The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Sunday, 15 November 2026

Wanandoa fundisheni watoto usafi mapema

Kama wanandoa na watatafiti wa masuala ya ndoa, huwa hatuna dogo linapokuja suala la ndoa. Katika kuongea, kusoma, hata kuwasikiliza baadhi ya wanandoa wenzetu, tumegundua vitu vidogo ambavyo vinaweza kuwa na madhara katika maisha ya ndoa hata watoto baadaye.
            Leo, tutaongelea suala la kuwafundisha watoto wenu usafi ili uwe sehemu ya mazoea yao hata watakapokuwa watu wazima wawafundishe na kuwarithisha watoto wa. Tunajua. Kuna watu wengi wana mazoea mabaya ya kulala bila kuoga wala kupiga mswaki kwa vile  hawaoni wala kujua madhara  Tulishawahi kujadili suala hili kwa wanandoa ila si kwa watoto wao.
        Katika kudurusu kwetu, bila kutarajia, tuligundua kuwa kuna mazoea, au tuseme mila au kutojua vinavyoweza kuwa hatarishi kwa watoto baadaye. Mfano, kuna watu walisema wana mazoea ya kulala bila kuoga. Walitushangaa tulipowashangaa kwa kulala bila kuoga. Tulishangaana. Kama haitoshi, wapo waliosema kuwa huwa wanalala bila kupiga mswaki! Nao tuliwashangaa nao wakatushangaa kwa kupiga mswaki kabla ya kulala. Wapo waliosema kuwa wanaamini kuwa wakipiga mswaki kabla ya kulala, watakosa usingizi jambo ambalo si la kweli bali imani pofofu na mazoea mabaya. Je, ni wanandoa wangapi wanafanya au kuyaamini haya?
            Japo kwa wanaofanya hayo juu ni kutokana na mazoea na kutojua, yanaweza kuwa madhara fichi kwa afya zao. Pia, yanaweza kusababisha madhara kijamii. Mfano, unapolala bila kuoga au kupiga mswaki, unaweza kusababisha nyumba kuwa na harufu mbaya asubuhi usijue kwa vile umezoea harufu hiyo. Isistoshe, unapolala bila kuoga au kupiga mswaki, unaweza kusababisha madhara yafuatayo kiafya na hata kijamii:
            Mosi, wanasayansi wanaonya kuwa unapolala bila kuoga, lazima mwili wako utatoa harufu mbaya tokana na kuwapo kwa bakteria mwilini wanaokula mafuta ya mwilini na kutoa harufu mbaya.
            Pili, kutooga kwaweza kusababisha kuvunjika kwa kinga ya ngozi na kuifanya ishambuliwe na magonjwa ya ngozi kwa urahisi. Magonjwa ya ngozi yanasababisha usumbufu na kuharibika kwa ngozi.
            Tatu, usipooga, mwili hujenga utando wa uchafu unaoganda kwenye ngozi ambao waweza kukusababishia kuwashwa na kukukosesha usingizi mbali na hatari na madhara mengine.
            Kama ilivyo kwenye kulala bila kuoga, pia, kulala bila kupiga mswaki kuna madhara kwako kiafya na kijamii.
Mosi, husababisha, kuharakisha, kurahisisha kusambuliwa na maradhi ya kinywa na meno. Kwa mujibu wa Shirikisho la Meno la Marekani (ADA) bakteria waliomo kinywani hutegeneza tindikali ambayo hutafuna na kudhoofisha ufizi na kuufanya uwe rahisi kuambukizwa magonjwa ya kinywa. Chukuta tahadhali mapema.
Pili, husababisha magonjwa ya fizi ambayo kuyatibu ni gharama na kunaweza kuwa kugumu tokana na mahali ulipo na uwezo wako wa kugharimia.
            Tatu,  husababisha kinywa kutoa harufu mbaya na ya kukera kiasi cha kuwakera wengine.
Nne, unapokuwa na kinywa kinachotoa harufu mbaya, licha ya kuwakera wengine, unaweza kukosa kkujiamini, kuhukumu wengine vibaya na mengine kama hayo ukidhani wanaringa au kukubagua kumbe ni harufu mbaya utoayo.
            Sasa tuje kwa watoto. Japo tuliwashangaa wanaolala bila kuoga au kupiga mswaki, ukweli ni kwamba yote ni matokeo ya malezi yanayojenga mazoea kama haya. Hivyo, wahusika wanaweza wasijue madhara ya wafanyayo au mazoea yao.
Kulala bila kuoga au kupiga mswaki ni matokeo ya malezi ya wahusika. Hapa, ndipo wanandoa ambao ni wazazi wanapoingia. Yawapasa kujua kuwu, kama wahenga waasavyo, mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo na mazoea hayana dawa bali kujitambua na kudurusu baadhi ya mambo ambayo yaweza kuonekana madogo lakini yenye madhara makubwa.
            Haiingii akilini mtu ushinde unakula, kunywa, na kufanya mengineyo ulale bila kuwa msafi.  Kwanini uoge asubuhi tu eti kwa vile unakwenda kazini au shuleni?  Usafi, licha ya kukufanya ujisikie vizuri, una faida kiafya, na unaweza kukufanya ulale vizuri.
Tusisiteze hasa kuhusiana na watoto. Japo, huwa hawasemi au kudhani hawajui, wana uwezo wa kujifunza mambo haraka na kuyashikilia. Hapa ndipo suala la mazoea linapojikita. Watoto hata wanyama ukiwazoesha tabia fulani, hata wakikua, huwa vigumu kuiacha.
            Tuhitimishe kwa kuhimiza wanandoa umuhimu wa kuwafundishe watoto wao tabia ya usafi na nyingine nzuri ili ziwafae baadaye wao na watoto wao. Mjue, ndoa ndiyo kiwanda cha baba, mama, wake, na waume wa vizazi vijavyo. Hivyo, wapeni mazoea, mila, na urithi bora.
Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: