The Chant of Savant

Monday 23 August 2021

Barua kwa Rais Tuletee Waziri wa Ulinzi Mwanamke

Thandi Modise waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini
Baada ya kufariki aliyekuwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias John Kwandikwa, wizara hii imebaki na pengo ambalo lazima lizimbwe. Kwanza tunatoa salamu za rambi rambi kwako Mheshimiwa Rais, familia na taifa kwa kuondokewa na mwenzetu na kiongozi wetu. Baada ya hapa, tunaomba kutoa ushauri wa bure kwako. Ushauri wenyewe ni juu ya kuomba kipindi hiki katika teua teua yako kuziba nafasi iliyoachwa na Kwandika, tafadhali mama Rais, tuteulie waziri mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa ulinzi ili kuleta si usawa wa kijinsia bali heshima pia na kubadili mazoea ya mfumo dume ambao umetawala tangu tujitawale takriban  miaka 60 iliyopita. Hii maana yake ni kwamba uhuru wetu bado ni mashaka na haujakamilika. Hivyo, unahitaji kukamilishwa kwa kutenda haki kijinsia.
Tangu kupata uhuru, Tanzania haijawahi kuwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwanamke hata naibu wake. Haijawahi kuwa na mkuu wa majeshi au naibu wake mwanamke wala IGP au naibu wake ukiachia mbali mwanasheria mkuu. Hatujawahi kuwa na jaji mkuu au naibu wake mwanamke. Hatujawahi kuwa na waziri wa mambo ya ndani au naibu wake mwanamke. Kwanini sasa tusifanye mabadiliko hasa kipindi hiki kinacholenga kumkomboa mtoto wa kike toka kwenye minyororo na kongwa za mfumo dume? Je ina maana tangu tupata uhuru hatujaweza kuwa na akina mama wanaofaa kuhudumu katika nafasi hizo na nyingine? Je tatizo ni wanawake au mfumo? Kwa wanaojua namna tulivyorithi mfumo wa kikoloni, hawatashangaa kuambiwa kuwa mfumo dume hata kama tulikuwa nao kabla ya kutawaliwa, ni mabaki na makandokando ya ukoloni tena mkongwe na uchwara.
Zifuatazo ni sababu zilizonisukuma kukushauri Mheshimiwa Rais–––kama itakupendeza na kufaa–––ututeulie waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwanamke kama njia ya kuliandaa taifa kisaikolojia kuwaweka kwenye nafasi nyingine nyeti ambazo zimekuwa himaya ya wanaume tangu tupate uhuru:
Mosi, ni kuwatendea haki akina mama na ku-decolonise (sina Kiswahili cha hili) mfumo wetu dume usiotenda haki kijinsia. Ukiachia mbali kutenda haki, kitendo hiki kitawapa mamlaka (empower) waliyonyimwa muda mrefu, kumuinua na kumpa motisha na uzoefu wa kufanya makubwa kama binadamu na raia katika nchi  na jamii yake ukiachia mbali kujenga mazingira na mfumo wezeshi kijinsia na kwa usawa. Kama Rais mwana mama umeweza, atashindwa waziri?
Pili, ni kuwapa fursa ya kuonyesha uwezo wao ili kuondoa dhana ya ujinsia na madhara ya mfumo dume. Nchi ya jirani ya Kenya ina waziri wa Ulinzi Rachel Omamo aliyechukua ukanda toka kwa mwanamama mwingine Monica Juma na mambo yanakwenda vizuri.  Afrika ya Kusini wanaye Thandi Modise ambaye aliteuliwa wiki mbili zilizopita akichukua nafasi toka kwa mwanamama mwingine Nosiviwe Noluthando Mapisa-Nqakula. Na mambo yalikwenda vizuri. Kabla ya hawa wamama wawili alikuwapo Lindiwe Sisulu na mambo yalikwenda uzuri tu. Sudan ya Kusini wanae Angelina Teny huku Kwanini sisi tusifuatie ili kutenda haki kwa wote. Kama kweli tuna nia ya dhati kuleta usawa, kwanini wenzetu watupite hivi hivi wakati tunayo nafasi ya kuondokana na ubaguzi wa kijinsia?
Tatu, tunataka majeshi na idara zetu nyeti zianze kuzoea kusimamiwa na jinsia zote siyo kuleta usawa tu bali pia kujenga mazingira ya kutendeana kwa usawa. Kama mama atakuwa waziri wa wizara hii, hata makamanda hawataona vigumu wala kigugumizi kuwatendea haki wanajeshi walio chini yao bila kujali jinsia iwe kwa kujua au kutojua. 
Kwa vile Tanzania imesheheni wanawake wenye uwezo na vipaji vya kuweza kusimamia wizara hii nyeti, wakati wa kuwaibua na kuwapa nafasi hizo umefika ili waonyeshe na kutumia vipaji vya kwa taifa lao na watu wake. Kuwateua wanawake kushika nafasi ambazo siku zote zimekuwa za wanaume, kunawajenga watanzania kisaikolojia kujikubali kwa maumbile yao ambayo hakuna aliyeandika barua kwa Mungu amuube alivyo bali kuwa kamari ya kuzaliwa na maamuzi ya Muumbaji mwenyewe. Pia ifahamike, kwa kuwateua wanawake kwenye nafasi ambazo zimekuwa himaya ya wanaume, hakutawapa kujiamini na uzoefu wateuliwa tu bali kutatoa motisha kwa watoto wa kike hata wa kiume kujiona wako sawa na wanaweza kufanya kila kitu bila kuzuiliwa kwa kisingizio jinsia zao. Kuna kazi kubwa kama kumtengeza mtoto na kumbeba ukiachia mbali kumtunza hadi anakuwa mtu mzima? Mbona wote tumetokea kwa hao tunaowaona dhaifu?
Tumalizie kwa kukushukuru mama Rais kama utasikiliza ushauri wetu wa bure ambao tumekuwa tukitoa kupitia barua ya wazi kama njia mojawapo ya kuchangia kwenye uendeshaji wa taifa letu.
Chanzo: Raia Mwema Jnne.
Angelina Teny waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini


No comments: