Mpendwa rais, kwanza, nikiri. Naandika waraka huu nikiwa nimevaa kofia nne. Kwanza, ni mwandishi wa habari. Pili ni mchambuzi. Tatu ni mwandishi wa vitabu zaidi ya 20. Nne ni msomi wa kiwango cha kimataifa. Hivyo, kwangu, kufungiwa kwa gazeti la Uhuru linalomilkiwa na kuendeshwa na Chama tawala baada ya kuandika ‘uongo’ kuwa huna mpango wa kugombea urais mwaka 2025, licha kuonyesha sheria inavyotumika bila upendeleo, linatoa dukuduku, funzo, maswali na onyo kwa umma ukiachia mbali wengine waliozoea kufanya mambo kwa mazoea wakijua watalindwa.
Mpendwa rais na Mwenyekiti wa CCM, pamoja na kukipongeza chama na serikali yako kutojipendelea, tunaomba tutoa machache kuhusiana na kadhia hii tekenyeshi na pumbazika. Lengo la waraka huu wa wazi kwa Rais si kuikosoa serikali za awamu zilizopita ambazo zilijenga aina fulani ya kujipendelea huku likiwaumiza wengine. Kufungiwa kwa gazeti tajwa kunatoa masomo kadhaa kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla. Lengo la barua hii ya wazi kwako ni kuibua maswali mengi ili kuweza kutafuta majibu mengi kadhalika mbali na kuonya kuwa kunaweza kukawapo zaidi ya uongo hata ukweli katika hiki kilichosababisha 'kufungiwa' na si kufungwa kama wengine. Je Uhuru lilipaswa kufungiwa au kufungwa? Hilo nawaachia nyinyi hasa wewe bosi na kiongozi wao.
Mosi, wote tujue na kukubali kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Japo katiba yetu iko wazi kuhusiana na hili, siku zilizopita kulikuwa na watu wachumia tumbo, wasaka tonge na makanjanja tena wasiojulikana hata walikokua wameibuka kujifanya wako juu ya sheria baada ya kujitokeza na kujipendekeza kama watetezi wa wakubwa. Nadhani wengi tunamkumbuka mmoja aliyejipachika cheo cha kumtetea rais ambaye hata hivyo, baada ya kuondoka utawala wa awamu ya tano naye ametoweka kinamna. Unawezaje kumtetea rais ambaye ana wasemaji tena wanaolipwa kwa kodi za umma? Je rais anahitaji watetezi wakati ana washauri kibao wa kisheria ukiachia mwanasheria mkuu? Kwa wanaojua madhara ya vidhabi haya waliyowasababishia madhira watu wasio na hatia tena wengine watu na heshima zao, tungeomba sasa hivi wachunguzwe hata kufikishwa mahakamani. Wachunguzwe walipata nini kutokana na kujipendekeza kwao na kwanini walikuwa wakifanya upuuzi walioufanya na nani alikuwa akiwafadhili. Tuwachunguze na kuwashughulikia ili liwe somo kwa wengine wanaopanga kutumia njia kama hizo kuwaumiza wengine kumbe ni wachumia tumbo na wabangaizaji na matapeli wa kisiasa.
Pili, sina shaka CCM ima wamenusa namna wewe kama rais na mwenyekiti wao hutaki upuuzi–––wala hauko tayari kuwaumiza wengine kwa kuwaendekeza wanaojikomba–––wakaamua kujiwahi ili wasiumbuke wala kuwa sehemu ya wale watakaoumbuka kama taasisi. Pia hili linaweza kutafsiriwa kuwa rais hayuko tayari kufuga wala kuendekeza makundi ya kimaslahi ya kifisadi chamani hata kama wanamuimbia mapambio. Kwa hili pia tunawapongeza kwa kusoma alama za nyakati badala ya kungoja wasomewe na wengine. Nadhani hili ni somo kuwa wameanza kubadilika badala ya kungoja kubadilishwa.
Tatu, je kuna watu wanataka kupima maji mapema ili wajiandae kugombea hasa ikizingatiwa kuwa CCM–––pamoja na kusambaratishwa mitandao yake ya kimaslahi na Hayati Dkt John Magufuli–––si kwamba ilikufa. Je siasa za makundi za CCM zinaanza kurejea na kuanza vita ya kugombea madaraka hata kufikia kukulisha maneno? Je hawa wanakupima au kukutisha kama siyo kukupeep na sasa umewapigia japo wapambe wao? Je wanapata wapi jeuri ya kufanya hivyo wakati wakijua una marungu mawili la chama na la serikali? Je kuna watu waliowatuma walioandika ‘uongo’ juu ya kutogombea au kugombea kwako ili wajihakikishie fursa ya kuanza kupanga mikakati ya kutaka hayo madaraka uliyo nayo? Je hawa ni akina nani na wafanywe nini? Je waandishi walishindwa kutafsiri maneno yako uliposema kuwa hukuwa na mpango wala ndoto za kuwa rais kabla ya kuwa rais lakini wakasahau kuwa sasa wewe ni rais na pia na mwanasiasa tena siyo wa tangu juzi wala jana ambaye umeishaonja madaraka kamili baada ya kukaa kimya ukiwa makamu tu? Je hawa waliowatuma waandishi–––kama kweli wapo–––walijiamini nini hadi wakamkosea adabu rais hivi hivi? Je waandishi na wahariri walipewa nini hadi wakaweka kazi zao hatarini? Je CCM imejifunza nini katika kadhia hii ya aibu?
Mpendwea rais, nne, nadhani wewe Samia Suluhu Hassan, kama rais na mtanzania yeyote una haki ya kugombea hata kutogombea kama uonavyo na utakavyoona. Hivyo, kusema hutagombea si kosa. Kosa ni kusema kitu ambacho hujasema. Ni kosa kubwa. Hata mumeo ambaye ni ubavu wako hawezi kukusemea kwani siyo itifaki wala stahiki kwa namba moja wa nchi. Isitoshe, kwa namna unavyochapa kazi na ukitumia na rekodi yako iliyokupaisha hadi ukateuliwa makamu wa rais, una kila sifa na sababu za kugombea. Rejea ambavyo, kwa mara ya kwanza Tanzania imeweza kuuza bidhaa nyingi kwa Kenya kuliko inazoagiza toka huko. Badala ya kukukatisha tamaa, kukuzushia na kukulisha maneno, ningeshauri wakushauri ugombee–––kama ilivyokuwa kwa bonge la kaka, ukiokoe chama chako kudondoshwa na wapinzani. Hata hivyo, uhitaji gazeti kukusemea kana kwamba huna mdomo wala ubavu na ithibati ya kusema hivyo. Cha mno tunachojifunza hapa ni kwamba umeonyesha usivyotaka kuruhusu watu kuanza kupoteza muda na hata fedha vya umma kwa kujiingiza kwenye kampeni kabla hata ya muhula wa kwanza haujafiki hata nusu yake. Hili liko wazi. Umesema unataka kuisimamisha nchi ili kuleta maendeleo na kutimiza yale yote uliyorithi tena toka kwa awamu uliyokuwa kiongozi wake namba mbili. Nadhani hili ni onyo na tangazo kwa wanasiasa kuwa hakutakuwa na siasa hadi kwanza kazi iendelee na kufanikiwa.
Tano, wale waliokuwa wakiituhumu serikali kuwa inaminya uhuru wa vyombo vya habari, sasa wataanza kung’amua: kumbe kinachobanwa si uhuru wa habari bali kutaka uhuru huu usiwe wa kila aliye nao kujifanyia atakavyo. Na akifanya hivyo, ajue sheria ni msumeno na mwenye kuisimamia ameishaonyesha wazi yuko tayari kuiruhusu imkate yeyote atakayekuwa ameivunja awe mbele au nyuma serikalini, chamani au upinzani au nje. Nani alidhani gazeti, tena, la chama tawala lingefungiwa kwa kuandika ‘umbea’? Je kweli liliandika umbea au kuna namna? Je hawa watakaoandika uchochezi wategemee nini hapa?
Mpendwa Rais, nimalize kwa KUKUSHAURI BURE kuwa siyo kufungia gazeti tu bali uangalie ndani zaidi hasa kwenye chama chako hata serikali yako kujua ni kwanini haya yameanza hata kabla hujatimiza hata siku 200 madarakani. Maana, wahenga walisema mwanzo wa ngoma lele; na isitoshe, akumulikaye hukuchoma. Hivyo basi, kusimamisha gazeti na watendaji wake hakutoshi. Lazima wabanwe waeleze kila wanachojua ili kuepuka kuitia nchi kwenye sintofahamu bila sababu au na kama kuna hujuma tujue ili tuchukue hatua. Maana haiwezekani gazeti la Chama kinachounda serikali likajiandikia ‘uongo’ kuhusiana na bosi wa vyote yaani mwenyekiti wake na rais nchi na mkuu wa serikali ya chama chenyewe. Ili iweje na kwanini?
Mwisho kabisa, sina haja ya kuamini kuwa waandishi walifanya kazi yao vizuri na sasa wanatolewa sadaka. Hii staili yako ya kuongoza. Hili halimo kwenye darubini yangu. Lazima kuna zaidi ya kukusingizia hata kukushinikiza au kukuchimba ili wanaokimezea kiti chako wapate namna ya kukushughulikia kulhali. Kimsingi, walichoandika Uhuru si uongo kama walivyoadhibiwa kwao bali hujuma na njama vya hali ya juu. Pia, siamini kuwa wametolewa kafara. Hata hivyo, haya ni maoni na mawazo yangu kama mchambuzi. Je Gazeti la Uhuru Wamepotoka au Kuna Mengi Tusiyojua? Nikushukuru kwa kunisoma. NIKUSHUKURU ZAIDI kama utaufanyia kazi ushauri wangu. Kila la heri.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment