinafsi. Kuna clip inayozunguka kwenye mitandao ambapo Daktari Gwajima akionekana kukerwa wazi wazi na tabia ya Mbunge wa Kawe Josephat Gwajima aliyejipachika uaskofu ambaye anasema ni shemeji yake. Anaonya kuwa hana mchezo na kazi ya umma hasa viapo alivyokula. baada ya kuchoshwa na maneno ya shemeji yake. Ndipo alipoamua kumtolea uvivu. Dk Gwajima alikaririwa akisema kuwa yeye ni waziri aliyeapa kwa viapo vyote vya kuwatumikia wananchi na siyo familia. Pia, alionyesha watanzania wanavyopaswa kutambua uzushi wa huyu shemeji yake ambaye alidai mojawapo ni madai kuwa angemfufua marehemu Amina Chifupa–––ambaye, hata hivyo, hakumfufua zaidi ya kumtumia kujipatia ujiko–––mbali na kuwahi kudai kuwa ubunge na hara urais ni vyeo vidogo ambavyo mtu wa Mungu hawezi kushindani akaishia kupwakia ubunge bila aibu tena kwa kubebwa na chama chake. Pia Dk Gwajima ameeleza kigeugeu cha shemeji yake ambaye aliwahi kukimbia CCM na kujiunga na CHADEMA na kurejea CCM kinyemela.
Dk Gwajima aliongeza kuwa Gwajima aliwahi kufumwa na mrembo akadai ulikuwa mkono wa baunsa. Pia alimuonya Gwajima kuacha kumharibia kibarua. Hata hivyo, Dk Gwajima amesema hatamuachia aendelee kupotosha umma. Na badala yake atamshughulikia hadi athibitishe madai yake ambayo ameonyesha wazi kuwa ni ya kuzua na kuungaunga bila usayansi wala mantiki yoyote. Madai yasiyo na uthibitisho wa kisayansi ya Gwajima, licha ya kukera na kupotosha, yanaonekana kumkera shemeji yake huu ambaye ameweka kila kitu hadharani. Nadhani hatua hii huwa haifikiwi bila kujaribu kumaliza mambo nyuma ya pazia. Ukiona hivi, ujue kila mbinu ishajaribiwa na kushindikana ili mhusika aumbuke kama ambavyo itakuwa na siku moja waliosoma makala hii watakumbuka.
Je tunachoshuhudia ni mwanzo wa mwisho wa Gwajima? Maana, ukiona wanaojua mchezo mzima uzalendo unawashinda wanaamua kukutolea uvivu, jua arobaini yako inakaribia. Na arobaini ikifika huwa haizuiliki wala haikupi taarifa bali kuwadia.Kwa wanaojua waliotangulia kufanya biashara ya neno kama yeye, wanafahamu namna ambavyo wafanyabiashara hii na wasanii huporomoka hasa kutokana na uongo wanaokuwa wakitumia kufikia kikomo. Hii ndiyo nature ya mambo ya kibinadamu hata yavishwe uungu vipi.
Hata hivyo, wakati tukimsaidia Gwajima kuona ukweli, tufahamu. Wapo baadhi ya wenzetu wenye ugonjwa wa kutaka umaarufu hata kama ni kwa njia mbovu, kuumiza, kupotosha, kunyonya wenzao bila huruma japo nao hudondoka bila huruma. Kama si ugonjwa ni nini mtu mzima tena anayejiita msomi na mtu wa Mungu kuhadaa dunia nawe ukiwamo eti unaeweza kutenda miujiza kama kumfufua Amina Chifupa? Swali ambalo ni onyo ni lile lile alilouliza Dkt Gwajima “je Gwajima alimfufua Chifupa? Japo hii ni aina ya utapeli wa kujipatia fedha na ujiko kupitia migongoni mwa wengine, mara nyingi mwisho wake huwa si mzuri. Pia, uhitaji kiwango fulani cha ujinga, ukatili na unyama kutoa madai kama haya bila kujali yanawaumiza vipi wafiwa.  Hata tunavyorejea kadhia hii, tunaumiza ndugu zake marehemu.  Hata hivyo, hatupaswi kufanya hivyo ili kuwafungua macho wale ambao bado wanaamini katika ujinga huu. Nchini Marekani ulipoanzia mchezo anaocheza Gwajima al maaruf televangelism, mtawakumbuka wakongwe kama Jim Bakker ambaye aliporomoka baada ya kugundulika kuwa alikuwa amempa mama mmoja aliyekuwa akifanya naye mapenzi wa nguvu dola 270,000 ili kumnyamazisha. Mwingine ni Mkenya Gilbert Deya, mchungaji wa kujipachika, aliyewaaminisha wagumba kuwa alikuwa na uwezo wa kuwapatia watoto kimiujiza al maaruf miracle babies kumbe watoto wenyewe walikuwa ni kuiba mahospitalini. Wengi watakuwa wanakumbuka kilichompata Jesse Jackson aliyewahi kujizolea umaarufu kama mhubiri na mtetezi wa haki za binadamu ambaye aliwahi kutoa msaada wa ‘kiroho’ kwa Rais Bill Clinton wakati wa kashfa ya Monica Lewinsky akaishia kuzamishwa na kashfa hiyo hiyo baada ya kugundulika kuwa kumbe alikuwa amezaa na mtumishi wake.
Hao wote hapo juu hawakujua kuwa kulikuwa na arobaini yao. Hivyo, siku ilipofika, walijikuta wakidondoka kwa aibu na kutoweka kwenye ujiko waliozoea ukiachia mbali fedha walizokuwa wakiwakamua waumini na wafuasi wao. Hili halina kinga. Ni kama ajali. Wakati ukifika unafika na huanza kama masihara. Hakuna mjanja katika mambo ya uongo. Mhusika atafanya kosa dogo siku moja na kila kitu kitafunguka na ataanguka na kuumbuka. 
Tumalize kwa kumpongeza waziri Gwajima huku tukimtaka Gwajima atie akilini kuwa anachofanya kitamrudia muda si mrefu hasa ikizingatiwa kuwa wale anaowachokoza, yaani serikali, wanaujua mchezo wake mzima sema walikuwa wakimpuuzia na kumwacha tu. Kwani, hakuna kosa kubwa kama kujisahau ukaanza kuukata mkono unaokulinda au kuiteketeza silaha inayokulinda. Tumeyaona nchi ya jirani ya Kenya ambapo naibu wa Rais sasa analalamika kuanza kufichuliwa uoza wake. Wahenga walisema kama unaishi kwenye nyumba ya vioo, usiwachokoze watupa mawe. Watakusambaratisha na jumba lako la vioo. Je wakati wa kumshughulikia Gwajima ndo unapiga hodi? Je huu ndiyo mwanzo wa mwisho wa Gwajima. Ama kweli, dawa ya moto ni moto na dawa ya Gwajima ni Gwajima!
Chanzo: Raia Mwema Ijumaa.

No comments: