Mnamo Juni 21, 2022, kulitokea ‘ajali’ ya treni huko Tabora ambapo watu manne na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa. Japo ajali haina kinga, inaweza kuzuilika. Ajali tajwa inasemekana kusababishwa na hujuma dhidi ya miundombinu iliyofanywa na watu wasiojulikana. Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikaririwa akilalamikia hujuma hapo Julai 3, kuna uwezekano ajali husika ilisababishwa na hujuma. Kama kweli ni hujuma, tunashauri yafuatayo kufanyika ili kuepusha ajali kama hizi za kutengenezwa ambazo zinaweza kuepukika kama tutachukua hatua madhubuti na mujarabu tena kwa wakati ufaao.
Mosi, kuna haja ya taifa kuiangalia kadhia hii kisayansi ili kupambana nalo. Mfano, napendekeza kuunda kikosi maalumu cha kuhakikisha usalama wa miundombinu yetu zikiwemo reli na nyingine chenye kufanya kazi kweli kweli kama bado hakijaundwa na kama kimeundwa kukiuliza, imekuwaje hujuma kama hizi zinatokea na kimechukua hatua gani au kina mipango gani ya kuzikomesha. Kuwa au kuunda kikosi hiki ni suala moja. La pili, ni kukiwezesha. Lazima kikosi hiki kipewe ujuzi na uwezo kama ule vilivyo nao bandari na viwanja vya ndege. Pia, serikali ijenge utaratibu wa kuwafukuza kazi wakuu wa taasisi kama hizi pale wanaposhindwa kukidhi matarajio au kuzembea kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Mkurugenzi wa Bandari aliyebadilishwa baada ya kutokidhi matarajio. Mbali na kikosi na utendaji wake, lazima tukipe nyenzo tena za kisasa. Mfano, reli zetu ziwekewe mfumo wa sensors ambapo mtu aliyeko makao makuu anaweza kujua ni lini au wapi kuna tatizo. Kama. Huu umepitwa na wakati, bado upo mwingine ambao ni mujarabu. Siku hizi kuna teknolojia ya kutumia ndege aina ya drones. Kwanini mamlaka husika zisinunue na kuweka drones ambazo zitakuwa kazi yake ni kuruka juu ya reli na kutoa taarifa kabla ya treni kutumia njia husika? Hili linawezekana kabisa. Pia, litapunguza ugumu wa shughuli yenyewe hata gharama za kuwatumia binadamu kufanya shughuli hii ambayo ni nyeti kwa usalama wa reli, treni, abiria, mizigo hata uwekezaji husika katika miundombinu hii.
Pili, mbali na usalama, kuna haja ya taasisi husika kuwaelimisha watu wetu faida ya kutunza na kulinda mali za taifa. Kwani, wanaozihujumu, wanajihujumu wenyewe tokana na uoni mfupi. Kuelimisha umma, licha ya kutoa elimu, kutatoa taarifa na ujuzi juu ya nini kitawakuta watakaobainika kuhujumu miundombinu ukiachia mbali madhara yanayoweza kusababishwa kwa taifa, watu wake na mali zao. Mfano, ajali kama hizi zinagharimu maisha ya watu. Hivyo, kuathiri familia zao sambamba na wale wanaopata ulemavu tokana na ajali hizi. Pia, hawa wanakuwa mzigo kwa taifa na familia zao bila ulazima tokana ukweli kuwa ajali hizi siyo za kimaumbile. Nashauri ziwepo kampeni za kutoa elimu juu ya umuhimu wa miundombinu kwa taifa na watu binafsi ili kuwawezesha watu wetu kuwa sehemu ya uwekezaji huu muhimu kwao na taifa.
Tatu, wanaohujumu miundombinu ya taifa wanatenda makosa ya jinai ukiachia mbali kukwamisha, kuchelewesha hata kuua maendeleo ya taifa. Hapa ndipo usemi kuwa mjenga au mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe unapoleta maana. Serikali inabidi iwe kali kweli kuhusiana na hawa wanaohujumu miundombinu yetu, kuua watu wasio na hatia na kusababisha hasara. Busara inasema kuwa auaye naye lazima auawawe ingawa hatuwezi kutumia adhabu ya kifo kama suluhusisho ya kila kitu. Hata hivyo, tokana na uzito na madhara ya kadhia kama hii, lazima tuje na jawabu mujarabu. Hapa, lazima tuwashughulikie hata ikibidi kufumba macho nakuwanyonga au kuwafunga vifungo vya maisha ili kuwaondoa au kuwapunguza watu kama hawa mbali na kutoa onyo kwa wale wanaopanga kufanya hujuma kama hizi kwa sababu zozote zile ziwe tamaa au ujinga.
Nne, wahusika wajulishwe kuwa wanasababisha taifa hasara tokana na uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ambapo Rais alisema kuwa inagharimu takriban Dola za kimarekani milioni tatu na ushei kujenga kilometa moja ya reli. Hii siyo chenji ya mboga kwa taifa maskini kama letu. Kwanini kujitia hasara wenyewe hata kama wahusika wanafanya hivyo kupata vyuma chakavu na kupata fedha kidogo kwa matumizi binafsi kwa gharama ya hasara kwa umma? Nadhani hapa twende mbali na kupiga marufuku ununuzi na uuzaji wa vyuma chakavu nchini ili kunusuru miundombiu yet una taifa letu. Kwani mauzo ya vyuma chakavu yanachangia kiasi gani kiuchumi ikilinganishwa na hasara inayolisababishia taifa? Hakuna ubishi kuwa uwepo wa masoko ya vyuma chakavu ni kichocheo kizuri kwa watu wajinga na wenye tamaa kuhujumu miundombinu yetu kwa faida au mapato ya muda mfupi.
Tano, kama taifa, tupambane vilivyo na umaskini kwa kuwawezesha watu wetu kichumi huku tukitenda haki kwa kupambana na ufisadi unaotoa motisha kwa watu wetu kuhujumu nchi yao wakiamini wanaweza kufanya hivyo na kutofungwa au kuadhibiwa. Maana, mojawapo, japo si lazima kuitumia kuvunja sheria, ya sababu ni umaskini unaoweza kuepukika kwa kuwajengea mazingira bora na uwezo watu wetu kiuchumi. Hapa lazima waelimishwe kuwa miundombinu ni mojawapo ya nyenzo za kuwawezesha kujiletea maendeleo na kuboresha maisha yao na kuondokana na umaskini. Sambamba na hili, lazima tupambane na ujinga ambao, kimsingi, pamoja na tamaa na ubinafsi ndivyo vinasababisha hujuma kama hizi.
Tumalize kwa kushauri mamlaka kuchukulia suala la hujuma dhidi ya miundombinu na mali za taifa kufa na kupona ili kuepuka hasara za uhai na mali mbali na kuchelewesha au hata kutowesha maendeleo kwa watu wetu. Hii ifanywe kuwa vita ya kudumu ya kipaumbele cha juu kwa taifa ili kuepuka ajali na hasara zinazoepukika kama tutakuwa makini. Lazima tujue kuwa vitu hivi si mali binafsi wala ya waliopo sasa bali hata vizazi vijavyo. Muhimu, tutoea adhabu kali na elimu vya kutosha kwa watu wetu wajione ni sehemu ya uwekezaji huu kwa ajili yao na vizazi vyao.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment