The Chant of Savant

Friday 8 July 2022

Jamii Ijifunze Utamaduni wa Kuchaganua


Kabla ya kukua, kupata fedha na kufilisika, sikujua busara ya Mungu. Mfano, kwanini kuumba maskini na maamuma au mbumbumbu wengi kuliko wasomi, wahubiri, mashehe na wengine wengi wawatumiao kupata au kuishi kitajiri kwa mgongo wa wao wanaoteseka. Je ni kwanini wakati wahubiri wanatuambia kuwa Mungu anajua na anamilki kila kitu? Je alishindwa nini kuwamegea maskini na mbumbumbu mali na ujuzi wake visivyomithalishwa?

Katika kutafuta majibu ya maswahil hayo, nilizidi kuchanganyikiwa kuambiwa kuwa Mungu ana uwezo wa kuwapa viumbe wake mali na ujuzi bila kufilisika. Je ni kweli au ni hadithi za wajanja wachache wanaojifanya kuwa na majibu ya kila swali wakati hawajui chochote zaidi ya kujipa sifa na kuwatisha wengine kwa kisingizio cha kutumwa na Mungu bila ushahidi wa kiakili. Je ni nini mantiki ya kuumba wenye nguvu wachache kuliko wasio na nguvu? Je ni nini mantiki ya kuumbwa kwa majanga kuliko furaha katika dunia hii? Kujibu maswali hayo hapo juu na kuyajua haya kunahitaji fikira jadidifu na uwezo wa aina yake wa kudurusu mambo bila woga wala hofu ya kukufuru au kuwaudhi baadhi ya watu.

Katika kutafuta majibu ya naswali hayo hapo juu nilijikuta nikiuliza maswali mengine badala ya majibu. Je maswali yaweza kuwa majibu na majibu kuwa maswali?  Nani anajua? Hebu tuzame na kufikiri kwa pamoja. Je wote tungekuwa wasomi au wajanja nani angemwibia nani? Nani angemtumia nani? Kama wote tungekuwa matajiri nani angemwajiri nani? Je wote tungekuwa na magari abiria wangepatikana wapi? Na kama wote tungekuwa madereva, wapiga debe wangepatikana wapi? Bila wagonjwa, daktari hana kazi. Bila wahalifu, polisi hana kazi. Bila wajinga wachungaji na mashehe hawana chao. Ujinga, udhambi, umaskini, wog ana hata upumbavu vipo kwa sababu maalumu japo si wote wanaweza kuzijua kwa vile si wengi wanayadurusu malimwengu. Bila kuvunja sheria, majaji, mahakimu, wanasheria na mapolisi hawana kazi. Bila walevi serikali haina kodi ya ubwete. Bila wabaya wazuri wangepatikana wapi na vipi? Bila wafupi nani angewatambua warefu?

Kwa wanaojua nyodo na ulafi wa matajiri watakubaliana nasi kuwa kama Mungu angeumba matajiri wengi kuliko maskini Dunia ingekuwa ishatoweka. Hebu fikria namna matajiri wanayotumia kwa kufuja huku maskini wengi wakiteseka kwa umaskini. Kama tutaangalia namna matajiri wanavyoivuja kwa magari, madege, na upuuzi mwingine–––––kama si kupata majibu–––––japo tutapata ufahamu japo kiduchu juu ya mantiki ya kuwa na maskini wengi kuliko matajiri duniani. Mfano, ni taifa la Marekani. Nani anaweza kuamini taifa kama Marekani linatumia fedha nyingi kuliko bara la Afrika? Nani angeamini kuwa bajeti ya Kanada––––nchi yenye watu wasiofikia milioni 40­­­­–––ina bajeti kubwa kuliko nchi zote za Afrika Mashariki? Je hapa busara ni nini? Angalia kijipande cha nchi kama Dubai kinavyofanya makufuru kwa utajiri wake. Angalia magari ya bei mbaya mitaani yanayochafua mazingira kiajabu bila sababu.

Hebu twende mbali na mbele zaidi kufikiri na kudurusu. Angalia mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na bara dogo kama Ulaya ikilinganishwa na Afrika. Nani hajui kuwa tatizo la ongezeko la joto na mabadiliko ya tabia nchi duniani yalianzishwa na bara la Ulaya lilipoanza kile kinachoitwa mapinduzi ya viwanda ambayo hayakuwa na msaada bali madhara ya kijamii hata kiuchumi kwa mabara mengine hasa Afrika na Asia tokana na kutawaliwa na kuibiwa?

Je busara inasemaje hapa? Kuna mamimilioni ya watu ambao bado wanaishi kwa vile ni maskini japo wapo wengi walioisaidiwa na utajiri wao kuishi japo si wengi. Wapo wajinga wengi wanaoishi kwa amani tofauti na wasomi wanaoishi kwa mateso na majuto. Je mbu wangekuwa na miili mikubwa hata kama ya njiwa au sungura wangeacha madhara kiasi gani duniani? Je tembo wangekuwa wengi sawa na mbu miti na majani vingeathirika kiasi gani? Je wanawake wangekuwa na tabia za wanaume au wanaume tabia za wanawake familia zingekuwaje?

Hebu tuzidi kudurusu. Hivi almasi na dhahabu na vito vingine vya thamani vingekuwa vingi kuliko mawe hali ingekuwaje? Je mito na maziwa visingekuwa na mambo maji yangekuwa safi tokana usafi wafanyao? Je ni wangapi wanajua hii busara lau wafurahi kazi ya viumbe hawa ambao wengi huwaona wakatili? Suala huzaa sana kuliko simba kwa vile huliwa na simba. Samaki huzaa sana kwa vile huvuliwa.  Je simba wangezaa kuliko simba wanyama wengine wasiokula nyama wangekuwa wapi? Je bila wadudu mimea ingekuwapo? Je wadudu na mimea havitegemeani? Wadudu huishi kwa kutegemea kula nta ya miti. Kadhalika, miti huzaliana kutokana wadudu kuchanganya mbegu zake za uzazi. Je ni kipi bora zaidi ya kingine kati ya wawili hawa? Je mke na mume si pande mbili za sarafu moja zinategemeana na kulingana kwa wale wenye kuona visivyoonekana? Wajinga husema ndoa ni ndoana. Je ndoana ni ndoa? Je ndoa ni doa au dau la maisha?

Tumalizie kwa kushauri wasomaji wetu kuanza kujenga tabia ya kudurusu na kuhoji kila jambo hasa malimwengu ili wasiishie kulalamika au kutumiwa na watu wachache wanaoiga au wanaojua kudurusu kuliko wao. Mbali na hiyo, watajiongezea busara na ujuzi ambavyo ni haba kwa watu wengi. Mfano, ukijua kuwa kuwa maskini si kosa wala kasoro, hutadanganywa na tapeli yeyote awe wa kiroho au tunguli kuhusu namna ya kutajirika hata kwa kuua wenzako mfano walemavu wa ngozi au kuibiwa kirahisi kwa visingizio mbali mbali kama vile miujiza.

Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: