How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 5 July 2022

Mgogoro waLoliondo/Ngorongoro vita ya kiuchumi au?

Mgogoro unaoendelea huko Loliondo na Ngorongoro unahitaji busara, maridhiano na ukweli. Mpaka naandika, kuna mkanganyiko hata utata juu ya nini kinaendelea Ngorongoro. Kila stori ina pande mbili. Hata huu mgogoro wa Ngorongoro kadhalika una pande mbili yaani wanaounga mkono na wanaopinga zoezi zima. Kumekuwa na tuhuma kuwa wananchi wa Ngorongoro wanaamishwa kupisha uwekezaji wa Ortello Business Corporation (OBC) ambayo si ngeni nchini. Kwa wanaokumbuka jina Brigadier Mohamed Abdulrahim al-Ali lilianza kuchomoza wakati wa awamu ya pili ilipodaiwa kuwa mwarabu huyu alikuwa ameshiriki uwindaji uliozungukwa na ufisadi na uharibifu. Ni bahati mbaya kuwa––––tokana na sera ya hovyo ya ruksa wakati ule––––kashfa hii iliuawa sawa na nyingine kama vile Richmond iliyomg’oa Waziri Mkuu Edward Lowassa, TICTS iliyomhusisha Waziri wa Biashara zamani, Nazir Karamagi na wenzake, kuhujumiwa na kuuawa kwa NBC kulikohusishwa na familia ya mke wa Rais wa zamani mbali na IPTL ambayo nayo pia ilianza awamu ya pili na kuuawa katika awamu hii.

            Kimsingi, mkanganyiko wa Loliondo na Ngorongoro si wa jana wala juzi. Kilicho kipya ni ile hali ya nchi jirani kulishupalia kuliko wakati wowote. Wapo wanaoona kama wananchi wa maeneo haya wanaonewa na kuhujumiwa kupisha uwekezaji wenye shaka na wale wanaoona ni hujuma ya majirani zetu ambao ni washindani wetu katika biashara ya utalii. Je ukweli ni upi? Kuondoa mkanganyiko na utata, mamlaka zinapaswa kutueleza ukweli ili tufanye maamuzi wenyewe. Je ni kweli kadhia ya Loliondo na Ngorongoro ni ufisadi au ushindani wa kibiashara? Wapo wanaoona ni ushindani hasa kutokana na suala zima kupigiwa kelele na majirani zetu sana kuliko hata sisi wahusika na wenye mali. Je kitanda usicholalia waweza kujua kunguni wake? Wapo wanaoona kama kuna harufu ya ufisadi kuhusiana na kampuni tajwa hapo juu. Je ni mojawapo au yote?

            Swali linalozua utata bila majibu ni kwanini wamasai wahamishwe wakati wameishi na wanyama husika kwa mamilioni ya miaka? Inakuwaje wahamishwe wakati wamekuwepo hata kabla ya Tanzania kuwapo? Je ni vigezo gani vimetumika kuwahamisha wahusika? Kwa wanaokumbuka, hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Tanzania kuwahamisha baadhi ya watu wake. Nani amesahau namna vijiji vya ujamaa vilivyoanzisha kadhia hii ya kuhamishana? Je wahusika wameshawishiwa na kuelimishwa vya kutosha na kujua faida na hasara za kuhamishwa au kukataa kuhama?

Sina ugomvi na uhamishaji hata ukataaji kuhamishwa kama wahusika wanaona inafaa. Hata hivyo, binadamu hawahamishwi kama wanyama. Kama tunamilki shamba kijijini na hakuna anayeweza kuchukua ardhi bila fidia, inakuwaje wafugaji ambao mashamba yao ni mbuga yao waondolewe kana kwamba hawana haki? Wapo wanaohoji mantiki ya kuwahamisha wananchi wa maeneo tajwa kwa vile hii ardhi wamepewa na Mungu. Hivyo, binadamu hata awe serikali kuwanyang’anya ni dhuluma ya wazi na isiyo na sababu zaidi ya uonevu. Je nani wako kwenye huu uwekezaji wa ajabu ajabu? Je kazi ya serikali kubwa siyo kulinda wananchi wake? Je ni kazi ya serikali kufikiri kwa niaba ya wananchi au kuwashirikisha kwenye kila inachofanya kwa vile wao ndiyo wenye serikali na wananchi si mali ya serikali?  Je wenye kutaka majibu ya maswali hayo juu na mengine wanaweza kupata majibu sahihi toka kwa nani na wapi?

Juzi kuliripotiwa kifo cha askari mmoja. Je kulikuwa na sababu ya kupoteza uhai wa mtu asiye na hatia? Je kwa kufanya zoezi kama hili bila maridhiano, mnawafundisha nini wahanga zaidi ya kutaka waanze kujihami ukiachia mbali kutumiwa na maadui wetu wa taifa? Tafadhalini tusijenge mazingira ya kuwa na makundi ya kigaidi kama kule Somalia na Nigeria ambayo mengi kuundwa kwake kumetokana na dhuluma ya serikali.

Katika kupanga kuwahamisha wamasai, tukumbuke kuwa Wamasai walikuwa taifa moja la Masai lililogawanwa na wakoloni waliounda hizi nchi zao tunazotumia kwa sasa kuwaita Wakenya na Watanzania japo kwenye damu na mioyo yao wao ni Wamasai kwanza. Wale wanaotaka kufanya zoezi hili lionekane halitendi haki tokana na maslahi wanayojua wanaona kama siku hizi wanyama wamekuwa na thamani kuliko watu kana kwamba nao walipigianiauhuru wa taifa letu. Wanaenda mbali; na wana mantiki. Wanasema wazi kuwa Wamasai wameishi na wanyama kwa mamilioni ya miaka bila kuwadhulu kama sisi tunavyofanya kwa sasa. Naamini serikali ina nia safi. Hata hivyo, haina haja ya kufanya jambo zuri kwa njia mbaya tokana na ukosefu wa uelimishanaji na makubaliano.

Je faida zitakazotokana na zoezi hili ni kubwa kuliko hasara? Tunahitaji maelezo. Mfano, tuna kile kinachoitwa trophy hunting ambapo watalii wengi wazungu na waarabu huja na kuua wanyama na kupiga picha nao na kututupia dola tusijue wanyama ambao ni hazina yetu wakiisha hizo dola hazitengeneza wanyama.  Kuna dalili za ukoloni na kujikana kwa kuzubazwa na dola. Mfano, Wamasai waliokuwa wakiwinda mfano simba kuonyesha ushujaa wao, walichukuliwa kama wanaharibu simba kwa mila ‘potofu’. Je trophy hanting siyo uharibifu wa wanyama na mazingira na mila kipofu hata kama tunatupiwa dola?

Tumalize kwa kuomba––––chonde chonde–––mamlaka zituelimishe kuhusiana na kadhia hii kutuepushia kutumbukia kwenye mtego wa kutumiwa kujihujumu bila kujua. Je ukweli ni upi kuhusiana kadhia ya Loliondo na Ngorongoro? Wakati wa kutoa majibu mujarabu na yanayoingia akilini ni sasa.

ChanzoRaia Mwema leo.


No comments: