The Chant of Savant

Wednesday 30 October 2013

Rais Kikwete watimue Chikawe na Wassira






MAWAZIRI  Mathias Chikawe (Sheria na Katiba) na Stephen Wassira ( Waziri wa Nchi Ofisi ya rais Mahusiano na Uratibu) ni watu wasioisha vituko. Alijua kuwa waziri Wassira angewaambia wapinzani kuwa wanalilia kwenda Ikulu kunywa juisi kana kwamba juisi ni kitu kikubwa? Inashangaza mtu mzima kiumri na mwenye madaraka kuhangaishwa na udohoudoho namna hii.
Naye Chikawe alitoa mpya aliposema kuwa atamshangaa rais Jakaya Kikwete kama hatasaini muswada wa katiba uliochakachuliwa. Hivi karibuni Chikawe alikaririwa akisema, “Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani.” 
Hakuna anayejua kigezo alichotumia kiasi kuonekana kama anamfanya rais mjinga kiasi hiki. 
Rais hawezi kusaini au kutosaini muswada kwa kuogopa watu wasimshangae. Kinachomsukuma rais kusaini au kutosaini muswada ni sheria. 
Naye Wassira alikaririwa akisema, “Hawa tumewalea siku nyingi na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa Ikulu.” Kama tutauangalia ukweli bila makengeza na miwani ya mbao, kati ya wapinzani na Wassira nani amefugwa? 
Kuna dhana kuwa Wassira alikuwa akijitahidi kuwashambulia wapinzani ambako alitokea ili aonekane kuwa hana uhusiano nao tena. 
Wengi wanadhani kuwa Wassira anaiandama Chadema kwa maslahi yake yaani aonekane hana uhusiano nao tena ingawa kwa wanasiasa lolote linawezekana.  Kinachoshangaza ni ile ya Wassira kuwaandama wapinzani utadhani yeye hajawahi kuwa mpinzani. Ama kweli ‘nyani haoni kundule’.  Wakati mwingine ya nyani kutoona nonihino lake inaweza kutafisriwa kama unafiki au uchangudoa wa kisiasa.  
Ila ni vizuri Wassira na wenye mawazo kufu na mfu kama yake wakafahamu kuwa si wapinzani wote wako kwenye upinzani kwa ajili ya kukidhi tamaa na njaa zao. 
Wapo ambao ni makini na wana nia ya kuleta mabadiliko kwa Taifa lao. Mambo huenda yakibadilika.  
Hata hivyo Wassira anapaswa kuelewa kuwa wapo wapinzani walioko ndani ya chama kama yeye. Ila si vizuri kudhani wote ni kama yeye. Nani kwa mfano alijua kuwa Augustino Lyatonga Mrema au Maalim Seif Sharif Hamad wangekuwa na uswahiba na CCM?
Kinachofanya watu tuwashangae watu kama Chikawe wanaomshangaa rais kwa kukataa muswada uliochakachuliwa ni ile hali ya kuwa wanasheria wasiojua sheria. Inashangaza sana kuona mtu kama Chikawe waziri wa sheria na mwanasheria kitaaluma kufikiri kisiasa badala ya kitaaluma. 
Inashangaza kuona watu wanaopaswa kulinda katiba kama Chikawe ndiyo hao hao wanaotaka ichezewe na kila kundi la wahuni eti kwa vile ni wenzao. Nchi yetu haiwezi kuendeshwa kama kikundi cha ngoma ya mdundiko au baa ambapo kila mtu hujifanyia atakavyo. 
Hatuwezi kuwa wote vipofu tukiachia hatima ya nchi yetu kwenye sera za ubabaishaji na utendaji wa ajabu ajabu kama wabunge kukubali kutumiwa kuchakachua muswada ambao kimsingi ungewaletea ukombozi kama Taifa.  Isitoshe, suala la kujua kuwa muswada wa Katiba Mpya umechakachuliwa halihitaji kuwa na shahada ya sheria bali akili ya kawaida, ‘common sense’.  
Kuna wakati watu wanashangaa watu kama hawa waliteuliwa vipi wakati wanaonyesha kukosa uelewa mdogo ukiachia mbali ujuzi wa kuweza kuwa mawaziri. Tunajua kuwa wengine wamesoma tena nje kiasi cha kufikia kuwa na ‘Masters degree’. 
Je ni kwanini matendo na matamshi yao hayafanani na elimu wanayodai kuwa nayo au ni yale ya kutumia majina ya vyuo vya nje kuonyesha wana sifa kama siyo kughushi au kununua shahada za kwenye mtandao.
Kinachofanya watu wawashangae zaidi mawaziri hawa ni kuongelea mambo yasiyolingana na umri na nyadhifa zao ukiachia mbali mambo yenyewe kutoingia akilini. 
Kwa mfano, Ikulu na juisi wapi na wapi au kumshanga mtu anayefanya jambo ambalo ni la maana?  
Kuna haja ya mawaziri wetu kujitofautisha na wapiga debe, wavuta bangi, waimbaji taarabu au ‘rap’ au machinga wa pale mtaa wa Kongo. Kushindwa kufanya hivyo hupelekea watu kuamini kuwa wahusika wamefilisika kisiasa.
Kwa mawaziri kushindwa kutenda kama nyadhifa zao zinavyowatuma na ukiachia mbali kujiaibisha wao na bosi wao, wengi wanadhani wakati wa rais Kikwete kuwatimua ili kulinda heshima yake na Serikali ni sasa. Haiwezekani Serikali kuendelea kuwavumilia wahuni ikashindwa kuonekana ya kihuni kama wao. 
Maana Waingereza husema, nionyeshe marafiki zako nikwambie wewe ni nani. 
Hatuamini kuwa Serikali yetu na rais wake wamefikia kiwango hiki cha huruma na hasara. Hatuamini kuwa akina Chikawe na Wassira ni watu wanaopaswa kuonyeshwa iwapo mtu atamtaka rais Kikwete aonyeshe wenzake aambiwe yeye ni nani.
Tumalize, kwa kumtaka rais Kikwete asiishie kuwashangaa na kuwavumilia akina Chikawe na Wassira. 
Badala yake awawajibishe ili kulinda hadhi yake. Inabidi awaonyeshe kuwa yeye kuamuru katiba iandikwe upya hakuwa anataka kujiridhisha wala kufanya majaribio bali aliona hatima ya Taifa. 
Pia akina Chikawe na Wassira wanaomshangaa rais kwa kutimiza wajibu wake kama kiongozi wa nchi wanapaswa, kuogopwa kama ukoo. Kwa ninavyojua, rais Kikwete lazima awawajibishe ili kuwaonyesha Watanzania kuwa mambo yamebadilika. Atuonyeshe kuwa siasa za mazoea na kubabaisha zimeishapitwa na wakati na siyo stahiki na staili yake.
Kwa ufupi ushauri wetu kwa rais ni huu. 
Rais usiwavumilie nyani utavuna mabua. unayekaribia kumaliza muda wako ni wewe na ni wewe huyo huyo uliyeapa kulinda katiba ya nchi na si hao wapambe ambao wengi wao huwa ni nuksi. Rais Kikwete tuondolee kadhia. 
Wawajibishe mawaziri mzigo kwenye baraza lako la mawaziri kama hawa walioshindwa kutimiza wajibu wao kwako na kwa Taifa. Usiwape nafasi wakushangae au kukutisha.

Chanzo: Dira ya Mtanzania Oktoba 2013.

No comments: