BAADA ya kugundua kuwa kuna mchezo mchafu wa kuwachukulia wachovu kama mataahira huku wahusika wakizidi kuiba njuluku zao, kijiwe kimekuja na suluhisho la kudumu.
Mipawa analianzisha, “Nimecheka kusikia kuwa dokta Eddie Hoshea na Mura Freddie Weelema nao ni wajumbe wa kamati ya kufuatilia njuluku iliyofichwa Uswizi.
“Yaani unampa mbwa kazi ya kulinda nyama halafu unategemea kuwepo nyama au mifupa?”
Kapende anachomekea, “Hizi nazo ni sanaa na ngonjera ambazo wanasiasa watatumia kujipatia kura ya kula na ujiko kama anavyofanya Mzito Kabwela ambaye alituahidi kutaja lakini akawa anajikanyaga kama Dokta Mwakiwembe na wauza bwimbwi.
“Kwa nini msifunge madomo yenu na kutafuta mbinu nyingine ya kupata ulaji badala ya kutugeuza majuha wakati sisi siyo?”
Kapende anaamua kupasua jipu. Anasema, “Mimi sasa nataja potelea mbali liwalo na liwe.
“Walioficha njuluku Uswisi wanajulikana. Leo mie nataja. Nambari wani ni Endelea Chengaaa, Idiiliishua Rashidu, Niziro Kadamage, Rahasttamu L’ Aziz, Billy Ngeleza, Mood Daweje aka bilionea toka kaya kapuku, Pitia Noni, Eddie Ewassa, Njaa Kaya, Bazil Pesatatu Mrambaramba, Ben Dugong Makapu na nkewe na Dan son of Johah.”
Wakati tukiendelea kusuburi ataje zaidi si akamalizia kwa kusema, “Wengine nitawataja next time.”
Pamoja na kutuacha kwenye suspense Kijiwe kinamshangilia kwa hoi hoi na nderemo angalau kwa kuthubutu kutaja huku kikisema, “Wanyongwe au wachomwe moto kama vibaka.”
Kelele zimehanikiza hadi wapita njia wanaopenda kushangaashangaa wanasimama na kushangaa. Bahati yetu wakati watu wakitushangaa bila kujishangaa hakuna ndata aliyepita.
Maana, wanavyopenda kujitiatia asingesita kuuliza kunani.
Baada ya kijiwe kutulia Mipawa anasema, “Umemsahau Kanji?” Anasema kwa utani huku akikamua kombe lake la tangawizi.
Maana leo zimemtembelea kiasi cha kuachana na kahawa na kunywa tangawizi. Mwisho wa mwezi huu ati.
Kanji kashikwa pabaya. Anajitetea, “Mimi iko clean. Haina pesa kule Swizz. Kama napata pesa kuba kama hiyo kwa nini hapana hamia London bwana?”
“Kanji usitifanye majuha nawe. Kwani wote walioficha njuuku Uswisi lazima wahamie London?
“Ingekuwa hivyo mbona kina Ostam L’Aziz wangeishaishia London kama siyo Iani (Iran)?” anang’aka Mgosi Machungi huku akimtazama Kanji kwa dharau ya kisambaa.
Msomi aliyekuwa kimya akishangaa jinsi wanywa kahawa walivyoamka anaamua kutia guu, “Hakuna kitu kinanisononesha kama kushuhudia wanakaya tukikaa na kuangalia wakati tukiibiwa kila uchao kana kwamba hii pesa si yetu. Kitaalamu tunasema kuwa ‘power is always fluid. Like water, even air, it can move from one hand to another’.
“Kimsingi mali tunayo tunaikalia. Jamani tuamke na kuhakikisha tunazuia ujambazi huu wa mchana vinginevyo tutaliwa kila mara.”
Mzee Kidevu anaamua kumkumbushia itifaki. “Msomi taratibu, kumbuka itifaki Kikameruni hicho kaka.”
Mipawa na Mijjinga wananong’ona kitu kuhusiana na mzee Kidevu kuchukia Kikameruni wakati akikumbatia Kiarabu.
Mzee Kidevu anasema, “Eti mali tunayo tunaikalia? Tuombe msamaha Msomi.”
“Msomi umesema vyema. Mimi si maskini. Nimesikitishwa na hawa wezi. Hebu fikiria. Ushoto tunazalisha matunda na yanaoza.
“Hatina kiwanda hata kimoja. Je, huku si kutifanya maskini bila sababu yoyote zaidi ya upofu na ulafi?
“Hivi hii njuluku ingetiwezesha kujenga viwanda au mashule hata baabaa ngapi?” Machungi anazoza.
Anaendelea, “Tiamue. Tiende huko mawizaani. Tiwakamate na tiwafukuze wanaotiibia kila siku kana kwamba tu mataahia au vipofu. This is too much.”
Bi Sofi Kanungaembe ambaye hivi karibuni alilizusha kule kwa kina Twambombo anakwanyua mic, “Siungi mkono utoroshaji wa fedha za umma. Ila ningeshauri tumpe muda mtukufu rais afanye uchunguzi na achukue hatua.”
Mijinga anaamua kukatua mic, “Bi Sofi acha nikuingilie.”
Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anamuonya, “Chonde chonde Mijjinga unataka umuingilie bibi wa watu kwa kosa lipi?”
Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi Mbwamwitu anavyotafsiri vibaya kusudio la Mijjinga. Anyway, ndiyo Kiswahili chenyewe. Unasema hili wanafikiri lile.
Mijjinga anajitetea, “Basi ngoja nidandie.”
Kabla ya kuendelea Mpemba anasema, “Loo umeona kuingilia haitoshi sasa waamua dandia ami!”
Mijjinga anapuuzia utani na kusema, “Sasa unazidi kuniudhi. Rais achukue hatua ya nini iwapo serikali yake imekalia kashfa hii kwa miaka yote? Umesahau EPA mara hii! Hujui kuwa nyingi ya fedha iliyofichwa nje inatokana na MaEPA na Ma Richmonduli Kagoda na Meremeta rada na ndege mkangafu ya rais?”
Machungi anadakia, “Mijjinga usitikumbushe hiyo EPA ambayo ni mahepe. Huoni yale majambazi ya EPA yanaitwa watukufu na majina mengine makubwa. Hivi sisi timeogwa na nani?”
Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anachomekea, “Sisi hatujalogwa. Umelogwa wewe ambaye bila kumpiga mtu zongo hakukaliki.
“Dog Mwitu tiheshimiane ohooo! Wewe mtoto mdogo ambaye timecheza na mama yako inawezaje kusema eti timeogwa? Au unataka tikupige zongo la ukweli? Sema tikushughuikie sasa hivi.”
Mbwa Mwitu kuona yamekuwa hayo anaamua kujitetea, “Mgosi ndugu yangu hutaniwi?” Mpemba ambaye alikuwa kimya muda mrefu akisoma habari za Mzito Kabwela kutibua dili la majambazi wanono anampa gazeti Mchunguliaji na kukamua mic, “Yakhe mie nimekaa kimya nda nrefu. Sasa acha nipitishe fatwa wallahi. Mie naona tuache kulalama. Kama alivyosema Mgosi, twende huko maofisini tuwahukumu hawa wezi wanaojiona wana mamlaka juu ya kila kitu na kila mtu wakati mwenye mamlaka ni Subhana Wa Taala mwenyewe. Twangojani wakati kila kitu chaliwa? Mwataka nasi tuliwe?”
Kabla ya kumaliza Mgosi Machungi anachomekea, “Mgosi usitiletee mambo ya popo bawa hapa ohoo!” Mpemba anajihami, “Hapa mie sifanyi utani yakhe. Mambo ya popobawa yeshapitwa na wakati na waliofanyiwa ushenzi si mwawaona wakiumbuka wengine kupofuka?”
“Du bado hujamsahau Kamandoo wenu ambaye siku hizi ni apeche alolo huku akionekana kusononeka kwa aibu kutokana na ujinga aliofanya!” anachomekea Mijjinga.
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shangingi lililokuwa limembeba Mgimua.
Kila mtu alichukua kikombe chake na kuanza kulimwagia kahawa huku akilirushia kashata na tangawizi huku tukisema, “Acha siasa na ngonjera rejesha pesa yetu mliyoiba na kuficha Uswasi.”
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 30, 2013.
No comments:
Post a Comment