Julius Kambarage,
Naomba nawe nilonge,
Wewe mwana wa Mwisenge,
Sikia salamu zangu.
Wewe mwana wa Burito,
Usikie wangu mwito,
Ninaleta hoja nzito,
Sikia salamu zangu.
Kimwili hauko nasi,
Kiroho uko na sisi,
Ni yako kadamnasi,
Naleta salamu zao.
Daima twakukumbuka,
Mema’yo twayakumbuka,
Jinalo nalitamka,
Umeacha Tanzania.
Ulionyesha mfano,
Ulijenga fungamano,
Ulileta Muungano,
Dua tunakuombea.
Uliitoa elimu,
Kwa sasa ni uhujumu,
Mitaala ya haramu,
Isofunza maadili.
Elimu ya sasa pesa,
Kama huna waikosa,
Wenye nazo wanatesa,
Wajinga waongezeka.
Afya uliilinda,
Sasa mkandamkanda,
Wa'ne kimoja vitanda,
Sasa wagonjwa walazwa.
Japo wewe marehemu,
Bado una umuhimu,
Ulipo huko kuzimu,
Pokea zangu salamu.
Waja wangelirudishwa,
Mauti wanapofikwa,
Mamia wangejitoa,
Urejee Kambarage.
Urejee kiongozi,
Uliye wetu azizi,
Uje tutoke majonzi,
Njoo tufute machozi.
Tangu ulipoondoka,
Mambo yamebadilika,
Mengi yaliharibika,
Umma unakukumbuka.
Miiko ya uongozi,
Ilikufa kama inzi,
Ilishatiwa kitanzi,
Ulizuka udokozi.
Ukidai ifuatwe,
Utayeandamwa wewe,
Kwani mbaya ni wewe,
Kutaka ziba riziki.
Usawa umetoweka,
Yamezuka matabaka,
Majambazi na vibaka,
Nchiyo yajiibia
Wapo waliotamka,
Mafisadi watasaka,
Hili linatia shaka,
Matendo yaadimika.
Kudai wavaa njuga
Kusema unajipanga,
Hadi lini tajipanga?
Hili hawataki lijibu!
Dhahiri tumedanganywa,
Twaendelea kunyonywa,
Mengi nayo yamesemwa,
Hakuna linofanyika.
Misingi uliyoweka,
Baba imeporomoka,
Akiba uliyoweka,
Baba walishaiuza.
Madini uliyotunza,
Zamani yalishauza,
Ardhi uliyotunza,
Hatimaye hatujui.
Twaona wenye rupia,
Sasa wanainyatia,
Kwa vile mambo huria,
Zake zinahesabika.
Wanena watajaribu,
Mikataba kurekebu,
Kazi hii ya sulubu,
Wapo wanomhujumu.
Hapa upo ufisadi,
Sasa wageuzwa jadi,
Kinachouma zaidi,
Hakuna anayejali!
Tumeishia ahadi,
Wanadai ushihidi!
Rongo nazo mardudi,
Hali haitabiriki.
Utu uliohimiza,
Sasa tumeupoteza,
Tamaa imechomoza,
Ya kuabudia vitu.
Wamezuka paka watu,
Watula kama tunutu,
Tena ni kundi la watu,
Huwezi kuwadhania.
Wavaa ngozi ya chui,
Watu hawa ni marui,
Ni wakubwa maadui,
Wavamia kama ndui.
Mwalimu hutaamini,
Ukijua ya sirini,
Wezi hata maruhuni,
Waitwa waheshimiwa!
Tuliufanya msako,
Tuligundua vituko,
Mwalimu ni sikitiko,
Wengi hungewadhania.
Kumbe wakaanga sumu,
Jamii kuihujumu,
Ni wakubwa madhalimu,
Ingawa wanayo mali.
Wamo mamilionea,
Mali wamejichumia,
Mitutu wametumia,
Ukwasi kuufikia.
Wavaa nguo aghali,
Ukiwaona jamali,
Kumbe ni wakubwa nduli,
Kiwaona pisha mbali.
Wengine wauza unga,
Unukao ja kigaga,
Mahekalu wamejenga,
Kwa mapato ya haramu.
Kwa pesa zao za unga,
Wananchi walihonga,
Bungeni wanajimwaga,
Mwenye pesa si mwenzio.
Wana sura kama watu,
Tabia zao za chatu,
Siyo watu ni viatu,
Pia ni minyama mwitu.
Wengi wao wafadhili,
Ni watu walonawiri,
Kumbe hicho ni kuvuli,
Ndani kuna uoza.
Wang'aa kama kaburi,
Lililojengwa vizuri,
Kumbe ndani si utuli,
Ni harufu na uoza.
Rushwa sisemi Mwalimu,
Kwani ni nyenzo muhimu,
Kuufikia utamu,
Lazima utoe kitu.
WOSIA.
Mwalimu uliusia,
Yabidi kufikiria,
Pesa wanayotumia,
Si siri wanatumiwa.
Sisi wakitununua,
Wamenunuliwa jua,
Mbona yalishatokea,
Mwalimu tulikumbuka.
Naomba ujue hili,
Limezuka wimbi hili,
Kwani latukwaza hili,
La kuibia jamia.
Benki kuu si salama,
Ilishaonja kiama,
Wezi wameiandama,
Tukidai watuzoma!
Hukumuacha Kagoda,
Huyu sasa ni kidonda,
Ameushika ukanda,
Atenda anavyotaka.
Wizi mkubwa ajabu,
Majizi waliratibu,
EPA ndiyo maghusubu,
Pesa walijichotea.
Walitisha uchaguzi,
Kageuka uchafuzi
Wizi na uchakachuzi
Wenye pesa walishinda.
Rais tukichagua,
Mwalimu yabidi jua,
Mengi atayoibua,
Kweli yatia kinyaa.
Nonihi atasimama,
Ataka naye kuchuma,
Ataunda chake chama,
Mradi apate kula.
Ataanzisha miradi,
Ili chumo afaidi,
Utamwona ajinadi,
Kwa kila alipo baba.
Si mkewe si mwanae,
Wote watachuma nae,
Watatumia jinale
Ili kujitajirisha.
Ikulu si takatifu,
Ilishajaa uchafu,
Imegeuka turufu,
Ya kutafutia mali.
Mwalimu uliyaona
Nasi sasa twayaona,
Hadhi haipo tena
Ikulu chaka la wizi.
Ataingia ni mwema,
Kumbe ndani ni mnyama,
Mapesa atakachuma,
Kwa kuudanganya umma.
Mkewe hata watoto,
Wataanza michakato,
Wakikisaka kipato,
Ikulu wakitumia.
Atakusanya mapesa,
Utamwona akitesa,
Atafanya vyote visa,
Yuko karibu na
"Jua”.
Tuna vyama utitiri,
Sivikumbuki vizuri,
Wengine wasema dili,
Bora itue riziki.
Tumepigwa bumbuwazi,
Yametujaa majonzi,
Wako wapi wakombozi,
Mtupanguse machozi?
Wamejaa mabazazi,
Uliowaita wezi,
Wanaiba wazi wazi,
Wameviuza vizazi.
Nyumba zetu wameuza,
Viwanda wamechuuza,
Nchi yetu imeoza,
Waja tunapata tabu.
Mwalimu huko uliko,
Jua tuna unguliko,
Kwani hatuna mashiko.
Kwani letu hangaiko.
Siasa sasa biashara,
Kwa wananchi hasara,
Kila ninapodhikura,
Mwalimu nakukumbuka.
Nyoyo zimesononeka,
Hakika zimenyongeka,
Hakika zimepigika,
Hatunapo pa kushika.
Madini yanatoweka,
Wachimba wanavyotaka,
Wale wenye madaraka,
Waitwa wawekezaji.
Wakishayachimba humo,
Wanayaacha mashimo,
Hatari iliyo humo,
Nani anaifahamu.
Wanaacha humo sumu,
Mapesa zitagharimu,
Kuzisafisha sehemu,
Walipoiacha sumu.
Misitu inatoweka,
Wenye nazo waifyeka,
Miti mingi wamefyeka,
Wauze magogo nje!
Tunayo mihadarati,
Yaletwa kila wakati,
Polisi hawakamati,
Wanamzidi akili!
Wana 'serikali' yao,
Mkubwa mfumo wao,
Kila mtu mtu wao,
Wajua kumwaga pesa.
Rais tumtafute,
Asiye nao fungate,
Anosimama kidete,
Wapi nako tumpate?
Wengi wameshachafuka.
Tunayo bahati mbaya,
Katika masuala haya,
Hakuna wanalofanya,
Bali kujirusha rusa.
Muendee muulize,
Kwanini mambo yaoze?
Viapovye mueleze,
Amefanikisha nini?
Atajibu kwa ukali,
Vitendo viwe aghali,
Azue lile na hili,
Mradi uende muda.
Haramu sasa halali,
Kwani nani anajali?
Kinachotakiwa mali,
Hata kwa kuua mtu.
Tumegeuka wa hovyo,
Umetawala uchoyo,
Kila kitu hovyo hovyo,
Ndo maisho tulo nayo.
Usawa ulohimiza,
Haki ukisisitiza,
Sasa kimetanda kiza,
Tuipate wapi haki.
Kwa polisi siioni,
Kwa hakimu siioni,
Kwa DC siioni,
Haki yangu iko wapi?
Kwa Rais kuna haki,
Kumfikia mikiki,
Nitaiweza mikiki?,
Ili niipate haki?
Tulokuwa twazomea,
Sasa wanatukemea,
Pengine watuzomea,
Wameishatuiibia.
Watuona hamnazo,
Japo washiba masazo,
Tusipoacha mchezo,
Twauzwa tukijiona.
Twaambiwa ni mafala,
Bongo zetu zimelala,
Tunaomba Hala hala,
Uliepushe balaa.
Tumepata wachuuzi,
Waja na utandawazi,
Tena ndiyo viongozi,
Waongoza angamizi.
Tumepiga makelele,
Kulalamikia ndwele,
Kuuza hiki na kile,
Hawataki kusikia.
Wanao wajumbe wao,
Walindao mali zao,
Wapewa mgao wao,
Wawauze watu wao!
Wanajenga mahekalu,
Wanatangaza kufuru,
Nyumba zenye maru maru,
Migari ya bei mbaya.
Ajabu wamezungukwa,
Na watu waliozongwa,
Na ufakiri mkubwa,
Walosababisha wao!
Wanatibiwa Ulaya,
Wanafulia Ulaya,
Kila kitu ni Ulaya,
Wala hawaoni haya!
Na si wao peke yao,
Wake na watoto wao,
Hata mahawara zao,
Wenda na majibwa yao.
Kipato hakilingani,
Na mapesa mfukoni,
Hapa hakuna uzani,
Hata apime kiwizi.
Mtu ameajiriwa,
Laki moja analipwa,
Lakini akitumbua,
Atumbua milioni!
Wamehodhi kila kitu,
Miili na roho zetu,
Wachuuza kila kitu,
Nao pia wajiuza!
Tunaangalia tu,
Kwani hatunalo letu,
Zimepita zama zetu,
Ulipotoka Mwalimu.
Darasalo limefungwa,
Viti vyaliwa na mchwa,
Wanafunzi tumesundwa,
Katika utandawazi.
Wale ulowaamini,
Ukawapa usukani,
Gari liko msambweni,
Walitosa mtaroni.
Wale ulowatetea,
Wamekutia fedheha,
Siyo watu bali mbweha,
Ashakum si matusi.
Watu gani bila utu?
Wahujumu nchi yetu,
Wameshauzika utu,
Mpaka aje Rais?
Yuda wamejigeuza,
Kazi ni kutuchuuza,
Kama Yesu wanauza,
Kwani wachelee nini?
Paka umeshaondoka,
Panya wanatononoka,
Wala wanachokitaka,
Nani wa kuwazuia?
Hali hii ni hakika,
Paka anapoondoka,
Mapanya yatafutuka,
Kitiche yatakalia.
Mengine yakigugune.
Mtego umekatika,
Kizazi chahangaika,
Mapanya wa kuwasaka,
Wanananchi wamtaka.
Heshima uliyoleta,
Nchi ikametameta,
Taratibu yaondoka,
Maafa yatafuata.
Huwezi ukaamini,
Leo twaanza udini,
Juma amuhofu Joni,
Huu ndiyo ukweli.
Ujimbo umefufuka,
Ukabila wainuka,
Makundi yanajengeka,
Peke Rais 'tayaweza?
Yamezuka matabaka,
Ya wenye pesa kudaka,
Na wale waliochoka,
Huu ndiyo ukweli.
Kupo pia kujuana,
Pamoja na kulindana,
Usawa sasa hakuna,
Mambo yanaharibika.
Imezuka mitandao,
Ya wale wajuanao,
Wanafanya vitu vyao,
Tuliobaki tulie.
Kila kitu ni upatu,
Changia upate kitu,
Kama Baba huna kitu,
Wewe chungulia tu.
Hili siyo jambo jema,
Kwangu naona nakama,
Hapa twachuuza umma,
Kesho yake ni hukumu.
Mwalimu uliongoza,
Wenzio waliburuza,
Nchi uliitangaza,
Uloacha waliuza.
MANGUNGO WA LEO.
Mangungo wa Msovero,
Walitutia kihoro,
Waliuacha uchuro,
Twakulilia Mwalimu.
Leo Mangungo ni wengi,
Madhara yao ni mengi,
Wapo wanatesa wengi,
Kwani wanauza wengi.
Mangungo pande kauza,
Hawa nchi wameuza,
Tangu Tanga hadi Mwanza,
Hakuna waliposaza.
Wengine waliahidi,
Ili watu wafaidi,
Kilogomba ni juhudi,
Japo mzigo mzito.
Wewe ulijenga utu,
Wao wanajenga vitu,
Wanaabudia vitu,
Huchuuza kila kitu.
Hekalu ulilojenga,
Ni unyonyaji kupinga,
Uliufuta ujinga,
Na misingi uliweka.
Tuliibiwa mchana,
Twachuuza tukiona,
Wala aibu hawana,
Walifanya watakavyo.
Hukumuibia mtu,
Wala kudhulumu mtu,
Jamani wale si watu,
Wanouza hata utu!
Kibaya hawaridhiki,
Tena hawaambiliki,
Wizi wao si wa dhiki,
Bali ni ubaramaki.
Hukupenda ukoloni,
Leo tuna ukoloni,
Asemacho mkoloni,
Sisi ni kutekeleza.
Tumeyauza mabenki,
Kwa dharau na mikiki,
Kwa vitisho tiki tiki,
Wakienda kukuwadi.
Madege walinunua,
Na Rada walinunua,
Mungu aliwaumbua,
Majitu haya ni feki.
Tulifanyiwa vituko,
Na kugeuzwa vituko,
Tumechuma sononeko,
Yetu ni mahangaiko.
Ngonjera tuliimbiwa,
Na majina kutungiwa,
Mchana tukizomewa,
Kisa kutetea chetu!
Tuliambiwa wavivu,
Tulo na tupu mafuvu,
Ni wa kike wetu wivu,
Kwani tu wapumbavu.
Ivumayo haidumu,
Ipo siku itatimu,
Ipasukie kuzimu,
Ndivyo ilivyotokea.
Maungo haisitiri,
Na si nguo ya fahari,
Waazima unawiri,
Kesho wanakuchojoa.
Waliojilisha pepo,
Wakadharau viapo,
Walitoka kama popo,
Kwenye kiza cha usiku.
Walijiona wajuvi,
Wakaongeza na chumvi,
Walituita wachimvi,
Waulize wako wapi?
Wale ulotuachia,
Mwalimu tuliumia,
Mambo walojifanyia,
Ukijua tachukia.
Cheo lifanya biashara,
Nchi litia hasara,
Ni kweli si masihara,
Mwalimu tumeyaona.
Walikuwa limbukeni,
Habithi sina kifani,
Mambo yao kama nyani,
Kuishi kinyani nyani.
Waliyavamia mambo,
Wakayalamba makombo,
Waliondoka na shombo,
Mambo yalikwenda kombo.
Watu wasoambilika,
Pia wasioridhika,
Kila kitu walitaka,
Pesa yetu walipoka.
Nunda walijeuza,
Wapate kutumaliza,
Walitujazia kiza,
Wapate kutuumiza.
Naona utusi tusi,
Latanda wingu jeusi,
Kunguru nao tumbusi,
Wote wanatula sisi.
Walinenepa ja faru,
Wakifanya makufuru,
Waliita makaburu,
Nchi waliiguguna.
Walizoboka ja bomba,
Wakijiona miamba,
Tulipolifunga dimba,
Walikitema kilemba.
Walolewa madaraka,
Wakionywa wanang’aka,
Yakiisha kudondoka,
Wawa wapole ja hua.
Baki ni kujilaumu,
Yakuzomea kaumu,
Useme sikufahamu,
Wanakuona wazimu.
Utaja imbiwa wawe,
Kama biwi uungue,
Waja wakupige mawe,
Aibu ikuingie.
Maana hawana hawa,
Hawa ni sawa na chawa,
Nchi yetu inawawa,
Lazima tuwalaani.
Mwalimu tuliibiwa,
Urongo tuliambiwa,
Mwalimu ulipozikwa,
Ulitumiwa kuiba.
Eti moja bilioni,
Litumika msibani,
Kuuliza kulikoni,
Uzikwe kama mkwasi?
Hatukupewa jawabu,
Japo twataka sababu,
Ipo siku watajibu,
Kaumu ikiamua.
Walitula wakanona,
Maungo yalishindana,
Sisi tukikondeana,
Wao wenda kutibiwa.
Walitukoga mchana,
Tena kwa vinywa vipana,
Tukawa ma’na hatuna,
Ndivyo ilitokea.
Mwalimu tuliteseka,
Na bado tunateseka,
Tabu zimetuzunguka,
Kiza kimetufunika.
Rushwa imetuzunguka,
Kwa kila unachotaka,
Rais akasirika,
Atauchimba mkwara.
MATESO.
Mwalimu ulitamka,
Tutakuja kukumbuka,
Kweli tunakukumbuka,
Nani atatufariji?
Baba tunakukumbuka,
Mengi tunayakumbuka,
Jinsi tulivyosumbuka,
Ni vigumu kueleza.
Dawa ni za kununua,
Twapangwa kama vibua,
Dokta alobukua,
Kumuona tano mia!
Wanetu wakaa chini,
Mashule ya mashambani,
Mitaala nisemeni,
Kila kitu ni tuisheni.
Masomo ya uzalendo,
Na elimu kwa vitendo,
Vyote waliweka kando,
Wakaua mdo mdo.
Shule nzuri ni za pesa,
Zinaitwa za kisasa,
Kingereza si siasa,
Ndicho kinakazaniwa.
Kilimo tumekizika,
Uchuuzi tumeshika,
Hakuna anokitaka,
Wote wafanyi biashara.
Bidhaa tunaagiza,
Na sera tunaagiza,
Viwanda tulivyouza,
Maghala tumegeuza.
Sisi sasa vibarua,
Ari imetupungua,
Mwajiri anaamua,
Kuajiri na kufuta.
Kazi ni za mikataba,
Miaka sita au saba,
Usalama sasa haba,
Tunauza jasho letu.
Tunao wawekezaji,
Kila kitu wapangaji,
Nyumbani tu wapangaji,
Wasemacho hatuhoji.
Twaishi kwa wafadhili,
Watu wa kutoka mbali,
Sasa sisi yao mali,
Tumepokea utumwa.
Jeuri imetutoka,
Twaishi kama vibaka,
Heshima imetoweka,
Huna pesa huna kitu.
Bandari tumeachia,
Viwanja vya ndege pia,
Na reli tutaachia,
Hata nchi twaachia.
Zile njia za uchumi,
Nilizozijua mimi,
Hatunazo mikononi,
Kama ulivyofundisha.
Usalama wa taifa,
Sina shaka utakufa,
Twahatarisha taifa,
Kuachia vitu hivi.
Na ya umma mashirika,
Waliyaua vibaka,
Wao wametajirika,
Sasa watoa sadaka.
Hayanae mtetezi,
Twakumbwa na unyafuzi,
Watuua nyemelezi,
Walokuja tuwekeza.
Sera kujitegemea,
Nayo imetokomea,
Mikopo twategemea,
Toka benki la dunia.
Watu tu wategemezi,
Serikali tegemezi,
Tunao wasimamizi,
Wanaitwa viongozi.
Sera nje zinatoka,
Sisi tunachangamka,
Wakubwa wanavyotaka,
Sisi ni kuchakarika.
Makombo twaambulia,
Huku tukishangilia,
Wenye bongo wanalia,
Kuona hii jinai.
Tuna pepo ya mabwege,
Yatubidi tujipange,
Upya mambo tuyaenge,
Tuwaepuke marenge.
Watumwa tumegeuka,
Kuzimu twaporomoka,
Nani atakengeuka,
Kuwatetea wajao?
Nani atashika sime,
Kupambana na ukame,
Kubomoa hizi ngome,
Ngome za utegemezi.
UZAUZA.
Viwanda tulivyojenga,
Majumba tuliyojenga,
Vyote wanavibananga,
Sisi tunashuhudia!
Ukoloni umerudi,
Kwa nguvu mpya zaidi,
Tena kibaya zaidi,
Watumia watu wetu.
Baba tunakukumbuka,
Wale tulioumbuka,
Hotubazo twakumbuka,
Kidogo zatuliwaza.
Lionya juu ya rushwa,
Ya mapesa kumwagiwa,
Lazima kununuliwa,
Na walionunuliwa.
Walishakaa bungeni,
Wakaunda jambo geni,
Rushwa ilivikwa shani,
Ikaitwa takrima.
Rais twamtamka,
Nakumbuka aling’aka,
Wabunge walistuka,
Adabu wakaishika.
Walilikumbuka shuka,
Kumekwishapambazuka,
Tulikwishanunulika,
Wanunuzi weshapaa!
Uongozi sasa
pesa,
Lazima kumwaga pesa,
Wale wasio na pesa,
Wakubali kuburuzwa.
Walihonga wagombea,
Kwa vyakula hata bia,
Mitandio Khanga pia,
Kura wakizinunua.
Walikuja matajiri,
Kwa pesa pia jeuri,
Wakavamia vilili,
Wakapata uongozi.
Waipanga mishahara,
Ya kuondoa hasara,
Hazina wanaparura,
Wasijepata hasara.
Baba kama huna pesa,
Wewe sahau siasa,
Kura siku hizi pesa,
Siyo sera kama Mwanzo.
Uongozi biashara,
Tena iso na hasara,
Toa pesa utang’ara,
Hata uwe barakara.
Mambo sasa yanakhini,
Ukitia akilini,
Nani amuhonga nani,
Mwisho watapata nini?
Pesa vinatoka wapi?
Kinachouzwa ni kipi?
Anayeuza ni yupi?
Na anaye nunua yupi?
Pia zitarudi vipi?
Baada ya muda upi?
Kitachofuata kipi?
Baba kufunga mshipi.
Wananchi wanajua,
Kuwa hapa waungua,
Hawa wanowachagua,
Wataenda kujilipa.
Kujilipa ni rahisi,
Akishapoka nafasi,
Akishapewa ofisi,
Haki ataichuuza.
Atafanya maamuzi,
Hata ya maangamizi,
Akijua wazi wazi,
Umma anauumiza.
Bora aregeshe chake,
Zitimie shida zake,
Alitoa pesa zake,
Anakula haki yake.
Mwalimu nipe sikio,
Nikujuze matokeo,
Umeme ni wa mgao,
Hata maji tutagawa.
Haya ndiyo matunda,
Ya siasa za kuvunda,
Baba mwiba ukipanda,
Jua utavuna mwiba.
Elimu ilishashuka,
Shilingi ilishashuka,
Kila kitu kinashuka,
Shida ndizo zinapanda.
Miiko ya uongozi,
Ilipotiwa kitanzi,
Ikaja bora kiongozi,
Kuliko aliye bora.
Sasa ni bora kupata,
Na ujanja ni kupata,
Hata kwa wizi kipata,
Alopata amepata.
Yapo mambo ya aibu,
Na tena ni ya ajabu,
Ukiipiga hesabu,
Utaambua kichaa.
Hii jamii ya wezi,
Kila kitu ni kwa wizi,
Ninamuomba mwenyezi,
Asinigeuze mwizi.
Jamani wizi ni wizi,
Wa kalamu nao wizi,
Hata wa bunduki wizi,
Hata wa uwekezaji.
Mtu analipwa mia,
Elfu anatumia,
Wapi pengo azibia,
Hii Bongo takwambia!
Bongo hili linatisha,
Tuso nalo tumekwisha,
Kutwa kucha tunahaha,
Ndiyo maisha ya bongo.
Bongo wameiboronga,
Kitanzi wameifunga,
Mambo wameyakoroga,
Zaidi wameboronga.
Eti kupata ujanja!
Hata umma ukipunja,
Haki wameishaikunja,
Utu wetu wanafuja.
Wapi tuipate haki,
Wapi twende kushitaki,
wapi polisi wa haki,
hili ninalirudia.
Haki gani inauzwa,
Haki inayochezewa,
Mwalimu utakumbukwa,
Hadi irejee haki.
Haki sasa ni mapito,
Zama ilikuwa kito,
Wakumbushe ni wazito,
Hawawezi kuelewa.
Wabunge si kama zama,
Wanatumikia vyama,
Wameusaliti umma,
Kulinda nyadhifa zao.
Uliacha upinzani,
Nao uko matatani,
Atayewelewa nani,
Hata uende bungeni?
Inapotolewa hoja,
Utaviona viroja,
Kila atoaye hoja,
Atetea chama chake!
Tofauti siioni,
Ya bunge na serikali,
Ifanyacho serikali,
Ni kuamulia bunge.
Inauzwa mitihani,
Ushindi u mfukoni!
Wafaidi wa mijini,
Shambani aibe nani?
JUZI.
Juzi kisa kilizuka,
Habari ilitufika,
Baba tulisikitika,
Mitihani kuibiwa.
Aliyeiba ni nani?
Tumtie kifungoni,
Ni Mwalimu Kichwa duni,
Anamhonga Mwazani!
Mwazani katiwa mimba,
Nani kamtia mimba?
Yule Mwalimu Maumba,
Rafiki wa baba yake!
Nesi kapiga mgonjwa,
Kisa hakutoa rushwa,
Wapi mgonjwa na rushwa,
Na tena mjamzito!
Hata viranja wa dini,
Nao wamo mchezoni,
Wameshanaswa ugoni,
Walipa sadaka zetu!
Ajira wametangaza,
Ni pale kwenye Baraza,
Bosi pale Mmagwaza,
Aajiri wamagwaza.
Binti chumo amekua,
Anapaswa kuolewa,
Asema mamaye Hawa,
Uniletee kibopa.
Simtaki maskini,
Maskini ana nini?
Nataka mamilioni,
Nijenge nyumba ya mawe.
Awe ni muuza unga,
Jambazi na mla unga,
Pesa itatia nanga,
Kwani unga nala mimi?
Hodi anapoipiga,
Vigelegele tapiga,
Atakuacha pakanga,
Hili hautalienga.
Mwenye mapesa nataka,
Hohe hahe sitataka,
Pesa ndiyo tunataka,
Mama anasisitiza!
Hata kama ni jambazi,
Hiyo iwe yake kazi,
Wewe muuzie penzi,
Akiuawa warudi.
Watu wetu wamechoka,
Wasema wamepigika,
Hawanalo la kushika,
Waibariki jinai.
KIONGOZI.
Nani amshike paka,
Na kengele kumvika,
Shujaa ameondoka,
Panya wanateketea.
Nani avae viatu,
Vilivyokomboa watu,
Ahami taifa letu,
Tumuite kiongozi?
Twamsaka mvaaji,
Aliye navyo vipaji,
Twataka mpiganaji,
Si mwana wawekezaji.
La mgambo nalipiga,
Nani aivae njuga,
Akauvamie uga,
Uliojaa makapi.
Apitishe ufagio,
Kwa asubuhi na jio,
Uwake kama kioo,
Namtaka aje hapa.
Msafi namtafuta,
Popote tamfuata,
Aje tutoe utata,
Tuishi bila matata.
Namtafuta jabali,
Asohongwa na utuli,
Jelebi na pesa mbili,
Nitamkabidhi nchi.
Aje atumbue jipu,
Alimwagie upupu,
Ayafumue makapu,
Yaloficha mali zetu.
Namtafuta jabali,
Asopenda ujahiri,
Jadidi aso tahaari,
Aje akalie kiti.
MAPINDUZI.
Taakini mlo mbali,
Wote wenye taamuli,
Njoo msikie hili,
Nimwambialo Mwalimu.
Mambo yameshanikwaza,
Nateseka na kusunzwa,
Nimejawa na mafunza,
Ya huyu mdudu rushwa.
Tamaa yataradadi,
Imekufa yetu sudi,
Na tusipojitahidi,
Tutazikwa tukiona.
Wameuza mama zao,
Kukidhi tamaa zao,
Tumekuwa wasikwao,
Twamkumbuka Mwalimu.
Wamejiuza na wao,
Kwenye biashara yao,
Ikifika siku yao,
Watajalaumu nani?
Twajua wakila chambo,
Kwa kuendekeza tumbo,
Litapigwa la mgambo,
La kuwatoboa tumbo.
Tutakuwa mashahidi,
Kwa makundi na makundi,
Tutaeleza zaidi,
Bila kufanya fisidi.
Tutaitisha vitabu,
Tueleze taratibu,
Watueleze sababu,
Ile siku ya hesabu.
Mbwa atakuwa Bwana,
Na Bwana awe Mtwana,
Mtwana aitwe Bwana,
Arejeshewe maana.
Lenye mwanzo lina mwisho,
Hili halina uficho,
Hawa nao wana mwisho,
Mwisho usio na kicho.
Leo twachoma vibaka,
Twapapatikia mibaka,
Ile siku ikifika,
Vibaka takuwa sawa.
Twaitaka serikali,
Ilitunze jambo hili,
Ile siku ikijiri,
Sisi tu mashahidi.
Rushwa twanasa dagaa,
Manyangumi yanapaa!
Nani tunamhadaa,
Huyo asiye na mato?
Hatukuzaliwa jana,
Ni mengi tumeyaona,
Fanya jambo la maana,
Inusuru nchi yako.
Twakamata vyangudoa,
Tukiacha wenye ndoa,
Upofu tukiondoa,
Ndoa hii ya Mashaka.
Makahaba kiuchumi,
Mbona ni wengi sisemi?
Nani kaua uchumi,
Si kahaba kiuchumi?
Lazima tuwaandame,
Hata nchi waihame,
Vita hii isikome,
Hadi tutapowanasa.
Lazima tuchunguzane,
Mali tutangaziane,
Na tena tukaguane,
Ukweli tuambizane.
KILIO.
Kwa Mwalimu narejea,
Ingawa umepotea,
Bado tunakulilia,
Ili lau tusikike.
Wakati wa enzi zako,
Ulihami nchi yako,
Tulijua mali zako,
Hawa zao hatujui.
Tulisoma na wanake,
Wa kiume na wa kike,
Hakuwaficha wanake,
Kwenda kusomea nje.
Wanenu hatuwaoni!
Wanasoma shule gani?
Waibuka ofisini!
Walipwa mamilioni!
Tunataka umakini,
Enyi mlo ofisini,
Muishinde mitihani,
Mbaki kuwa kioo.
Muipige vita rushwa,
Na huku kufukarishwa,
Onyesha vyema vipawa,
Isogee nchi yetu.
Twataka maisha bora,
Siyo huu uchokora,
Hata viongozi bora,
Na siyo wale wakora.
Tunautaka uwazi,
Wa haki si ubaguzi,
Kila jambo liwe wazi,
Ofisi mali ya insi.
Mikataba ya madini,
Ile mnayosaini,
Tuijue ina nini,
Faida au hasara.
Mlokwisha isaini,
Isongia akilini,
Twataka ipigwe peni,
Zuia kuuza nchi.
Wale waloisaini,
Kwa akili mifukoni,
Tuwatie kifungoni,
Kwa wengine iwe somo.
Wapewe adhabu kali,
Wakishanyang'anywa mali,
Wasutwe kila mahali,
Hapa tutangaze vita.
Tuiambie dunia,
Ya kuwa tumepania,
Kusafisha Tanzania,
Iondokane na rushwa.
Tuwasage kama kupe,
Kwa bakora tuwachape,
Hata vifungo tuwape,
Waozee gerezani.
Lazima tuwaandame,
Hata nchi waihame,
Vita hii isikome,
Hadi tutapowanasa.
Lazima tuchunguzane,
Mali tutangaziane,
Baadaye tukaguane,
Wadokozi tuwajue.
Rais mali tangaza,
Waziri mali tangaza,
Hakuna wa kumsaza,
Mambo yawe hadharani.
Hata za mkeo taja,
Hata za mwanao taja,
Wote tuwe taja taja,
Hapa tutapata tija.
Lazima kuswafi nia,
Ni lazima kupania,
Bila ya kupendelea,
Tutashinda mapambano.
Tuondoe kujuana,
Udugu na kulindana,
Wala kuaminiana,
Bila ya kutenda haki.
Tuna sifa moja kuu,
Watu waso na makuu,
Hii ni kwa juu juu,
Matabaka yanazuka.
Tulikuwa wajamaa,
Watu wasio tamaa,
Sasa adui tamaa,
Atesa kama ukimwi.
Mwalimu twakukumbuka,
Umoja alisimika,
Nchi ilineemeka,
Udugu ulijengeka.
Wameua ujamaa,
Wameleta unyamaa,
Sasa tunalia njaa,
Kunyonyana kumejaa.
No comments:
Post a Comment