The Chant of Savant

Saturday 26 October 2013

Wauza bwimbwi, JK ataka tuwataje

Rafiki yangu mzito JK mwenye rungu la dola, katoa mpya kiasi cha kumfanya mlevi aamue kuingia full masinonda to clear the air. Mzito amesema eti tuwataje wauza bwimbwi kwa vile kila mmoja anawajua akiwamo yeye.
Kama yeye mwenye mamlaka kuanzia gereza, pingu na majeshi, kwa zaidi ya miaka saba ameshindwa kuwataja na kuwasulubu walevi wasio na madaraka wataweza au ni yale yale ya kugeuzana majuha?
Anyways, njia ya muongo ni fupi. Kama wao wanawagwaya, tuwataje watunyotoe roho kama Amini Chimfupa wao waje kumwaga machozi ya mamba kwenye maziko yetu siyo? Aminia amepotea. Nani anajali?
Madigara wa bwimbwi si wanaendelea kutukoga na mali zao haramu? Who cares if mlevi returns the number to his maker early? Navyopenda kanywaji kangu siko tayari kuguguna fupa lililomshinda fisi. Soma kimya bi mkubwa asikusikie akanivisha gagulo kwa kudai: Napenda kanywaji kuliko yeye.
Naonya. Wauza bwimbwi wasijisifu. Siku mibangi ikinibangua nitawataja potelea mbali. Kwani kuna ambaye ataishi milele? Nawadeku pale Kinondoni, Magomeni, Sinza kwenye kona ya wazito hata wale wa Masaki kwenye mahekalu yenye zulia za manene na kila kitu rangi moja.
Nyie kaeni mkao wa kuliwa hata kama mnawala wenzenu. Nawajua sana. Hata wanaotumia madhehebu ya dini kuficha biashara ya bwimbwi nawadeku huku wakiwandanganya wasiojua eti pesa inatoka kwa Mungu au usanii na imani nyingine ambazo zitazitaja kwa sababu za kiusalama. Maana hamkawii kulipuka na kunyotoana roho wakati ni ukweli.
Waliojificha nyuma ya siasa na biashara nyingine za uongo na ukweli wakati ni wauza bwimbwi nawadeku na siku yao ikifika mie nitataja. Kama mbaya, mbaya. I was born once and I’ll kick the bucket just once. So too, they’ll.
Nanukuu hekima za munene JK, aliyekaririwa na vyombo vya umbea akisema, “Baadhi yenu wanaojihusisha na biashara hiyo ya bwibwi mnawafahamu, hivyo watajeni ili siri-kali iwachukulie hatua za kisheria.” Munene alitoa rai hiyo wakati akihutubia katika sherehe za kelele cha mbio kibatari kikubwa cha udhuru sambamba na maadhimisho ya miaka 14 ya kifo cha Mchonga, yaliyofanyika unyalukoloni ambako wajivuni wengi walimsanifu wakijidai wanamkumbuka.
Tangu lini panya wakamkumbuka paka ambaye kuondoka kwake ni uhuru wao kufanya monkey business? Baada ya munene JK kuminya na kuona ni vyema, ameamua kuchonga akisema tutaje wenyewe kwa vile yeye hatataja. Natamani angesema tutaje halafu tuhukumu. Maana yeye ameamua kuminya na kutuachia wenyewe tumalize kadhia kama tunavyowafanyia vibaka huku tukiabudia mibaka tena inayobaka uchumi hadi Uswizi.
Munene, ningeshauri kwa ulevi wangu uongoze kwa mfano. Mfano, ulitwambia mwaka 2006 yaani miaka saba iliyopita kuwa una majina ya wadudu hawa. Ajabu hujawahi kukubali kuyaweka wazi wala kuwachukulia hatua. Mlevi mmoja anayefanya kazi Uhasama wa Taifa aliniambia kuwa hii nayo ni top secret for national security of insecurity. What a humungous lie! Kama tutaamua kufanya kama wewe, inabidi walevi tupewe miaka saba ndipo tuwaambie wenzetu wataje, tutaomba tuongezewe mingine saba ndipo tutaje.
Munene akimuongelea mzee Mchonga alisema, “Maisha yake yalikuwa zawadi kwetu; si kwa walevi pekee, bali kwa Wamakonde na dunia nzima.
Mwalimu alijitahidi kutunza roho ya mcha Mungu huku kazi zake akizifanya kwa hofu ya Mungu.” Kumbe mlevi akidedi anageuka lulu? Laiti Mwalimu Mchonga angekuwa zawadi tungeitunza na kuienzi badala ya kuacha hata wanyama mwitu wainyee kama ilivyo. Ni zawadi gani isiyothaminika? Siku mlevi nikirejesha namba msishangae kusikia wajivuni na waongo wakimmwagia sifa wakisema alikuwa askofu au bonge la shehe wakati si kweli. Are we serious really?
Munene aliongeza, “Tuna deni kubwa kwa hayati Mchonga na deni hilo lazima lilipwe. Deni hilo ni kuishi kwa pamoja kwa umoja na kuheshimiana pia.” Mlevi anasema wazi. Hizi ni kamba. Kwa sasa walevi na wakwasi hawaishi pamoja wala kwa umoja bali ujambazi na utengano mkubwa.
Wakwasi wanawaogopa walevi na walevi wanawachukia wakwasi. Wakwasi wanakula keki ya kaya wakati walevi wanakula vumbi. Wakwasi wanakula nchi wakati walevi wanaliwa na wakwasi pamoja kaya yao. Kama kuna umoja, upendo na hata amani basi ni vya uongo na kutungwa.
Kama kweli tungekuwa na deni kwa Mwalimu tusingeuza madini, wanyama, ardhi na viwanda alivyolinda kwa nguvu zake zote. Wala tusingefuga mafisi na mafwisadi. Huwezi kulipa deni kwa kuiba na kufuja zaidi. Kufanya hivyo si kulipa bali wendawazimu na jinai vya aina yake. Nadhani wanaofanya haya majanga yote wana deni kubwa kwa Mchonga. Huwezi kuiba mafuta kwenye kibatari bado ukashabikia mwanga zaidi ya kiza.
Hamuwezi kugawana nyumba alizotaifisha ili kusaidia walevi mkakosa kuwa na deni kwa Mchonga. Watu wa namna hii wana deni kubwa kwake na malipo yake lazima walaaniwe wapayuke hovyo hovyo bila kujali kuwa wanayosema yanapingana wazi wazi na matendo yao machafu. Huwezi ukawa bingwa wa kutetea madili kwa kuua maadili ukakosa kuwa na deni na Mchonga. Dawa ya kutokuwa na deni na Mchonga ni kupiga kanywaji na kuwaambia na kuwafanyia walevi ukweli.
Kama tungekuwa na deni kwa Mwalimu tusingesumbuliwa na wauza bwimbwi kama ilivyo mbapo kila mtu anawaogopa kama Ukimwi au waya wa umeme hai. Mimi sina deni na Mwalimu bali muuza kanywaji. Mwalimu hakuruhusu vigogo wainunue kaya na kuiweka mifukoni mwao kiasi cha kushindwa nani ambaye hayumo mifukoni mwao. Hivi tuna watu wana migunia mikubwa hadi wanawaweka wanene. Waulize akina Kagoda na Deep Finance wameishia wapi?
Turejee kwenye utajaji wa wauza bwimbwi. Hivi nani wa kumuamini kumpelekea majina wakati wenye nayo na madaraka wameyakalia? Nani huyu juha na mlevi apeleke kesi ya nyani kwa ngedere wakati wote lao moja? Nani amshitaki kambale kwa kambale kuhusiana na sharubu?
Ni ajabu kama ng’ombe ataruhusiwa kuwa hakimu kwenye kesi ya ngamia kuhusiana na uharamu wa nundu. Salama kwa marafiki zangu akina Abudala Matimbwa, Seifuu, Saiiid Litela na wengine pale Kaliyakoo. Nakumbuka mlivyonisotesha nilipopanga kwenye mbavu zenu za mbwa kabla sijapata pa kuchomokea. Nanyi mnamuenzi Mchonga siyo?
Chanzo: Nipashe Jumamosi Okt., 26, 2013.

No comments: