Leo kijiwe kina ajenda moja kuu,
kumkaripia mhuni mmoja aliyetukana wenzake kuwa ni waroho wa juisi.
Dk Msomi Mkatatamaa leo amrauka na
makabrasha yake. Kanji hayupo. Amekwenda India kupeleka fweza na kuangalia kama
bi mkubwa wake ameishaongeza faida ya mtoto mwingine. Maana hawa jamaa kwa
faida hata mtoto wa kubambikiziwa ni faida. Utamsikia akisema, “Mimi fika
Bombei na kukuta bibi ongeza toto mbili.”
Msomi analianzisha? “Jamani mmemsikia
mlevi wa madaraka Steve Waasiraa na nyodo zake za kizamani? Ama kweli nyani
haoni nonihino lake!”
“Mbona yeye alipokimbilia Chakudema
hakuambiwa kuwa alikuwa anafuata kunywa juisi au alipojirejesha Nambari Wani
kwa aibu hakuna aliyesema alikuwa akihangaishwa na njaa? Huyu chinga Chikwawe
ni wa kuonea huruma. Hana adabu wala maana kabisa. Hana jipya la kujadili zaidi
ya kumpuuzia kama bosi wake alivyowapuuzia.” Anazoza Mijjinga.
Kapende hajimamasi, anamwaga pwenti, “Hakuna
upuuzi uliniudhi kama kusema eti wapingaji wanakwenda ikulu kunywa juisi. Kwani
hata wakinywa juisi huko ikulu hiyo juisi si ni matokeo ya kodi zao kama
wanakaya? Mbona hata hapa kijiweni juisi zimejaa kama juisi ni dili? Mbona hata inzi
wanakunywa juisi. Hebu angalia yale mainzi yalivyozunguka juisi pale.”
Anaonyoosha kidole kuelekea kwa muuza juisi jirani na kijiwe. Anaendelea, “Hivi
wangekwenda kule kunywa bia huyu jamaa si angejinyotoa roho?”
Mchunguliaji ambaye siku nyingi
haudhurii kijiweni anaamua kutafuna mic, “Huenda Waasiraa aliaanisha mainzi
yaliyomzunguka rais yakifaidi juisi kule ikulu na mawizarani. Who knows?”
Mzee Maneno anang’aka, “Kumbe ikulu siku
hizi inaweza kudhalilishwa hivi tena na wale inaowafuga? Tunakwenda wapi?”
Mbwa Mwitu ambaye alikuwa kimya muda
wote tofauti na kawaida yake aliamua kukwanyua mic, “Nyie hamumjui huyu mura. Aliwahi
kuwarushia kimondo wapingaji kuwa ni malaya akakutikana kuwa kumbe yeye ndiye
mwalimu wao. Jamaa ana ugonjwa wa kuongea bila kufikiri ukiachia mbali kulala
lala mjengoni au mmemsahau yeye na Joni Kombaaa?”
Sofi hajivungi. Anaonyesha usongo wake,
“Pamoja kuwa mimi ni mwanachama na mkereketwa nambari wani, kauli za hawa
wenzangu zimenikera sana. Hata hivyo, msijali. Huyu Waaasiraa operesheni
kimbunga itamkumbwa kwa vile ni mkimbizi haramu wa kisiasa. Sijui hata kama
Chakudema watampokea. Maana hana sera tena zaidi ya mitusi ya nguoni.”
“Mwagie Sofi. Mmwagie kahawa, kumbe hata
wenzao wameishawastukia siyo? Mshaurini huyo anayewafuga awapige chini tuwaone
wakila majani kama ng’ombe wahuni hawa.” Anapayuka Mijjinga ambaye huwa haivi
na bi Sofia.
Msomi, “Hebu niwakumbushe maneno ya
nyodo na ukosefu wa busara ya Chikwawe.” Anafungua mkoba wake na kutoa gazeti
liloandika habari za Chikwawe kumshangaa bosi wake na kusoma, “Nitamshangaa
sana Rais Kikwete kama atashindwa kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za
wapinzani.”
Anapekua mkoba na kutoa gazeti jingine
na kusoma maneno ya kifedhuli ya Steve Waasiraa. Anasoma, “Hawa tumewalea siku
nyingi na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa
Ikulu.” Anamalizia, “Kunywa juisi.”
Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi
anaingilia kati, “Kwani huyu waaasia ikulu ni mali ya mama yake. Tinapaswa
kwenda huko kwenye ofisi timtoe kwanza haafu timuejeshe kwao Chakudema. Kwani
hatumjui hata kama anawaponda Chakudema wenzake? Bosi wao awapige chini wakamshangae vizuri.
Hata hivyo, kwa alivyowapuuzia, wangekuwa na akili wangeachia ngazi wenyewe. Maana
hata naye anawashangaa kwa wasivyotumia akili bali masaburi.”
Mpemba naye hangoji mwenzie amalize,
“Huyu yakhe asumbuliwa na usingizi na madawa anayokula ati. Wategemea jitu
lilalavyo hovyo hovyo liwe na kumbukumbu na hekima? Wallahi hawa si wazalendo
hata kidogo.”
Mipawa, “Yeye mwenyewe Waaasiraa
anafugwaga kiasi cha kujisahau na kuwaambia wenzake eti wanawafuga. Haya ni
matusi ya nguoni yasiyopaswa kutoka kwenye kinywa cha mtu anayeitwa waziri. Kwanini
tusimtokee na kumtolea uvivu kama anadhani hiyo ofisi ni yamama yake?”
Kapende anachomeka pwenti nyingine, “Nilisikia
eti naye anajiandaa kugombea urais. Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi. Yaani
urais umekuwa rahisi kiasi hiki hadi kugombewa na watu ambao midomo yao ina
mgogoro na vinywa vyao?”
Msomi akatua mic, “Tusipokuwa makini
such sick, skinny and bankrupt dudes are going to wreck our ship. Loh! Samahani
jamani. Nimechukia hadi naongea kikameruni,” Anajitetea na kuendelea. “Hata
hivyo, siwalaumu wao bali yule aliyewafunga wasijue wote wanafungwa kwa kodi
zetu. Kuna haja ya kuwakumbusha hawa
vimbelembele kuwa hata kama bosi wao aliwatuma wanapaswa kufahamu mahesabu ya
mbayuwayu. Mara hii wamesahau kilichompata Nipe Mapape Ninaye aliyeambiwa
awatukane mafisadi asijue lao moja. Si jamaa alimalizana nao na kumuacha Mapepe
na aibu zake.”
“Kumbe hata wakameruni wanajua hawa
jamaa walivyo na kuwaita madude kama sisi!” Anashangaa mzee Kidevu.
Kapende anakoleza, “Waache wajisahau
wasijue kiama chao kinakaribia. Jamaa alishawaambia wajiandae kisaikolojia kila
mtu kufa kivyake lakini inaonekana hawajaelewa somo. Shame on them!”
“Msimlaumu Waasiraa. Tangu ajitoe
chamani na kujiejesha kama mtalaka anapaswa apige kelele sana ili wenzake
wamuamini. Huyu hana tofauti na yale mabuda kama Chibuda na Lyatongolwa Mlemavu
ambao huchonga hadi mapofu yakawatoka ndiposa watupiwe mabaki wapwakie. Nawajua
sana watu hawa mangungaembe wa kisiasa na wachumia tumbo.” Mgosi Machungi
anakandia kwa sana.
Kusikia
nungaembe Sofia anaamua kutia guu, “Sasa hapa unungaembe unatoka wapi mgosi?”
“Soe
dada Sofi. Hapa tinamaanisha manungaembe wa kisiasa si wengine. Ngoja tibadili.
Hawa ni mafisi na mafisadi wa kimawazo au vipi? Tabasamu sasa dada yangu.”
Anajitetea Mgosi huku akimtania bi Sofi ambaye naye anatabasamu kuonyesha kuwa
amemuelewa.
Kumaliza
mgogoro Mgosi anasema, “Hebu kijana titilie kahawa mimi na Sofia tinywe na
tifurahi,”
Kijiwe
kikiwa kinanoga si likatokea shangingi la Waasiraa tukaamua kulirushia mimawe
huku yeye akionekana wazi kustuka na kutoa mimacho kana panya aliyenaswa
mtegoni. Kama si ndata kuingilia kati
huenda tunge nyotoa mtu roho na kuacha wanaofuga upuuzi wakishangaa kama
waasiraaa anavyowashangaa asijishangae.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 16, 2013.
No comments:
Post a Comment