The Chant of Savant

Saturday 16 July 2022

Taifa linapaswa kuambiwa siyo kuombewa tu

Na Nkwazi Mhango, Kanada
Hivi karibuni Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria, Zephania Ntuza aliogoza ibada ya ‘kuliombea’ taifa ili liondokane na uhalifu kama mauaji yanayozidi kulipotiwa na vyombo vya habari mbali mbali nchini na hata nje ya nchi. Ntuza alikaririwa akisema “siyo sifa kuona matukio ya mauaji yakiripotiwa katika jamii huo siyo utamaduni wetu watanzania na watu tunaomwamini Mungu. Ni wakati sasa jamii inatakiwa kufunga kwa maombi kwa ajili ya kukemea mauaji hayo.” Japo sina ugomvi na imani katika kufunga na kuomba, sina imani na imani na maombi tu kama njia mujarabu ya kupambana na tatizo. Pia, sijui kama kuna taifa lenye utamaduni wa kuuana japo ukombozi katika Ukristo unatokana na mauaji ya mtu asiye na hatia.
Pamoja na nia nzuri ya Askofu, lazima tukubaliane kuwa kuomba hakutasaidia chochote zaidi ya kujipa matumaini yasiyokuwepo kama hatutachukua hatua kivitendo. Tumepewa akili na viungo vingine ili kuvitumia kutatua matatizo yetu badala ya kungoja Mungu au miujiza yake kutatua matatizo yetu. Mungu alijua kuwa tunahitaji akili, maarifa na viungo vya kutendea kazi badala ya kujifungia kwenye kumuomba. Atupe nini zaidi ya akili? Aingilie nini wakati hatujipi fursa ya kujaribu kutatua matatizo tuliyosababisha wenyewe kwa kutumia akili kama jamii ya Watu japo tumeanza kuwa hatarishi kuliko hata hayawani? Dini zimekuwepo hasa hizi nyemelezi za kigeni tangu ulipoingia ukoloni. Je zimefanya nini zaidi ya kutujaza imani huku tukiendelea kuwa maskini mbali na Waafrika kuwa binadamu wa kiwango cha chini mbele ya rangi nyingine kiasi cha kubaguliwa na kuchukiwa tu kwa sababu ya rangi yetu?
Kuomba si jambo baya. Hata hivyo, huwezi kuomba baada ya kufanya uzembe mahali fulani na Mungu akasikia maombi yako. Si mjinga kiasi hiki wala hajipingi. Ameishakupa akili na talanta mbali mbali. Usipozitumia, hata ukikesha ukifunga, kusali na kuomba hatakusikia wala kukusaidia. Sana sana atakuadhibu kwa kosa la uzembe na kutotumia akili vilivyo. Msomaji wangu aitwaye Mtwangio aliwahi kunipa kisa kimoja kuhusiana na kuomba. Anasema kuwa katika kinyang'anyiro cha mashindano ya kombe la dunia la mpira wa miguu ya mwaka 1982 yaliyofanyika Uhispania ambapo nchi ya Poland iliyashiriki, viongozi wa timu hiyo na wachezaji wake waliamua kwenda kumuona Papa John Paul II, Mpoland mwenzao ili awaombee kwa Mwenyezi Mungu walitwae kombe hilo la dunia katika mashindano hayo. Papa aliwajibu kwamba "katika mpira wa miguu Mwenyezi Mungu hapendelei timu yoyote. Je hapa busara ni nini? Kiufupi ni kwamba licha walichoomba kutowezekana na kutokuwa na sababu zaidi ya ufundi uwanjani, aliwataka watumie akili.
Kwa sasa, nchi za kiafrika zina utitiri wa matapeli wa kiroho waliochipachika vyeo vikubwa na vitukufu wakati ni wezi wa kawaida walioshindwa utukutu na ubunifu kupambana katika maisha na kuamua kuwaibia wajinga na watu waliokata tamaa ambao nao wamekataa kufikiri na kutafuta majibu ya matatizo yao. Yapo mambo unaweza kumuomba Mungu kwa wale wanaoamini. Ni yale ambavyo binadamu huna uwezo navyo mfano kitakachokutokea kesho, majanga ya kimaumbile na mambo mengine ambayo yako juu ya uwezo wako. Hili la uhalifu lipo chini ya uwezo wetu kama taifa na jamii ya watu kama tutafuata kanuni za kupambana na kadhia hizi kisayansi na si kiimani kama Ntuza na wengine kama yeye wanavyotaka kutuaminisha.
Tunaweza kukubali kuomba. Je lisipopatikana jibu––––ambalo sina wasi wasi halitapatikana––––tutafanya nini? Je tatizo litakuwa liko pale linatungojea tundelee na ubabaishaji huu? Mbona Tanzania kila Jumapili (kwa wakristo) na kila siku (kwa waislam na waumini wa dini za asili) linaombewa sana tu? Nadhani hapa tuna tatizo la kisaikolojia.  Tangu niishi hapa Kanada karibia miaka 20, sioni wazungu wakitumia sala kutatua matatizo yao. Kuna miji kama vile St. John’s NL makanisa mengi yamefungwa kwa kukosa waumini huku mengine yakitumiwa na wazinzi usiku majira ya joto kufanyia ufuska. Kwa wenzetu hili si tatizo. Taifa lao ni tajiri tu na shida yao siyo ukosefu wa usalama. Kwa muda niliokaa mji ule, nilishuhudia watu wakilala bila kufunga milango tena bila wasi wasi wowote. Unadhani hawa wazungu ni malaika? Hapana, wana uhakika wa kula. Serikali yao, badala ya kuomba, iliondoa matatizo ya umaskini na ujinga ambavyo ndivyo vyanzo vya ushirikina na uuaji tunavyoshuhudia nchini. Wakanada sasa wameshiba kiasi cha kukufuru wakihanganaishwa na ‘haki’ za hovyo kama vile ushonga, usagaji, uvutaji bangi na mengine kama hayo.
Tumalize kwa kusema kuwa taifa letu linahitaji kuambiwa ukweli na si kuombewa. Liache kutumia ndoto za alinacha kutatua matatizo. Kufanya hivi ni kuishiwa na kuendelea kukuza matatizo bila sababu zaidi ya uzembe na vipaumbele. Haya hayahitaji kuwa na shahada ya uzamivu katika mipango wala kupambana na jinai.
Pili, hawa wanaoamini katika maombi inapaswa waelezwe wazi kuwa tumpewa serikali ili isimamie sheria kujitatulia matatizo yetu kama yote kuanzia ya kibinafsi hata ya kijamii. Je serikali, ambayo inazidiwa na wauaji wachache inatimiza wajibu wake wa kutekeleza sheria? Hapa tatizo liko wapi? Mbona wakati wa awamu ya tano upuuzi huu uligeuka historia? Je ni wapi Jeshi letu la polisi limezembea au serikali kuwa legelege? Je tunahitaji kuiombea serikali na jeshi la polisi au kuwaambia kuwa kuna vitu vinaenda ndivyo sivyo? Tutaombea mangapi? Ukitokea ufisadi ambapo tunashuhudia mafisadi wakiachiwa huru au kufutiwa kesi hivi hivi tuombe kweli au kulalamika? Zikitokea ajali za barabarani zitokanazo na uzembe tuombe! Ukitokea ukame baada ya kukata miti sana tuombe! Mimba za utotoni zikizidi tokana na kuporomoka maadili, tamaa, ujinga, umaskini, ufisadi na upuuzi mwingine tuombe!
Chanzo: Raia Mwema Juzi

No comments: