How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 12 July 2022

Tanzania tumejiandaaje kunufaika na Kiswahili?

Julai 7 ni siku ya Kiswahili duniani. UNESCO, shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni, liliamua tarehe tajwa iwe siku ya Kiswahili duniani. Kuna sababu kadhaa za Kiswahili kupewa siku yake kimataifa.  Hii ni kutokana na ukweli usiopingika kuwa,licha ya kuwa lugha inayokua haraka, lugha ya Kiswahili ni moja kati ya lugha kubwa duniani. Kwa sasa lugha hii ina watumiaji zaidi ya milioni 200. Ni lugha inayotumika katika mataifa ya Kenya, Tanzania, Uganda ambayo ndiyo waanzilishi wa Jumuia ya Afrika Mashariki ambayo pia inaitumia lugha hii kama lugha yake rasmi katika shughuli zake. Pia, Kiswahili kinatumika katika nchi za Burundi, DRC na Rwanda. Mbali na mataifa haya, Kiswahili kinazungumzwa na kutumika katika mataifa ya Malawi, Msumbiji, Rwanda, Somalia, Comoros, na Zambia. Mbali na mataifa haya, Nchi ya Afrika Kusini imeonyesha wazi kiu yake ya kutaka lugha hii itumike kama lugha  muhimu ya Afrika.  Ndiyo maana hivi karibu ilisaini mkataba na Tanzania juu ya ufundishaji wa Kiswahili. Afrika Kusini na mataifa yote yaliyokuwa chini ya kile kilichojulikana kama Tume ya Ukombozi Kusini mwa Afrika (FLS) yanajua umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya ukombozi si wa Tanzania tu bali Afrika kwa ujumla.

            Wengi wanaamini kuwa asili ya lugha ya Kiswahili ni Tanzania ingawa hata wenzetu wa Kenya––––baada ya wao kukidharau, kukiponda na kukataa kutokitumia tangu siku walipopata uhuru kwa vile walipwakia kiingereza––––wameanza kudai wao ndiyo asili ya Kiswahili––––baada ya Kiswahili kupanda chati. Mbali na kudai wao ndiyo asili ya Kiswahili, wameanza kufaidika nacho kuliko wenyewe, yaani Tanzania, ambao walikikuza kwa kukifanya lugha ya taifa na lugha ya ukombozi. Watanzania wamebaki kuwa watazamaji wakati wengine wakifaidi matunda ya Kiswahili kutokana na tabia yao ya kutochangamkia fursa zinapotokea. Kama serikali yetu haitaingilia kati na kuweka mikakati ya makusudi, sitashangaa kukuta wakenya hata wanyarwanda na warundi wakifundisha Kiswahili wakati watanzania wakikalia kulalamika au kuzubaa. Changamkieni fursa hizi jamanini.  Ukiangalia hata kwenye tafsiri nyingi za maneno ya Kiswahili kwenda kwenye lugha nyingine, kinatumika Kiswahili kisicho sanifu cha Kenya. Wakenya wengi wanafundisha Kiswahili Ulaya kuliko Watanzania ambao ndiyo wenye lugha yao. Pamoja na wakenya kufundisha Kiswahili ughaibuni, huwa wanakionea aibu na kukidharau wakiwa kwao. Hupenda kuongea au kujinasibisha na kiingereza kuliko Kiswahili. Nimeishi Kenya kwa miaka mitatu tena jijini Nairobi. Niligundua kuwa si wakenya wengi wanajua kiingereza wala Kiswahili zaidi ya lugha zao za kikabila ambazo wanazipenda na kuzitukuza japo siyo kama kiingereza huku wakikidharua Kiswahili kama lugha ya watu ima wasiostaarabika au wasio soma. Nakumbuka siku moja niliambiwa mie siyo mtanzania kwa vile nilikuwa naongea kiingereza kizuri kwa sababu watanzania hawajui kiingereza.  Nilichukizwa na kushangazwa na mjumuisho huu na kuuliza kuwa mbona Mwalimu Nyerere alikuwa anaongea kiingereza kizuri kuliko Kenyatta na Moi? Nilihoji kwanini wanasheria maarufu kama vile rafiki zangu Profesa Makau Mutua na Ndugu Willy Mutunga (PhD) Jaji Mkuu Mstaafu na Rais wa Mahakama kuu ya Kenya walisomea Tanzania na kutokea kuwa maarufu walisomea UDSM.

            Ni bahati mbaya kuwa hata watanzania wengi, hasa walio wajinga au ambao wamesoma au kutosoma lakini wasielimike wanakionea aibu Kiswahili kwa kuchanganya Kiswahili na kiingereza ili waonekane wamesoma hata kama si kweli. Wanabemenda Kiswahili na kubukanya kiswanglishi kiasi cha kutia kichefuchefu. Wapo waliowahi hata kumcheka Hayati Dk John Magufuli kwa kusema eti alikuwa hajui kiingereza kwa vile hakupenda kukiongea kana kwamba hiyo nayo ni dhambi au kasoro. Je hawa waliokuwa wakimcheka au kumng’ong’a wazazi wao walikuwa wakijua Kiswahili au wamesoma japo waliona mbali na kuwasomesha?

             Pia, lugha hii ni lugha kubwa pekee isiyo ya kigeni wala kikoloni barani Afrika. Mbali na hiyo, Kiswahili ni lugha isiyo na mwenyewe lakini lugha ya kila mtanzania. Hii ni kutokana na ukweli kuwa hakuna kabila la waswahili linaloweza kudai kuwa hii ni lugha yake. Ajabu ya maajabu ambao pia ni aibu na kashfa ni ile hali ya magazeti makubwa ya Tanzania kushindwa kuitangaza wala kuitambua siku hii.  Nilisoma habari za siku ya Kiswahili ulimwenguni kwenye gazeti la Kenya la the Daily Nation iliyoandikwa na ndugu yangu Austin Bukenya. Chini ya kichwa cha habari Saba Saba Day is coming: What should Kiswahili tell the world? Bukenya alisema kuwa, licha ya kukaribisha, kufurahia na kushangilia siku hii adhimu kwa lugha hii adhimu, anakumbuka Saba Saba kama siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere kuanzisha chama cha TANU kilichoenzi na kukuza lugha hii ukiachia mbali kuitangaza kimataifa.

Sifa nyingine ambayo Kiswahili kinacho­­­ tofauti na karibu lugha zote za kiafrika na hata za kikoloni ambazo serikali huru zilipwakia kama vile kiingereza, kifaransa, kireno hata kiarabu––––tena kama suto kwa tawala zetu uhuru zisizo huru­­­–––ni uwezo wake wa kuwaunganisha waAfrika na dunia pale ambapo wanasiasa walishindwa tokana na uchoyo na upogo wao.

Leo hatusemi mengi. Tumalizie kwa kuwasihi watanzania hata serikali kutambua umuhimu wa Kiswahili kisiasa, kiuchumi hata kiutamaduni. Lugha ni bidhaa inayoingiza mabilioni ya shilingi kama itatumiwa vizuri. Kabla ya nchi nyingi zilizotawaliwa na mwingereza au mfaransa na kurithi mifumo yao kujitambua japo si nyingi, nchi hizi zilikuwa zikiziuzia vitabu vya kiada mbali na kuwajaza ujinga wao kwa kisingizio cha elimu na usasa.  Japo lengo la Tanzania kufundisha nchi nyingine Kiswahili siyo baya kama la kikoloni, kuna haja ya kuunda mikakati mahsusi na ya makusudi kuhakikisha, kama taifa na wenye Kiswahili, tunafaidika na fursa hii ya lugha yetu kukubalika kimataifa.

Chanzo: Raia Mwema Jana.

No comments: