Hivi karibuni, kama alivyowahi kufanya Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliandika barua kwa watanzania na dunia juu ya demokrasia ya vyama vingi. Japo aligusia masuala mengi kama vile historia ya vyama vingi, hali ya kisiasa barani Afrika tangia wakati ule na wakati ule, kuna mambo hakuyaweka wazi.
Leo katika kuidurusu barua ya Rais, tutaangalia mambo manne aliyopa kipaumbele. Rais aliandika “ni busara ya Mzee Mwinyi na viongozi wenzake wa wakati huo walioamua kusikiliza wachache. Kama wazee wetu wangesubiri mpaka asilimia 80 itake vyama vingi ndiyo tukubali, pengine leo tusingekuwa tulipo.”
Tukiwa wakweli, je viongozi wetu walifuata busara au mawazo na utashi vya wananchi au tume zile zilikuwa ni danganya toto zikiendeshwa na amri za wakubwa walioziteua? Je uwepo wa vyama vingi ni mawazo na utashi wetu au ghilba ya viongozi wetu wakiitikia amri za wafadhili wa serikali zao? Je ni kweli kuwa tuliingia kwenye mfumo wa vyama vingi kwa busara za viongozi wetu, utashi wetu au siasa za kidunia (realpolitik) ukiachia mbali kulazimishwa na nchi wafadhili?
Kwa wanaojua historia ya mfumo wa sasa wa dunia, vyama vingi vililazimishwa kwa nchi za Kiafrika. Ndiyo maana, hadi sasa, nchi nyingi zimeviua kinamna ikiwamo Tanzania. Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu na wenzetu–––––tukijua wana akili timamu kama sisi––––kweli Tanzania tuna vyama vingi utawala wa chama kimoja kinachotumia uwepo wa vyama vingi visivyoweza kukiondoa madarakani? Je tunayo demokrasia bora na inayoridhisha au bora demokrasia ya kujiridhisha?
Je Tanzania tuna vyama vingi vyenye kukidhi matakwa ya kidemokrasia au bora vyama vingi? Je tunayo mazingira wezeshi au mazingira angamizi kidemokrasia ukiachia mbali ubabaishaji kisiasa? Je serikali inavitenzaje na kuvitendeaje vyama vya upinzani ikilinganishwa na chama tawala? Je Tanzania inatawaliwa kidemokrasia kweli, kinadharia au kivitendo? Unaweza kuwa na utitiri wa vyama vingi lakini ima vya hovyo au goigoi kama ilivyo nchini. Je wingi wa vyama ndiyo demokrasia? Mbona Marekani na Uingereza zina vyama vya maana vya kisiasa viwili? Kama utiriri wa vyama ndio demokrasia, kwanini walimu wetu wa demokrasia hawanavyo? Nchini DRC zama za jambazi Joseph Mobutu ilikuwa na vyama vingi alivyokuwa akivifadhili ili kuwadanganya wakongo kwa kushibisha matumbo ya wenye vyama. Je vyama vyetu ni vya wanachama au ni vya mifukoni kwa faida ya viongozi au waanzilishi wake? Je hapa nani wa kulaumiwa? Je wananchi, viongozi na serikali hawabebi lawama ya kuvurugika kwa demokrasia nchini? Tumefanya nini kama wananchi, viongozi hata binadamu?
Rais anamkariri imla wa zamani wa China, Mao Zedong akisema “Acha maua 100 yamee kwa pamoja.” Kama maua ni vyama, na bila shaka ndicho alichomaanisha Mheshimiwa Rais, je maua ya Tanzania yanakuwa pamoja au ni ua moja yaani CCM lililopewa mbolea na maji huku mengine yakinyimwa na kuliacha likue na kuyafunika mengine (vyama vya upinzani)?
Sasa ngoja tudurusu vipaumbele vya Mheshimiwa Rais. Anaandika “ndiyo sababu kwenye uongozi wangu ninaamini katika kile kinachojulikana kama 4R – ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconcilation (Maridhiano), Resiliency (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya).”
Kuamini na kutenda ni vitu viwili tofauti. Wengi walidhani Mheshimiwa Rais angesema, katika uongozi wangu nashughulikia 4R. Sina ugomvi na imani pia sina imani na imani. Wangapi wanaamini katika dini lakini wanafanya mambo ya kishetani? Pia, sina nia ya kupingana na Rais wangu bali kuboresha.
Kimsingi, Mheshimiwa Rais alipaswa kufafanua namna ambavyo atafanikisha hizo 4Rs. Anaposema anaamini katika maridhiano anamaanisha nini? Je atayafanya vipi na lini na yatafanywa na nani na baina ya nani na nani? Je ana mpango wa kuunda tume ya maridhiano? Je nini matokeo yake kisheria hasa kwa wale waliokosewa au kudhuriwa na mgogoro unaolazimisha yawepo maridhiano? Maana, huwezi kuwa na maridhiano bila ya kuwepo mgogoro na waathirika na sababu zake.
Mheshimiwa Rais anaongelea ustahamilivu. Je ni ustahamilivu wake au wa wahanga wa mgogoro hasa wa ukosefu wa demokrasia na haki sawa katika kufanya siasa? Nani anamstahamili nani au nini? Je nini njia ya kuondoka kwenye sintofahamu kama hii? Je serikali yetu ni stahimilivu hasa tukizingatia namna 'ilivyoshughulikia upinzani' hadi ukaambua patupu kwenye uchaguzi uliopita? Je wapinzani na wakosoaji wanauona huo ustahmilivu? Je umeanza lini? Futeni kesi zote zinazowakabili wapinzani na kuacha kuwabeba wanachama wao waliowatimua kama ilivyo kwa wale waitwao Covid-19.
Mbali na hayo hapo juu, Mheshimiwa Rais anaongelea mabadiliko. Mabadiliko katika nini? Nini kinahitaji mabadiliko na kwanini? Nani alisababisha ukale wa kitu hiki hadi kihitaji mabadiliko au marekebisho? Je kuna mabadiliko au mwendelezo wa yale yaliyosababisha demokrasia ya vyama vingi iwe kiini macho, changa la macho au utani nchini? Je Mheshimwa Rais ana mpango wa kufanya mabadiliko yapi na kwa ajili ya nani?
Mwisho, Mheshimiwa Rais anaongelea kujenga upya. Je ni kipi kinajengwa upya na kwa namna gani? Je imefanyika tathmini ya kujua ni kipi kilichobomoka na kwa kiasi gani na nani ana au nini kinahusika? Je sababu za kubomoka kwa hiki kinachopaswa kujengwa upya zinaeleweka ili kutafuta namna ya kuepuka kuzirudia? Je hawa waliosababisha ubomokaji au umomonyokaji watapewa adhabu gani? Je waathirika wa kadhia hii watafidiwa au la? Kama watafidiwa, ni vigezo gani vitatumika? Kama hawatafidiwa, ni kwanini?
Maswali haya ni muhimu kama tutazingatia kuwa kuna watu walifungwa au kuteswa tokana na kufanya mambo ambayo––––kwenye demokrasia ya kweli––––ni haki yao. Mfano, waliokamatwa na kushitakiwa na kufungwa kwa kuandamana, kupoteza wapendwa wao waliopigwa risasi na kufariki wakati polisi wakizuia maandamano ya kupinga ukandamizaji wa serikali. Nadhani Mheshimiwa Rais alisahau R nyingine, yaani Realism au Uhalisia wa hali halisi ili aweze kutatua matatizo kisayansi na kivitendo na si kinadharia kama dira na lengo vyake vinavyoonyesha. Je Mheshimwa Rais anamaanisha tofauti zaidi ya hapo sema hajapata blueprint ya kile anachokiwazia, kudhamiria au kumaanisha?
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment