How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 23 July 2022

Dini zinapogeuka janga (V)

Katika muendekezi wa makala hii, leo nitajikita kwenye masuala ya kiusalama binafsi na kitaifa. Nitatolea mfano kinachoendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) mbako makundi pinzani ya kikristo na kiislamu yamewagawa wananchi kiasi cha kuuana wao kwa wao na kukaribia kuisambaratisha nchi kama siyo mataifa ya nje kuingilia kati. Mamia wameuawa huku maelfu wakilazimika kukimbia makazi na shughuli zao. Dini hizi mbili zimewaaminisha wafuasi wake kuwa ni maadui na si ndugu. Ni ajabu kuwa Waafrika––––ambao ndiyo wanaongoza kwa kupokea na kupwakia dini za wenzao––––tunajua ni lini tumekuwa wakristo au waislam lakini hatujui ni lini tulikuwa Waafrika. Kwa wenzetu mfano waarabu, uarabu wao huja kwanza na udini ufuata baadaye. Hebu jaribu kusikia mataifa na viongozi wa kiarabu wanapokutana au kufanya jambo. Utasikia wakitambulisha kwa uarabu wao kwanza. Hata majina ya nchi zao kadhalika. Hebu angalia mfano the Kingdom of Saudi Arabia au the United Arab Emirates au Syrian Arab Republic kwa uchache. Ukiondoa nchi kama Afrika ya Kati na Afrika ya Kusini ambazo zinatumia neno Afrika, si nchi nyingi za Kiafrika zinatumia uafrika. Hata hizo hapo juu zinautumia uafrika kijiografia lakini siyo kiufuasi au ushufaa na utambuliko wao.

Je dini zinaathiri usalama binafsi na kitaifa vipi? Mfano wa CAR hapo juu uko wazi. Wananchi wanapochukiana, kushukiana hata kuuana wanahatarisha usalama wa nani kama siyo wao na taifa lao? Wananchi wanapogoma kufikiri pamoja matokeo yake ni nini zaidi ya kuhujumiana kiasi cha kujidhoofisha kama jamii na taifa? Mfano mzuri unaweza kutolewa kwenye makundi ya kigaidi yaliyoko Afrika. Kila kundi linaloibuka, lina jina la Kiarabu na si la Kiafrika. Hii maana yake ni nin? Ni kwamba watu kama hawa ni hatari kwa taifa kwa sababu:

a)     wamejikana kiasi cha kuweza kutumika hata kuhujumu wenzao na mataifa yao.

b)     ni rahisi kutumiwa na maadui wa taifa hata kwa mambo yasiyo ya msingi kama kupigania au kufia imani mbali na kuwa makuwadi wa wale wanaowaabudia kama ambavyo imejionyesha kwenye nchi zinazosumbuliwa na ugaidi.

c)     wengi wao wana ajenda za siri za kisiasa zilizojificha nyuma ya dini. Hawa hawana tofauti na wachungaji wa kujipachika wanaishia kwenye siasa baada ya kutumia dini kupata umaarufu na ufuasi ambao huugeuza kuwa mtaji binafsi kisiasa.

Mbali na ugaidi, kuna chuki ya kupandikizwa chuki na kudharauliana. Nadhani ni Waafrika peke yao wenye tabia ya kuchukiana na kutothaminiana. Ni Waafrika pekee wenye tabia ya kujichukia na kuchukia mila zao kwa vile dini zimewafundisha na kuwaaminisha hivyo kwa miongo mingi bila ya wao kuhoji. Mfano, kwanini ni Waafrika tu waliokubali kubadilishwa majina yao tofauti na wengine? Ukienda kwenye nchi za kiarabu, utakuta waarabu wakristo wana majina yao ya kiarabu ambayo hayana tofauti na yale ya kiarabu tunayoyaita ya kiislam kwa Afrika. Mfano, ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wakati wa utawala wa Saddam Hussein Tariq Aziz ambaye alikuwa muumini wa kanisa la kikatoliki na kikaldayo na bado akabeba jina ambalo kwa Waswahili wangelichukulia kama la kiislam bila kujua kuwa kumbe majina tuliyobandikwa ni aina fulani ya ukoloni wa kimila na dharau dhidi ya utambuliko na mila zetu ambavyo ni vitu muhimu kwa binadamu.

Tusisiteze kuwa utambuliko ni muhimu sana kwa binadamu kuliko hata wanyama. Hebu fikiri. Simba angekuwa anajua kuwa anaitwa simba halafu ghafla ukamuita fisi au mbwa angejesikiaje? Hapa Kanada huwa nashangaa kusikia wanyama wakiitwa majina ya binadamu na hakuna anayedai. Juzi tulipeleka vijana wetu kujiburudisha kwenye kuendesha vigari vidogo kama vya mashindano. Tulipokelewa na paka jike aitwaye Peter au Petro. Huku majina mengi hayana hata ujinsia. Si ajabu kusikia mwanamke akiitwa Alison, Hilary, Kennedy, Stanley na mengine. Kwa wanaume kuitwa majina kama Elizabeth Maria na mengine inawezekana mbali na ubin wa kike kwa Wakikuyu kule Kenya pale baba mtoto anapomkataa mtoto na kwa waarabu kadhalika.

Nafasi haitoshi. Nimalizie kwa kusema kuwa ni hatari pale baadhi ya dini zinaposema wazi kuwa ndugu wa muumini wao ni muumini wao. Je hili nalo ni jipya na la maana la kumfundisha mtu? Je nani anahitaji kufundishwa ndugu zake ni nani wakati ni wale aliozaliwa nao kwanza na pili wale waliomzunguka? Inakuwaje uwe na ndugu msiyezaliwa pamoja wala kufanana huku ukimgeuza uliyezaliwa naye adui eti kwa vile mna dini tofauti? Nadhani hata kuku, pamoja na kuwa na ubongo usiojaa kijiko, anawajua ndugu zake. Kwa ufupi dini zimetuandaa na kutufanya tuwe tayari kuteketezana, kuhujumiana hata kuuana kwa sababu za tofauti za kiimani. Hapa ndipo dini zinapogeuka janga jipya Afrika.

Chanzo: Raia Mwema jana.

No comments: