The Chant of Savant

Tuesday 19 July 2022

Mgogoro wa Mwasonga Kisarawe kunani na nani?

                                                        Mkuu wa Wilaya Kisarawe Nixon Simon

Hivi karibuni vyombo vya habari vilifichua na kuripoti kashfa inayozidi kupanda kasi ambapo wakazi wa Mwasonga, Kisarawe wakilalamikia hujuma wanayofanyiwa kwa kisingizio cha uwekezaji. Wanadai kuwa eneo lao limegundulika kuwa na madini ya mchanga ambayo yameishapata mwekezaji bila kumtaja ni nani. Je mwekezaji au Wawekezaji ni nani na kwanini wanataka au kuruhusiwa kuwadhulumu, kuwaibia au kuwaumiza wananchi? Je hii siyo kashfa ambayo inaweza kuepukika au kushughulikiwa kwa wakati na kwa haki kabla ya kuwaumiza wananchi? Je taifa linapata faida gani kwa kuruhusu au kushuhudia wananchi wake wakiumizwa na mafisadi na walafi wachache?

            Wananchi wanadai kuwa walikubaliana na mwekezaji awalipe shilingi 20,000 kwa mita moja ya mraba. Hata hivyo, wanadai mwekezaji amewageuka na kutaka kuwalipa shs. 3,000 kwa mita ya mraba badala ya shilingi 20,000. Je kunani hapa? Hii siyo dhuluma ya mchana kweupe? Kwanini walikubaliana kulipa 20,000 halafu ghafla wanageuka? Je huyu ni mwekezaji au mchukuaji? Mfano, Milka Kaoneka alikaririwa akisema kuwa alijenga nyumba yake kwa shilingi 75,000, 000 miaka kumi iliyopita. Mwekezaji eti anataka kumlipa shilingi 54,000,000. Je nani atalipia hiyo hasara ya shilingi milioni 21? Je thamani ya nyumba hiyo, baada ya miaka kumi tangu kujengwa ukiachia mbali bei ya ardhi, bado ni ile ile au imepanda? Je inawezekana Kaoneka akajenga nyumba kama hiyo kwa bei hiyo hiyo kwa sasa ambapo kila kitu kimepanda bei? Je kwanini wahanga nao wasidai walipwe zaidi kama mwekezaji ameona ana haki ya kupunguza bei au wakaamua kuachana naye na kuendelea kuishi kwenye nyumba zao? Kwanini wakubwa wetu wanashindwa kuona kitu kidogo na rahisi kama hiki? Kunani? Je ni watanzania wangapi wanakumbwa na kadhia kama hizi hasa wale wa mikoani ambako hakuna vyombo vingi vya habari kuzifichua?
            Je nini kimetokea hadi kiasi kilichokubaliwa kipunguzwe hadi 3,000? Kuna haja ya wahusika kuandaa maelezo ya kina na yanayoingia akilini kabla ya umma kufikia hitimisho kuwa ima kuna dhuluma au rushwa imetembezwa kwenye kashfa na hujuma hii. Je serikali yenye macho mia na mkono mrefu haijui kashfa hii? Kama inajua, kwanini haiingilii kati? Na kama haijui ni kwanini na vyombo vyake na watendaji wake ni vya nini? Je inakuwaje Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe yupo na anaaacha mtama huu umwagwe kwenye kuku wengi?  Inakuwaje anajiachia na kuwaachia wananchi wamlalamikie Mheshimiwa Rais kana kwamba yeye hana mamlaka ya kuingilia kati kulinda haki za wananchi? Je kunani Mkuu wa Wilaya amekaa kimya? Je ameshindwa? Je amepuuzia au kudharau? Je ananufaika vipi na kashfa hii? Je kazi yake ni nini kama anashindwa kutatua mgogoro mdogo kama huu hadi wananchi wake wamlilie Rais ambaye ana mambo mengi ya kufanya kitaifa? Je huyu bado anafaa kuendelea kuwa ofisini huku akishindwa kutatua matatizo ya wananchi wake?
            Hata hivyo, ushahidi wa kimazingira––––kama maelezo ya wahanga yatafanyiwa kazi vilivyo–––unaonyesha kuwa serikali inajua. Maana wanasema kuwa walipodai haki yao, mmojawapo wa viongozi ambaye hawakumtaja jina aliwaambia kuwa watake wasitake watalipwa pesa hiyo kwa vile haya ni maagizo toka toka juu. Huko juu ni wapi na nani wapo huko na wanafanya nini? Je juu ni Wilayani, Mkoani au Taifa na kwanini maelekezo yatoke juu kana kwamba huko juu ndiye mwekezaji? Je huko juu ni wawakilishi wa mwekezaji na kwanini? Kama wahusika wanaolipwa mishahara kwa kazi kama hizi wameshindwa kuwatetea wananchi, je nani atawatetea?
        Kinachoendelea Mwasonga ni ushahidi tosha kuwa baadhi ya watendaji wetu wamo ofisini ima kutumikia matumbo yao au mafisadi wachache na wale wanaoitwa wawekezaji wasiojali hata haki na uhai wa wananchi tena maskini. Kwa anayejua maana ya uwekezaji, anayepaswa kubembeleza siyo mwenye ardhi bali yule anayetaka kumuondoa akawejeze. Pia, ifahamike kuwa wahusika wanapaswa kufahamu na kutambua kuwa mwekezaji haji pale kucheza bali kutengeneza fedha. Hii ni haki yake. Lakini hana wala si  haki ya kufanya hivyo kwa kuwaumiza wengine hata kama ni wadogo kama ilivyo kwenye kadhia hii. Je serikali kweli inashindwa kuingilia kwa wakati ili kuhakikisha haki za wananchi wake zinalindwa? Je kwanini serikali inakubali kuweka nguo zake za ndani hadharani?
        Mradi husika hapo juu unaitwa shirikishi. Je nani anamshirikisha nani, vipi na kwa vigezo vipi? Inakuwaje kwenye mradi shirikishi upande mmoja unakuwa na nguvu kuliko upande mwingine. Huu ni ushirikishaji au ushirikishwaji gani? Je hawa wanaotaka kuwadhulumu na kuwaibia wananchi watafanyaje kama wananchi wataamua kutumia wingi wao na kujichukulia sheria mkononi kuhakikisha haki, mali na maisha yao havichezewi? Je, hili likitokea, nani wa kulaumiwa baina ya mwekezaji, wahusika walioshindwa kufanya kazi zao barabara na kwa weledi na wananchi? Maana, katika ya Tanzania iko wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kupigania na kusimamia haki yake kama haki yake kisheria. Katiba Sura ya Pili 9 (c) inasema “kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.” Je hawa wanaoshindwa kuzuia mwekezaji kuwahujumu wananchi hawaoni kuwa wanavunja katiba ukiachia mbali kukiuka viapo vyao vya uaminifu kwa nchi na watu wake na serikali yake? Je hawa wanapaswa kuendelea kuwa kwenye utumishi wa umma wakati wameshindwa wazi wazi?
        Tuhitimishe kwa kumtaka Mheshiwa Rais kama ambavyo wahanga wameomba aingilie ili haki zao zilindwe na haki kutendeka. Pia, tunashauri Mheshimiwa Rais au mamlaka husika kuwawajibisha na kuwaadhibu walioko nyuma ya kadhia hii inayoichafua serikali na kuitia aibu.
Wakati tukishauri Rais aingelie, inabidi tujiulize. Je Rais atafanya mangapi? Walio chini yake na wahusika kazi zao ni zipi? Kashfa ya Mwasonga ishughulikiwe mara moja ili kurejesha imani kwa serikali na kuleta uwajibikaji na utendaji haki katika ofisi za umma.
Chanzo: Raia Mwema leo

No comments: