The Chant of Savant

Tuesday 12 July 2022

Dini zinapogeuka janga (IV)

Katika muendelezo wa makala iliyopita juu ya unyonyaji na hujuma kiuchumi uliojificha nyuma ya dini au imani, leo tunadurusu ndani kwa baadhi ya wenzetu ambao, kama mabwana zao wa kiimani, nao wamegeuka wakoloni na wanyonyaji wapya. Hawa si wengine bali wachungaji au viongozi wa kidini wa kujipachika. Biashara hii ya kujipachika vyeo vya kidini imekua sana hasa kwenye ukristo ambapo wahusika ima hujipatia umaarufu au utajiri. Siku hizi, wachungaji matapeli (wachunaji) na waganga wa kienyeji wanatengeneza fedha kwa kuibia wajinga wetu wengi waliokata tamaa.

Wapo wanaowaahidi wateja wao miujiza wakati hakuna kitu kama hicho au utajiri wakati wenyewe ni maskini wa kunuka. Hakuna njia ya kuwasaidia hawa kama kufichua uovu ulioko nyuma ya dini zinazotumiwa kama njia ya kuwaibia na kuwanyonya kwa kuwaahidi uongo na mambo makubwa vyote visivyokuwepo. Watu hawa matapeli wamewaganya na kuwaibia watu wengi. Wengi wamepoteza hata maisha baada ya kuingizwa kwenye ushirikina huu wa kiroho ukiachia mbali waliojeruhiwa kimaisha. Kimsingi, matapeli hawa hawana tofauti na waganga wa kienyeji au wapiga bao au wababaishaji wengine ambao wengi wao ni wavivu wa kutafuta riziki kwa njia zinazoeleweka. Ni bahati mbaya kuwa hata nchi nyingi za Kiafrika zimeruhusu upumbavu huu kwa vile unawapumbaza watu wake wasiweze kupinga maovu mengi ambayo serikali zake huwatendea watu wake. Kimsingi, utapeli wa kiroho ni sawa na wa kisiasa ambapo wanasiasa waongo huwaahidi wapiga kura vinono kumbe lengo ni kuwatumia kupata ulaji wao binafsi.

 Kimsingi, mfumo wetu ni wa kikoloni na kiharifu unaoruhusu uhalifu kama huu. Kwa vile nao unaufanya na unautumikia kuendelea kuwapumbaza na kuwaibia walio wengi ambao ndiyo injini ya maisha ya mifumo. Hiyo. Yote hii inafanyika chini ya kivuli cha imani. Rafiki yangu na msomi maarufu toka Zimbabwe Profesa Munyaradzi Mawere aliwahi kusema kuwa “imani haitwambii nini cha kuamini bali hutuambia namna ya kuamini.”  Japo napingana naye juu ya nin cha kuamini kwa vile dini hutuambia tuamini ‘ukweli’ wake kwa kuua ukweli mwingine, nakubaliana naye kuwa dini hutuambia namna ya kuamini. Mbali na hiyo, dini hutufanya tusifikiri kwa vile zinaweza kufikiri kwa niaba yetu. Kwa maslahi yake siyo yetu.

Hakuna kitu kinakera kama kutegemea uvivu kuleta maendeleo wakati kazi pekee tena kwa kutumia maarifa ndivyo hakikisho la maendeleo na ufanisi. Huwezi kuleta mabadiliko wala maendeleo kwa imani bali matendo. Pia, matendo husika lazima yatokane na uhalisia na siyo utopia au ndoto au imani. Leo wapo watu wanawekeza kwenda peponi wakati wakiishi kwenye jehanamu hapa duniani.  Je kipi bora kwako, kile unachoweza kukifikia au kile usichoweza? Kwanini pepo iwe muhimu leo wakati hujaifikia? Kwanini pepo iwe muhimu wakati ahitatajiki kwa sasa? Hebu fikiria serikali zetu zingewaza kipepopepo, unadhani zingeweza kutimiza wajibu wake wa kutoa huduma, kuhakikisha usalama wa watu na mipaka yake na kuleta maendeleo? Biblia inasema kuwa utawezaje kumpenda Mungu asiyeonekana wakati unamchukia jirani au ndugu unayemuona? Unawezaje kuvuka daraja kabla ya kulifikia? Je ni wangapi wanazingatia haya au kuyadurusu zaidi ya kutafuta vya dezo. Leo watu wanaomba mvua wakati wamezungukwa maziwa, miti na mito. Wanataka waone miujiza wakati kila siku wanaishi miujiza. Hivi bustani, mashamba, misitu na hata ndoa siyo miujiza? Unapanda mbegu moja na kupata nyingi. Je ni miujiza gani hii tunayoaminishwa ipo wakati tunaiishi na ni matokeo ya miujiza? Je ukulima na uzazi siyo miujiza? Wengi wanadhani Mungu ni mvivu wa kufikiri kama wao. Unataka mvua gani wakati una maji yanayopaswa kutumia akili kuyachota au kuyavuta na kumwagilia?

Ni wangapi wanaaminishwa kuwa wakiamsha mikono na kuomba Mungu atafanya ‘miujiza’ wakati washaambiwa kuwa bila kutoa jasho hupati kitu na asiyefanya kazi na asile? Ni mafanikio gani wakati walishapewa ubongo wa kufikiri na kung;amua na kutafuta majibu ya matatizo yao kwa kutumia ubongo? Wanataka miujiza gani wakati akili ni muujiza wa kutosha uliofanya binadamu wawe tofauti na wanyama japo ni waharibifu wa dunia yetu tokana na upofu, upogo na uroho na kutoona mbali? Wangapi wanakesha wakiomba lakini hawashindi wala kukesha wakichapa kazi? Wangapi wanategemea tunguli kuwalinda wakati anayewapa tunguli haitumii? Wangapi wanaaminishwa kuwa kuomba kunaweza kuwalinda wakati wanaowaaminisha hivyo wamezungukwa na walinzi wenye mabunduki? Je papa hategemei walinzi badala ya Mungu anayemhubiri? Je hapa tatizo ni nini zaidi ya kushindwa kutumia akili barabara? Huwezi ukaacha kupalilia shamba lako ukategemea miujiza kuyaondoa. Huwezi kuweka kikombe cha chai au ugali mezani halafu ukaomba Mungu afanye miujiza viingie kinywani mwako wakati ushapewa mikono. Mungu hajipingi na hana uvuvi huu wa kufikri. Pamoja na chai au ugali kuwa mbele yako, kama hutainua mkono na kuchukua kikombe au kumega ugali utakufa njaa au kwa kiu.  Huwezi kuona simba akikunyelea kukugeuza kitoweo ukapiga magoti ukidhani Mungu atakuokoa wakati alishakupa macho na miguu au mikono ya kupamba na simba. Utakufa ukijiona kama ambavyo watu wetu wengi wamegeuka maskini wakijiona. Wamekata tamaa wakijiona wakati wakiaminishwa kwenye miujiza ili kuwakwepesha kutumia akili na kuwabaini wezi hawa wa imani wanaowapotezea maisha na muda huku mamlaka nazo zikiangalia kana kwamba si kazi yake kuwaelimisha na kuwaepusha na ujuha huu wa kimfumo na halaiki.

Leo tunaishia hapa tukitafuta muda kudurusu yatakayofuata kwenye sehemu ya tano.  Kwa ufupi, ni kwamba dini zimejitahidi kututawala kila upande kuanzia kisiasa, kiuchumi, kijamii hata kiutamaduni. Tukipata muda tutaongelea madhara ya kuapisha viongozi wetu wa kiafrika kwa imani za kigeni. Wakiashindwa kuwa watiifu kwetu tunaanza kulaumu tusijue chanzo ni mifumo.

Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: