The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Wednesday, 21 October 2026

Fyatuland kufyatua BASATER awafyatue wasanii wa siasa

Baada ya wanene wa Fyatuland kuanza ufisadi, utovu wa nidhamu, na ukatili, Fyatu napankuunda Bangaiza Sanaa Taratibu Epuka Rabsha (BASATER). Baada ya kuona kaya nyingine uchwara zikihangaika,, kuwaadhibu, na kuwaadhibu hata kuwafungia wasanii wa sanaa za maigizo na kelele huku zikigwaya kuwafyatua wasanii wa siasa, Fyatu, daktari wa utawala, nimefyatuka na kuamua kuwafyatua mafyatu wanaofyatua wenzao wakati wao ndiyo wanaopaswa kufyatuliwa kwanza. Mfano, mpiga kelele akijifyatua na kuvaa vimino au kupayuka matusi, anafungiwa na kupigwa faini. 
            Vipi mnene akijifyatua na kufyatua njuluku za mafyatu au kutoa lugha za matusi na vitisho? Haki na usawa viko wapi hapa? Juzi, nilisika fyatu mmoja ambaye sikujua ni fwala na kupe akiwatishia mafyatu akisema “mnajua mimi ni nani?” Wewe ni nani zaidi ya chawa au kupe mgongoni mwa mafyatu unaowafyatua na kujisahau kuwa ofisi uliyo nayo ni yao? Sasa nafyatuka na kuonya kwa mara ya mwisho. Kifuatacho ni kufyatuka na kufyatua wafyatuaji wa mafyatu wangu wasiofyatuka wakafyatua wawafyatuao. Fyatu nataka kaya ya haki na usawa na siyo ufyatuanaji wa kifalafala kama hizo kaya uchwara.
            Ni ukumbaff na upofu kiasi gani kuringia nguo ya kuazima isiyositiri manonihino? Kicheche mfyatua kuku za mafyatu, hata awe mjanja au kuridhiska kiasi gani, hana haki wa ubavu kumfyatua mwenye kuku. Kadhalika, chawa, funza, au kupe, hata ashibe, aridhike, na kunenepa kiasi gani, hatamzidi ng’ombe au mbuzi amnyonyae na kumtegemea. Aliyebebwa asijifyatue na kumfyatua punda ambebae. Kwani, kuna wakati punda atajifyatua au kufyatuliwa na kumfyatua yeyote ajifyatuaye na kumfyatua. Niwambe walo juu wa chini wanaipata. Acheni kuwajifyatua na kuwafyatua mafyatu wangu hata kama wamegoma kufyatuka na kuwafyatua wafyatuzi wao.
            Kuanzia sasa, mwanasiasa atakayejifyatua na kufyatua matusi au vitisho, lazima akamatwe na kufunguliwa mashtaka na hatimaye afyatuliwe kwa kufukuzwa ulaji na kuzuiliwa kushiriki sanaa za kisiasa. Hapa, wanene uchwara wanaojifyatua na kujitoa ufahamu na kuwa hamnazo wajiandae. Nitawafyatua kama sijawahi kuwateua ua kuwajua. Fyatu nimefyatuka kweli kweli. Sina haja ya kulilia haki na usawa wakati mafyatu wangu wakifyatuliwa na wale waliopaswa kufyatuliwa kwanza. Inakuwaje nguruwe amfyatue ngiri au mbwa amfyatue mbwa mwitu wakati wote ni sawa? Hivi, chawa au kupe na ng’ombe, nani wa kumcheka nani?
            Rasmi, nafyatuka na kutangaza. Fyatuyeyote munene atakayevunja au kukiuka maadili kama vile uadilifu, uwajibikaji, matumizi mazuri ya njuluku na ofisi za mafyatu, nafyatua. Atakayeingiza sanaa za kisiasa kwenye utendaji wa umma, nafyatua. Atakayelewa madaraka na kuyatumia vibaya kuwafyatua wengine, nafyatua. Ni kufyatua kwenda mbele. Nimegundua. Nisipofyatuka na kufyatua, naweza kufyatuliwa kwa sababu ya mafyatu niliowateua wawatumikie mafyatu wakaishia kujifyatua na kuwatumia. Ofisi mlizo nazo si baba yenu wala zenu. Ni za mafyatu. Mjue. Mlizikuta mtaziacha. Hivyo, hakuna haja ya kujifyatua na kuwafyatua wengine mkijihadaa kuwa hamtafyatuliwa. Mtafyatuliwa tu.
            Mafyatu wanaotumia unene wao kuwatisha mafyatu wakae wakijua. Wanaowatoza rushwa, wajue. Wanaoibia miradi ya maendeleo, wajue. Nitawafyatua kama siwajui. Haiwezekani mafyatu wachache waishi peponi wakizungukwa na mafyatu wanaonuka ukapuku nami niangalie au nisifyatuke na kuwafyatua. “Fyatua uwafyatue wengine ufyatuliwe” ndiyo kauli mbiu ya BASATER.
            Kwa vile mie ni kiongozi bora, nataka kuanzia leo nisikie maneno matamu kama vile kujali, kuwajibika, ukweli, unyenyekevu, huruma, stahiki, na mengine kama haya. Sihiitaji kufyatuliwa kw akusifiwasifiwa ujinga na uzwazwa. Hii nayo ni aina ya ufyatuaji uchwara. Mtanisifiaje wakati mnawafyatua mafyatu wangu? Nasema wazi kabisa. Nimefyatuka. Sitaki sifa. Nataka matokeo tena haraka kabla sijafyatuka na kufyatua.
             Kuanzia sasa, nitaanza kuangalia hata miili ya wateule wangu. Watakaonona kwa kuwafyatua mafyatu huku wakifutua kotekote, nitataka maelezo kabla ya kufyatuka na kuwafyatua. Nikikuteua, kwanza, nakutuma kwa daktari wangu wa ufyatuaji apime uzito wako. Baada ya miezi sita kwenye ulaji, unapimwa tena. Ole wako uwafyatue mafyatu wangu uongeze uzito ukutwe unjaza. Utanipiaa sababu zinazoridhisha. Vinginevyo, jiandae kufyatuliwa kama unavyowafyatua wengine.
            Pia, nitaanza kufuatilia namna ya wateule wangu wanavyoupara. Unakuta fyatu, kabla ya ukutreuliwa halikuwa hata na pea moja ya suti. Muda mfupi, unakuta linabadili suti kama halina akili nzuri. Mengine yamezaliwa na kukulia kwenye nyumba za kupanga. Pndipo nikiyateua, unasikia yamefyatua mafyatu na kumilki mahekalu na misururu ya ndinga za bei mbaya huku mengine yakiongeza kila kitu hadi masssaburi. Mafyatu wa namna hii wajiandae kufyatuliwa kama nyani tena bila kuwaangalia usoni nikaona huruma na kushindwa kufyatuka na kuyafyatua.
            Wote wanaofyatua mafyatu wangu utadhani mwisho wa dunia au kuwafyatua utadhani wataishi milele, wajiandae kufyatuliwa. Pia, wale wanaoatumia dini zao duni kujifanya wananitetea nao nawafyatua kwa sababu haya si maadili ya Fyatuland. Kama ni maadili si chochote wala lolote bali ukosefu wa busara, kumbukumbu, na ubunifu. Kusifia na kutetea kunaanza kugeuka dili kwa mafyatu wasio na maadili watakao kunifyatua kifala na kizwazwa. Mkome. Ng’oo. Dawa yenu iko mekoni na chuma kiko motoni. Hamnifyatui. Kweli, inaingia akilini kutetea fyatu kama mimi asiyeogopa kitu? Kumbe naweweseka usingizini!!
Chanzo: Mwananchi j'tano leo.

No comments: