The Chant of Savant

Monday 16 August 2021

Gwajima, Tafadhali Tuepushe na Siasa Uchwara Kwenye Chanjo

Hivi karibuni, wamejitokeza watu wenye ushawishi kupinga chanjo ya Ukovi-19. Japo ni haki yao kutochanjwa lakini si haki yao kupinga. Kwani wanapinga tu bila kutoa namna mbadala ya kupambana na janga hili. Lazima tujifunze toka kwenye makosa. Wakati wa awamu ya tano tuliaminishwa kuwa Mungu alikuwa ‘ameikinga’ Tanzania na janga hili kupitia maombi. Hata hivyo, tukiweka kujiridhisha, kujilisha pepo na woga wa wakubwa waliotuaminisha hivi, hakukuwa na kitu kama hicho. Wengi watauliza. Kwanini sikuyasema haya wakati ule. Nisingeyasema yakachapishwa na gazeti lililofanya hivyo likasalimika. Hivyo, kama tulivyounganishwa kupinga chanjo na kujiaminisha kuwa tulikuwa ‘tukilindwa na Mungu’ kwanini tusiungane kwanye kukubali chanjo?

            Leo ngoja tuseme wazi kuwa kupinga chanjo bila kuwa na namna mbadala ni ushirikina na kujilisha pepo. Tutaangamia tukijiona tokana na kutokuwa tayari kujifunza na makosa. Waswahili husema kosa si kosa bali kurudia kosa. Mfano, wenye ushawishi miongoni mwetu wanaosimama majukwaani na kwenye mimbari kupinga chanjo waambiwe fika. Hili, kwa sasa haliwezekani na halikubaliki. Hatuwezi kuwa wagumu hivi wakati tukishuhudia watu wetu wakiteketea. Kama wapo wanaoamini katika maombi kama ilivyokuwa, basi watuonyeshe yanavyofanya kazi badala ya kutupotezea muda na kupotosha watu wetu. Wameshaambiwa kuchanja au kutochanja ni chaguo la mtu. Kwanini watake kushawishi wengine kutofanya hivyo?

            Leo nitatoa mfano kwa Josephat Gwajima, Askofu na daktari wa kujipachika ambaye pia ni mwanasiasa. Hivi karibuni alikaririwa akisema “wanaotaka nifukuzwe CCM watumie akili, kwa mfano tukichanja wote halafu kufikia 2025 watu wako hoi tunapigaje kampeni, bora wengine tubaki tusaidie kutetea chama chetu.” Hii ni hoja mfu. Je hali ikiwa tofauti? Je mawazo mgando kama haya yatakuwa yamekisaidia hicho chama? Je chama kinahitaji msaada kwa mawazo mgando hivi? Je kati ya Chama na Gwajima nani anahitaji msaada wa mwingine? Nani amsaidie nani wakati Chama kilimsaidia Gwajima kuwa mbunge bila kustahiki baada ya kuwaengua waliokuwa wameshinda kura za maoni kihalali? Je tungetumia mawazo kama haya zama za Ebola na Ukimwi hali ingekuwaje? Je hapa nani anapaswa kukumbushwa kutumia akili? Je sera ya CCM kuhusiana na chanjo ni ipi? Gwajima ni nani anayepingana na mabosi wake waliochanjwa kama vile mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na vigogo wengine wa chama chake?

            Kimsingi, anachofanya Gwajima ni kutafuta kiki kisiasa baada ya utawala mpya kuingia madarakani bila kutarajiwa. Tukiwa wakweli, Gwajima anaongea anayoongea kwa utalaam upi? Mwenyekiti Mao Zedong aliwahi kusema kuwa kama hujafanya utafiti, huna haki ya kuhoji. Gwajima hana utafiti wowote wenye mashiko zaidi ya hisia zake. Si vizuri kumpuuzia tukidhani wafuasi wake na wenye mawazo kama yake watampuuzia. Chama chake kimpe onyo, anyamaze mwenyewe au anyamazishwe. Kama ataamua kutochanja basi afanye hivyo kibinafsi badala ya kugeuza sera na habari kwenye vyombo vya habari.

            Kuendelea kupiga kelele kwa Gwajima kuna mafunzo makuu yafuatayo:

Mosi, anapinga na serikali yake wazi wazi ukiachia mbali chama ambacho kina taratibu zako na vikao maalum vya kuweza kufutu masuala kama haya kama angeamua kuvitumia. Je Gwajima hajui utaratibu huu wa chama chake kama kweli ni mwanachama anayejua sera na taratibu za chama chake?

Pili, Gwajima anaonyesha dharau wazi wazi kwa serikali na chama chake. Hii maana yake ni kwamba chama na serikali vimekubali kuchanja kutokana na kutowajali watanzania au kutojua wanachofanya?  Anasema kuwa chanjo haijafanyiwa utafiti. Chanjo ipi kati ya zinazotumika kupambana na Ukovi-19 kwa sasa? Je maombi yamefanyiwa utafiti? Nini hoja hapa kutumia vitu visivyofanyiwa utafiti kutaka kusimamisha hoja. Kasisi, mganga wa kienyeji na wengine kama hawa, hawana utafiti wowote kuhusiana na huduma zao zaidi ya kutegemea imani jambo ambalo ni pata potea. Ndiyo, tunaweza kumuomba Mungu. Lakini Mungu anasema ukitaka akusaidie jisaidie kwanza. Mojawapo ya njia ya kujisaidia ni kutumia akili vizuri na kukubaliana na ukweli hata kama unapingana nao. Ukovi-19 ni janga la dunia.

Tatu, Gwajima anagawanya wanachama na watanzania bila sababu za msingi bali siasa za kutafuta umaarufu binafsi. Niliwahi kuonya kuchanganya dini na siasa. Sasa ndiyo kunaanza kujionyesha wazi wazi kupitia matamshi ya Gwajima. Je Gwajima ni nani katika CCM hadi ajiamini hivi? Nini msimamo wa chama dhidi ya upotoshaji huu. Tulisikia UVCCM wakimpa vipande vyake. Je baba lao CCM mko wapi au kuna namna yaani mgawanyiko ndani ya chama?

Nne, Gwajima anapaswa aelimishwe na kuulizwa nani anaowawakilisha dhidi ya serikali yenye ridhaa ya wananchi? Kama Gwajima anaona chama chake na serikali yake vinaenda kinyume, kwa mjuzi na mstaarabu, unajiondoa kwenye vyombo hivi na kusimamia kile unachokiamini badala ya kutaka kula huku na kule.

            Nimalizie. Leo sitasema mengi. Kwanza, Gwajima anapingana na sera za chama chake. Hawezi kupinga akiwa ndani ya chama. Ajiondoe au akiondolewa asilalamike. Sijui CCM wanambembeleza nini? Pili, Gwajima asilete siasa uchwara kwenye jambo gumu kama mapambano dhidi ya Ukovi-19. Asilete siasa kwenye chanjo. Umma unataka chanjo. Kama yeye ameishachanja ajuako au ana namna yake ambayo hawezi kuiweka wazi iwasaidie wengine, anachofanya ni siasa uchwara. Hivyo, asiruhusiwe kuleta siasa uchwara kwenye chanjo.

Chanzo: Raia Mwema Kesho.

 


No comments: