The Chant of Savant

Sunday 8 August 2021

CCM Wamuonyeshe Mlango wa Kutokea Gwajima


Japo lengo la makala hii si kumtetea mbunge wa Kawe-CCM, Josephat Gwajima ambaye hivi karibuni aliibua utata kwa kujifanya bingwa wa virusi au tuseme virologist wakati hana sifa hizo. Gwajima alionekana kwenye mitandao akipinga chanjo ya Ukovi kwa maelezo mepesi na yanayoonyesha kutojua zaidi ya kujua. Alisema kuwa chanjo zinaingilia kwenye vinasaba yaani deoxyribonucleic acid na (DNA), Ribonucleic acid (RNA); na hivyo, kubadili au kuvuruga utu wa mtu jambo ambalo kidogo linashangaza na kuchekesha hasa ikizingatiwa kuwa dunia nzima haiwezi kuwa wajinga kiasi cha kutoliona hili. Kimsingi, hisia na madai kama haya yapo chini ya kile kiitwacho conspiracy theory au nadharia njama. Hata hivyo, Gwajima hakuja na hoja zenye mashiko zaidi ya maelezo tu yasiyoonyesha ukweli wa kile anachodai.

                  Kabla ya kuingia kwenye undani wa kadhia nzima ambayo imezua upotoshaji na utata utokanao na ujanjaujanja na uvunjaji wa haki kimfumo kwa kupitisha watu wasio na sifa kwenye nyadhifa za umma, naomba niseme wazi kuwa kwenye uandishi wangu wa makala ambazo zinaweza kufika hata 5,000, nimekuwa nikiionya Tanzania dhidi ya mambo makuu matatu yafuatayo:

                  Mosi, ile hali na tabia za kuvumilia mafisadi, majambazi na wezi hasa kwa kutopitisha sheria na utaratibu wa kumtaka kila mtanzania aeleze alivyochuma utajiri wake. Hii hulenga kuondoa motisha wa makundi tajwa hapo juu kuuibia umma au watu binafsi. Kwani, kukiwa na utaratibu huu, wengi wa matajiri uchwara na utata tulio nao watapotea na visa vya ufisadi, ujambazi na wizi vitapungua sana. Hapa Kanada, ndiyo utaratibu unaofanyika. Kila mwaka lazima mwananchi au wakazi wa hapa lazima wajaze taarifa zao za kodi ili kuweza kubaini kadhia kama hizi.

Pili,  nimekuwa nikikemea tabia ya watawala kufanya vitu ima kwa kuangalia maslahi yao binafsi, marafiki au karibu bila kujali madhara ya baadaye kama yanayojionyesha kwenye kadhia ya Gwajima. Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi alikaririwa akisema “Sisi umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi kauli zile tunazipinga na kuzilaani kwa sababu utaratibu wa CCM kama mbunge ana jambo lake anapeleka kwenye party cocus (caucus) (kamati ya wabunge wa chama).” Aliendelea “Lazima atambue yeye sio Mungu anayetoa uhai ni Mungu. Tunakiomba chama chetu viongozi wa namna hiyo aachukuliwe hatua kali za kinidhamu na ajieleze kwanini anaongea maneno ya namna hiyo.” Tunashauri UVCCM na CCM wasiishie kulaani bali kumwajibisha mhusika kwa kuwadhalilisha na kupinga na sera zao.

  Muhimu, tujiulize Gwajima ni nani? Kwa ufupi, ni kiongozi wa kujipachika wa kiroho ambaye hutumia nafasi yake kujitajirisha na kufanya mambo ya kisiasa. Anaitwa Askofu wa kikristo ambaye, hata hivyo, uaskofu wake ni wa kujipachika na si wa kufunzwa. Pili, ni mtu anayejionyesha kama msomi mwenye shahada ya uzamivu bila kueleza alivyoipata na akifanya hivyo, ni toka kwenye vyuo vya mfukoni almaaruf diploma mills ambavyo vimetapakaa duniani kwa ajili ya kuhudumia matapeli na vihiyo wasio na uwezo wa kusomea shahada husika kiutaratibu. Wengine waliowahi kujipa udaktari ni kama vile marehemu Getrude Rwakatare na Maneno Tamba. Mmoja alikuwa mchungaji wa kujipachika huku mwingine mganga wa kienyeji. Ni aibu kiasi gani? Kwa wanaojua namna Tanzania inavyozuia kuchanganya dini na siasa, wanajua hapa nani wa kulaumu hasa CCM yenyewe ilipoamua kupinda kanuni na kuruhusu uchanganyaji wa dini na siasa ambao sasa unaanza kuitokea puani. Hivyo, UVCCM, tafadhali rekebisha hilo kabla ya kulaumu matokeo ya makosa ya chama chenu. Japo nakubaliana na msimamo na ushauri wa UVCCM, ila naonya kuwa kosa si la Gwajima. Je UVCCM wameangalia walipojikwaa au walipoangukia?

Tatu, nimekuwa nikikemea tabia ya kuruhusu matapeli, waganga wa kienyeji na wababaishaji wengine kujipa hadhi ya kutumia vyeo vya kitaaluma kama vile Daktari au Profesa bila kuvitolea jasho, kupewa wala kustahiki kama nilivyotaja kwenye mfano wa Gwajima ambaye sijui kama hata hiyo shahada ya kwanza na ya pili anazo ili kuweza kukidhi vigezo vya kusomea, kushinda na kutunikiwa PhD. Kwa tunaojua namna PhD zinavyosotewa, unacheka na kutikisa kichwa ukiwaangalia wanaojipachika kitu hii.  Ni Tanzania na Nigeria ambapo kihiyo yoyote anaweza kujiita lolote kuanzia Daktari, Ulamaa, Askofu hadi Profesa bila kustahiki na asichukuliwe hatua za kisheria. Jikumbushe akina Majimarefu na Vulata waliokuwa waganga wa kienyeji wakajiita maprofesa na hakuna kilichofanyika lau kuwakemea.

Tukirejea ni kwanini nasema CCM wasimuonee Gwajima ila wamwajibishe haraka sana ili kurejesha heshima ya chama na serikali yake haraka iwezekanavyo?

Kwanza, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Je UVCCM wamesahau rafu iliyochezwa Kawe hadi Gwajima kupitishwa kupeperusha bendera yao na kushindishwa? Je CCM wameanza kuona matokeo ya dhuluma waliiyofanya au wanaonyeshwa? Sina haja ya kuwalaumu sana bila kuwasaidia. Nashauri wafanye yafuatayo:

Pili, wamuite kwenye vikao vya chama na kumkaripia au kumfukuza kama wanadhani anachofanya kinakinzani na kanuni na sera za chama. Hata hivyo, kabla ya kufanya hivyo, wakumbuke. Ukimfuga bata, uwe tayari kuvumilia mavi yake. Alipokuwa akifanya maigizo kuwa alikuwa ameparalyse akajiombea na kupona hawakujua kuwa tabia haifi kwa siku moja.

Tatu, wamshauri awe mkweli kuhusiana na sifa zake kuanzia za kidini hadi za kisomi bila kusahau kumkumbusha kuwa anapaswa aache dini atumikie ubunge au aache ubunge atumikie dini. Kwani, siasa na dini hazichanganyiki. Hivi mnadhani Gwajima angekuwa kwenye upinzani angesema anayosema na kuendelea kufanya biashara anayofanya? Haya ndiyo madhara ya wazi ya kuchanganya dini na siasa na kutoa maamuzi yasiyofuata haki kwa upande wa mamlaka. Gwajima ni ushahidi kuwa dhulma hailipi na ujinga ni mzigo hasa kwa wale wanaoamua­­­–––kama taasisi ya umma–––kama chama tawala.

Nne, wamtake Gwajima kuthibitisha madai yake kitaalamu na si kisiasa wala kibabaishaji akishindwa wamuadhibu na pia kumlazimisha kukana kauli zake ambazo aeleze wazi si za kitaalamu nani za kupoteza na kutafuta ujiko rahisi.

Tano, CCM wajiepusha kulindana na kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Badala yake watumie makosa haya kama fursa ya kurekebisha mambo na makosa waliyotenda bila kuangalia mbali. Hii itasaidia kuondoa kadhia ya matapeli na wababaishaji wengine wanaotumia mianya ya kujikomba kwa viongozi au vyama ili kulinda jinai zao na kutafuta ulaji na ujiko wa haraka bila stahiki. Kimsingi, pamoja na Gwajima kustahiki lawama kwa upotoshaji wake kuhusiana na chanjo, CCM wanastahiki lawama zaidi kwa kukubali na kujirahisisha kutumiwa kisiasa wasijue madhara yake ya baadaye kama wanavyoanza kuyashuhudia sasa.

Mwisho, Gwajima–––kama kweli anamaanisha na kusimamia anachoamini–––hana haja ya kulumbana au kupingana na serikali yake. Kwa mtu mstaarabu na mwelewa, alipaswa kuyasema aliyosema akiwa ameishaachia ngazi kuanzia ubunge hadi uanachama. Nadhani, umefika wakati wa kuwatahadharisha CCM na wanasiasa wake wa aina ya Gwajima kuwa wakati wa kufanya mambo kwa mazoea ushapita sana. Tunawachelewesha wananchi ukiachia mbali kujiaibisha na kuaibisha taifa letu. Hapa niseme wazi. Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais, anangoja nini kumuonyesha mlango Gwajima ili liwe funzo na onyo kwa wengine wanaokurupuka? Ni ushauri tu. Kutofanya hayo, jamani mtakuwa mkimuonea Gwajima na kuendelea kujidhalilisha ukiachia mbali kujipinga na kujichanganya. Fanyeni mapinduzi kama lilivyo jina lenu. Na yawe ni ya haki na kwenda mbali lakini si kurudia makosa kama haya.

Chanzo: Raia Mwema.


No comments: