Wakati akfiungua barabara ya Afrika Mashariki (Arusha bypass) jijini Arusha, Mheshimwa Rais ulisikika ukilalamika kuwa wananchi wanaharibu miundo mbinu. Ulikaririwa ukisema “niwaombe sana ndugu zangu kufuata taratibu zilizowekwa ili tuendelee kutunza miundombinu yetu, iendelee kutukuzia uchumi wetu.” Mhe. Rais, hapa hakuna cha kuomba wala kubembeleza bali kutoa amri, tena kali na kavu kavu kweli kweli ili kufikisha onyo kali na ujumbe. Kama utafanya hivyo, wote wataelewa kuwa sasa hakuna mchezo wala utani amini nakwambia. Rejea namna kaka la nguvu, mtangulizi wako Hayati John Magufuli alivyozoea kutoa amri na vitisho bila kujali vingetafsiriwa vipi na wabaya wake. Na kweli, alifanikuwa kuitia nchi adabu kwa muda mfupi alioongoza kutokana na staili yake ya utawala. Hakuogopa kulaumiwa wala kuona aibu. Kama wao hawapendi wala kuonea huruma miundombinu yetu ambao ni yao au kuonea aibu vitendo vyao, kuna haja gani ya kuwaonea aibu au huruma? Hapa ni jino kwa jino, nipe nikupe, piga nipige, fanya nifanya, anza nimalize. Bila kuwa wakali, tutaendelea kupoteza fedha na muda wakati dawa yake ni rahisi.
Mhe. Rais, japo sitaki umuige kwa ku-copy na ku-paste, nina kila sababu tena nuzuhu kukujuza kuwa, wakati mwingine mambo hayendi. Tulishaambwa na wahenga kuwa mti hauendi ila kwa nyenzo. Kadhia ya uharibufu wa miundombinu ni mti wako halahala na macho. Lazima tuonesha kuudhiwa na kadhia hii bila kujali kama wanaoitenda ni watu wetu wa karibu au mbali. Mfano, inapoharibiwa miundo mbinu, lazima tuwe na uwajibikaji wa pamoja kulingana nani wanawajibika na miundombinu husika.
Mhe. Rais ili kuondokana na kadhia hii ya kujitakia, kama jamii na taifa, tunapaswa, kwanza, kutunga sheria za kushughulikia hujuma hizi kama hazipo. Kama hatuna sheria za kushughulikia uarifu huu, tutakuwa tumechelewa sana. Kimsingi, sioni aibu kusema wazi kuwa, kwa kuendelea kushindwa kukomesha kadhia hii, serikali na wananchi kwa ujumla tunakuwa washiriki katika kuitenda. Hivyo, tuna hatia ya pamoja.
Pili, Mhe. Rais, kama sheria zipo au zitatungwa, tunapaswa kuzisimamia vilivyo bila cha mswalie Mtume wala nini. Hapa lazima tutunge sheria kali zenye kutoa adhabu kali kwa waharifu na hata wanajamii ambao ni washirika katika uharifu huu. Tuwajulishe wananchi kuwa kunyamazia au kuficha waharifu ni kujifanya mshrika wa uharifu huu ambao ni kinyume cha sheria. Hii ndiyo kazi yako na serikali yako. Una uhalali wote wa kufanya hivi. Najua, kama utaamua, unaweza na vitendo hivi vitageuka historia kama ilivyokuwa wakati wa awamu ya tano ambapo nchi ilinyooka na kusahau ujinga na upumbavu kama huu.
Tatu, Mhe. Rais, tuhakikishe tunaweka mifumo ya kisasa ya kusimamia miundombinu yetu. kwani, hili ni jasho letu hasa walipakodi maskini wa taifa letu tunaowakamua na kutaka kuwaletea maendeleo. Kama tunavyolinda mabenki hata majumba yetu, lazima tutumie teknolojia na fedha kulinda miundombinu yetu. Lazima tuonyeshe kuwa tunajali na kujua tunachofanya kama jamii ya watu na taifa lenye kujitambua na kuwa na ari ya kujiletea maendeleo. Hapa lazima tuunde kikosi kazi kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa salama. Ikibidi, tupunguze utitiri wa walinzi wa wakubwa zetu uende kwenye kulinda miundombinu yetu. Pia, tuweke utaratibu wa kuwawajibisha watendaji wa umma kama vile wakuu wa wilaya na mikoa ambao miundombinu itaharibiwa kwenye maeneo yao. Nao watajua nani wa kumwajibisha katika hili.
Nne, Mhe. Rais,lazima tuelimishe watu wetu faida za hizo barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege nakadhalika. Lazima wananchi waelimishwe kuwa wao ndiyo walinzi na wenye miundombinu husika na siyo mali ya serikali kwani, serikali haina umbo zaidi ya kuwa wao. Ninapendekeza kutoa faini kwa wakazi wa maeneo ambapo miundombinu itahujumiwa kwa sababu zozote zile bila huruma. Badala ya TV zetu na vyombo vingine vya habari kutangaza ulevi na mambo mengine, vitoa matangazo kwa umma na elimu juu ya umuhimu wa miundombinu na umuhimu wake pia. Elimu ni nyenzo kubwa sana katika kufanikisha jambo lolote. Wananchi wetu wakielimika juu ya umuhimu wa miundombinu, watakuwa ndiyo walinzi nambari wani wa kuilinda na kuiendeleza. Lazima wajue kuwa miundombinu hii ni yao na inawawezesha kupata ajira, kufanya biashara, kusafiri kwa urahisi mbali kuwaletea maendeleo ya pamoja kwa kujenga mazingira safi ya kiuchumi.
Mhe. Rais, naomba nisikuchoshe. Japo ni muda mrefu tangu tuwasiliane, nafurahi kurejea na mawazo mapya ambayo najua utayafanyia kazi kama ambavyo umeyafanyia mengine kimya kimya. Kusema ukweli, hatuna wala huna haja ya kubembeleza waharifu bali kuwashukia kama mwewe na kuwapatiliza. Tumekupa rungu la Urais ili ufanye hivyo. Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni. Kila la heri.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment