Hakuna ubishi. Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mojawapo ya vyama vikongwe duniani. Ni chama kilichochoka kuisha na kuishiwa kiasi cha kupaswa kustaafisha tokana na utendaji wake wa hovyo na wa kizamani. Kwa mtu anayefuatilia utendaji wa CCM, hasa katika awamu mbili zilizopita, anashangaa ni kwanini bado kimo madarakani. Japo wengi wanajua kuwa CCM imekuwa ikichakachua uchaguzi jambo ambalo kila mtanzania anafahamu, inashangaza kwa watanzania kuendelea kuivumilia ilhali inazidi kuwazimisha. Hivyo, si vibaya wala uchochezi kuwataka watanzania kukisaidi chama hiki kwa kukiwajibisha ili kipumzike na kujipanga upya. Kwanini siku zote chama kile kile na mambo yale yale, tena ya hovyo, wakati kuna vyama vipya vyenye mawazo mapya vinavyoweza kufanya mambo kisasa na inavyotakiwa? Kwanini kung’ang’ania chama ambacho, licha ya kuboronga, kimeishajichoka na kujichokea?
Utendaji wa CCM umekuwa ni wa kiwango cha chini mno kiasi cha taifa letu kuzidi kutokomea kwenye umaskini wa kutengenezwa na watu waliochoka na kuishiwa huku wao wakijitajirisha bila kujali umma wa watanzania. Nani hajui kuwa CCM imeishiwa na kuchoka? Kama yupo basi aangalia utendaji wa vyama vingine tena vilivyozaliwa jana katika jirani zisizo na raslimali nyingi kama Tanzania. Ni jambo la aibu na hatari kwa nchi yenye raslimali karibu kuliko zote katika Afrika Mashariki kuendelea kuachwa nyuma na viinchi vidogo kama Kenya na Rwanda na hata Uganda katika nyanja za maendeleo. Kila mwaka utegemezi katika bajeti unazidi kuongezeka huku bajeti yetu ikitegemea sigara juisi pombe na wafadhili kana kwamba hatuna raslimali. Je raslimali zetu zinafanya kazi gani na ni za kazi gani kama kila mwaka tunazidi kuwa tegemezi? Je tatizo hapa ni vyanzo vya mapato au uongozi imara na adilifu? Huwezi ukaendesha nchi kwa kutegemea ulanguzi wa juisi sigara na pombe ukajifisifu kuwa umefanya kitu. Hapa ndipo CCM inadhihirisha wazi ilivyoishiwa, kuisha na kupaswa kuondolewa madarakani kabla ya kuizamisha nje kabisa.
Ni bahati mbaya kuwa watanzania wamekuwa wakileweshwa na kutishwa kuwa CCM ikiondolewa kutazuka vita. Uongo mtupu. Mbona KANU pale Kenya, UNIP Zambia, MCP Malawi na PDRE Ethiopia ziliondolewa na nchi zinasonga mbele? Huu ni ushahidi kuwa kuondolewa kwa CCM hakutasababisha lolote zaidi ya kutoa fursa kwa nchi kusonga mbele. Tunavyoongea Ethiopia ni mojawapo ya nchi zinazosonga mbele kwa kasi kiuchumi barani Afrika ukiachia mbali Kenya kukwa mbele yetu.
Utendaji wa CCM umekuwa wa hovyo na wa mashaka tangia awamu ya tatu hata ya pili ukiachia kurithi misingi imara ya uchumi toka awamu ya kwanza. Mfano, CCM imeua uchumi, elimu, uzalendo, uwajibikaji, uchapakazi na dhana nzima ya utaifa. Watu tena walioaminiwa dhamana ya umma wanaibia taifa kana kwamba halina mwenyewe! Iulize CCM. Ni mafisadi wangapi papa tena wanaojulikana wameishafikishwa mahakamani? Si wamo chamani tena wakiongoza kamati nyeti pamoja na kubainika wazi wazi kuwa ni mafisadi? Angalia waliotenda makosa ya jinai kama vile kughushi vyeti vya kitaaluma wanavyozidi kupandishwa vyeo huku wakivurunda kila waendapo. Kwani hawajulikani hata kwa majina? Nani anawagusa iwapo sera ya CCM ni kulindana na kulipana fadhili hata kama wanaofanyiwa au kufanya hivyo ni wachafu?
Nani anabisha kuwa ufisadi na wizi wa fedha za umma vimeongezeka chini ya awamu mbili tajwa. Mfano mzuri ni taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na mbunge wa Ubungo John Mnyika aliyekaririwa akisema, “Mwaka 1980, Dola 570. 6 fedha hizo zilitoroshwa wakati hayati baba wa Taifa mwalimu Jullius Nyerere akiwa madarakani na dola 1,566 milioni zikatoroshwa 1985 wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi.Jambo la kusikitisha zaidi mwaka 2002 zilitoroshwa jumla ya Dola za Marekani 1, 1010 milioni katika kipindi ambacho Rais Benjamin Mkapa yuko madarakani.” Huu ni ushahidi tosha kuwa CCM imekuwa ikisimamia utoroshaji wa matrilioni haya ya shilingi kwa vile inanufaika nao. Hapa ndipo swali kuu linapojitokeza: Kwani kazi ya serikali ni nini kama inashindwa kuzuia wizi huu? Je hapa CCM haijaishiwa kiasi cha kuonekana kama mshirika wa wezi tena wakubwa wa mali ya watanzania?
Ukitaka kujua kuwa CCM imeishiwa na ni mshirika mzuri wa wizi wa matrilioni ya fedha za watanzania, iulize serikali yake. Harakati za kurejesha mabilioni yaliyofichwa Uswizi imefikia wapi zaidi ya kufutikwa chini ya busati huku mbalioni mengine yakizidi kuchotwa mchana kutwa na wahusika kuendelea na mambo mengine kana kwamba kitendo hiki ni haki na halali.
CCM imeonyesha wazi kuchoka na kuishiwa kutokana na kutokuwa na sera maalumu ya kuongozea taifa. Ukiwauliza leo nini sera ya Tanzania utaambiwa ujamaa na kujitegemea wakati ulizikwa miaka ya 90 chini ya azimio la kijambazi la Zanzibar liliruhusu wizi na ujambazi tunaoshuhudia ambapo wale viongozi waliozoea kumzunguka mwanzilishi wa taifa letu hayati Mwl Julius Nyerere wakijiita na kujionyesha kama wajamaa ndiyo wezi na mabepari wakubwa. Nani anabishia hili? Kama yupo awaulize makada wa CCM kama vile Andrew Chenge, Rostam Aziz na wengine wengi ambao utajiri wao unajulikana ulivyopatikana kwa njia ya kuhujumu na kuibia taifa. Imefikia mahali hata mwenyekiti wa CCM anapata kigugumizi kutaja mali zake kutokana na kuhofia ukubwa wake na jinsi alivyozipata tena kwa muda mfupi. Nani anabisha tumuonyeshe ushahidi zaidi?
Ukiachia utendaji mbovu, CCM ilifilisika muda mrefu pale ilipokosa uongozi makini na wenye kufikiri. Nitajie mmojawapo wa viongozi wa sasa anayeweza kusimama hadharani akatetea sera na miongozo ya chama. Hayupo. Waliopo ni wasasi wa ngawira ambao wako tayari kuhongwa vitu vidogo kama suti na upuuzi mwingine kumuuza mtanzania. Anayebishia hili arejee mikataba ya kijambazi ya uwekezaji ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha uhujumu wa taifa, utoroshaji fedha nje na ulanguzi wa huduma kama ilivyofichuliwa hivi karibuni juu ya kampuni la IPTL.
Nafasi haitoshi. Tunatoa dokezo kuwa CCM imeishiwa. Haipaswi kuendelea kuwa madaraka wakati imekuwa iktenda madudu ya kila aina.
Chanzo: Dira Julai, 2014.
4 comments:
CCM wanajua janja weshamtuma kijana Makamba atangaze kugombea urais hii yote kuchokonowa UKAWA
Anon, nadhani walengwa wamesikia na hawataingia mkenge hata kidogo.
C,C,M kamwe haiwezi kutoa Rais mzalendo
Anon usemayo ni kweli ila ni jukumu la wapiga kura wa Tanzania kuhakikisha hawafanyi makosa tena kuiamini CCM yaani Chama Cha Manyang'au kama si Mafia.
Post a Comment