BAADA ya kunyaka nyuzi kuwa katika libajeti la hovyo linalojadiliwa baada ya kuletwa na Saada Mkuyati kuwa ofisi ya rahisi imepangiwa njuluku sawa na za kilimo, Kijiwe kimeamua kutoa shinikizo pendekezo na uchanganuzi adhimu ili lau wahusika wajue kuwa nacho kipo na kina-monitor the whole situation.
Analianzisha Mpemba, “Yakhe mmesikia haya mauzauza ya kilimo kwanza wakati siyo? Kwanini hawasemi ukweli kuwa ni matanuzi kwanza na kilimo kitajijuu?”
Msomi Mkata tamaa hangoji. Anakatua mic, “Njaa Kaya ataingia kwenye vitabu vya historia kama mtu anayeweza kusema lolote na asifanye lolote. Alipoingia kwenye ulaji kwa kauli mbiu yake ya maisha bora kwa wote wengi walizugika wakamwamini wasijue itakuwa kinyume. Baada ya kugundua kuwa maisha bora kwa wote yaligeuka maisha balaa kwa wengi, alikuja na gea ya kilimo kwanza kuonyesha kuwa ana mpango wa kuinua maisha ya wachovu wadanganyika walio wengi ambao wengi ni wakulima. Alianzisha kinachoitwa kilimo kwanza.”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea, “Kilimo sisi watoto wa mjini kinatuhusu nini iwapo tunakula kwa njuluku zetu?”
Msomi anampuuzia Mbwamwitu na kuendelea, “Taarifa kuwa safari za matanuzi za rahisi nje zimetengewa bilioni 50 huku kilimo kikitengewa milioni 51 ni matusi ya nguoni kwa wakulima. Haiwezekani kilimo ambacho tunaambiwa ni uti wa mgongo wa kaya kitegengewe njuluku sawa na za mtu mmoja na genge lake kwenda kutanua kwa kisingizio cha kubomu mambo yawe sawa. Hapa lazima kuna tatizo upstairs vinginevyo, huu ni ulafi uliokithiri.”
Mijjinga anaamua kuingia full masnonda, “Unashangaa hivi vijisenti wakati tunaambiwa kuwa kwenye libajeti hili la shilingi trilioni 19.8 shilingi trilioni 3.7 zimetengwa kwa ajili ya posho za makalio, chai, vitafunwa na mahanjumati mengine? Hii ndiyo Bongolala ya Danganyika ambapo genge la wezi huwashika mateka wachovu wote huku likiwalewesha kuwa linafanya hivyo kuwakomboa wakati ni maangamizi ya wazi wazi. Shame on them all!”
Kapende anachomekea huku akinyosha vizuri tai yake, “Msomi hujaweka takwimu zako sawa. Kwa taarifa yako ni kwamba zilipuguzwa na kuwa 39 ambazo nazo hazimtoshi hasa ikizingatiwa kuwa kwenye bajeti iliyopita alitengewa bilioni 15 akatumia zaidi ya hizo ndani ya miezi miwilli. Wakati tukishangaa hii hebu fikiri hii kali ya wizara ya Ilm na Ujinga ambayo imeomba jumla ya shilingi bilioni 790.325 ambapo njuluku ya safari ni zaidi ya bilioni 50 na bilioni 46 madawa. Huu ni ushahidi kuwa matanuzi ya waishiwa ni bora kuliko kilimo. Hivyo nakubalina na wanaosema: Matanuzi kwanza Kilimo Mwisho.”
Mipawa anampoka Mijjinga mic na kupayuka, “Yote tisa. Kumi ni pale tunapoambiwa kuwa libajeti lenyewe linategemea wafadhili. Kila mwaka mnategemea wafadhili hapa kweli mtaepuka kuendelea kuliwa hata kama mnawala wachovu? Mimi sioni libajeti hapa zaidi ya visingizio vya kuongezeana ulaji ili walafi na wezi wazidi kunona wakati umma ukiangamia. May you perish?”
Sofia Lion Kanungaembe hangoji, “Ulitaka rais asiende kuomba? Asipofanya hivyo kaya itaendeshwaje?”
Mijjinga hangoji mwingine ajibu, “Sofi umeingiliwa na nini dada yangu? Kaya haiwezi kuendeshwa kwa fedha ya bakuli ikiwa salama. Sema hii pesa ni ya kumwendesha huyo anayebomu lakini si wachovu. Kusema itatuendesha ni matusi ya nguoni vinginevyo kama inakuendesha wewe.”
Mgosi Machungi aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kula mic, “Tisishangae Vasco da Gama kutumia njuuku nyingi hivi. Ana shida gani iwapo anatawaa kondoo anaoweza kuchinja atakavyo? Tipinge. Hii biioni 39 itatumika ndani ya miezi minne au mitano na nyingine itachukuiwa benki na kumpa amaizie ngwe yake ya matanuzi.”
Mzee Maneno anachomekea, “Hata hivyo ana hasara gani iwapo mwakani anakitoa na kutuachia mabalaa huku akitengewa mabilioni mengine baada ya hapo? Danganyika bwana.”
Kanji nakwanyua mic, “Mimi hapana ona baya ya kuu tembea sana. Kama napata juluku na mambo iko kwenda na kaya iko na peace, why shouting. Kwani juluku yenu au ya umma?”
“Looo! Kanji nawe umeingiliwa na nini. Kwani hujui hiyo njuluku yatokana na kodi zetu? Hata hivo wewe masahibu yetu yakuhusu nini wakati unao uraia wa kaya nyingi tuniozuiliwa sie? Wallahi huu wizi hata kama watendwa na wakubwa ati.”
Bwege aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kuchomekea, “Nadhani hamjui tabia ya hawa mabwege. Wanachofanya sasa ni kupitisha libajeti la lala salama bila kujali kama sisi tunaumia au la. Wako pale kuchuma na kujaza matumbo yao. Hivyo, kujitengea njuluku nyingi ya kuzurura, kula na kutanua wao wanaona ni haki yao hata kama siyo. Kwao ni matanuzi kwanza kilimo kitajiju.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si tukapewa ofa ya msosi kwa mamantilie! Nasi kama wao tulikwenda kujihudumia mazao ya kilimo. Kwetu ilikuwa ni mlo kwanza kilimo baadaye.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 2, 2014.
No comments:
Post a Comment