How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Saturday, 5 July 2014
Mlevi:Kumradhi kuvunjika pambano Mjengoni
Siku hizi mjengoni kumegeuka Railway Gerezani ambako ndondi hupigwa.Tofauti ni kwamba Railway Gerezani huwezi kuingia bila kulipa kiingilio na wala hulipwi posho ya kukaa na kushangilia ndondi kama ilivyo mjengoni ambapo mambo ni kinyume. Tofauti nyingine ni kwamba mjengoni kuna posho za mipasho na makandokando mengine.
Baada ya waishiwa kuishiwa kiasi cha kukosa cha kuonyesha, wamekuja na utundu mpya wa kuonyesha masumbwi kufidia pale walipochemsha. Zamani tulizoea kusikia wahishimiwa wabunge wakishinda na kuchachafyana kwa hoja.
Siku hizi usiposhuhudia masumbwi basi utasikia kashfa zinazohusu ubunge zikiwahusu wale uliodhania ni wabunge.
Mijadala moto moto radioni haipo tena.
Badala yake kuna mipasho tena kwenye televisheni jambo ambalo baadaye tutastukia madhara yake baada ya kuwa watoto wetu wameishaharibika kutokana na kuangalia vipindi kama hivi.
Siku hizi imebaki kuwa historia hasa pale chama twawala kilipojaza wahuni wake mjengoni kiasi cha kuondoa maana nzima ya mjengo tuliyouzoea zama zile.
Tulizoea kusikia hoja nzito zikitikisa mjengo na kaya.Siku hizi tunasikia tambo, mipasho na mitusi tena ya nguoni na isiyofaa kuandikwa hapa.
Hebu fikiria hiyo mitusi ni michafu kiasi gani kiasi cha kumfanya hata mlevi na mvuta bangi kuigwaya.Je! inapomwagwa na muishiwa anayeitwa mhishimiwa unajisikiaje wewe unayelipa kodi ili alipwe kuanzia mshahara, posho ya makalio, mahanjumati, hata posho ya mipasho na kuuchapa usingizi mjengoni?
Baada ya kugundua kuwa mipasho na mitusi haitoshi, waishiwa wanaoitwa wahishimiwa kimakosa kutokana na kukosa heshima na maana wameamua kuanzisha ligi ya ndodi isiyo rasmi.
Hivyo, tunapoandika ni kwamba wengi wa waliotegemea kuwa wale wanaowawakilisha wangefanya hivyo, wajiandae kuona watu waliojaa P.o.P au piopio kama Uswazi waitavyo lile dongo la kumuungia mwanadamu mifupa.
Kama tulivyowatanganzia walevi, baada ya mlevi kuanzisha Waishiwa Boxing Club (WBC), ameamua kufanya kweli.Juzi juzi aliandaa pambano baina ya David Kafulia na Goliati Freddie Were-ma ambaye ni wakili mkuu wa sirikali aneyesifika kwa kutetea uoza.
Pambano hili lilikuwa lifanyike Mjengoni kwenye jiji la Las Dom.Hata hivyo, kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wetu, pambano husika ilibidi lisimamishwe baada ya mmojawapo wa maboxer kupata ugonjwa wa kupandwa hasira kiasi cha kupandisha mwenembago na vinyamkera.
Mpambano ulitibuka baada ya mabondia kukamatana uchawi ambapo Daudi alimwambia Goliati kuwa alikuwa ameiba mshiko wa Escrow ambayo maana yake ni pesa ya malipo ya kutumia nishati ya wawili hawa kuzitwanga.
Kimsingi, pesa ya Escrow hutokana na viingilio tunavyowatoza watazamaji.Kilichogomba ni kwamba Daudi alitaka kujua ni kwanini Were-ma na wenzake waliiba pesa ya Escrow iliyokuwa imekusanywa na kampuni ya ndondi iitwayo Tanesco ambayo hata hivyo ilikuwa na msuguano na kampuni nyingine ya kitapeli ya kudhamini michezo ya kutumia nishati iitwayo IpTL.
Baada ya Daudi kugundua kuwa Goliati na washikaji zake akina Saada Mkuyati, Sosipita Muongo, A liar Kim Maswi na Benny Ndururu walikwapua njuluku za Escrow aliamua kuwaka kiasi cha kufanya mjengo usikalike.
Daudi hakuwa peke yake, aliungwa mkono na Joni Mnyika ambaye naye tunapanga kumtafutia wa kupambana naye siku moja ili tuone atakavyomaliza ngebe za wanaojitia wababe wakati si mali chochote.
By the way, mlimsikia madam Kipaza Sauti Anna Makidamakinda akimkingia kifua mura tena kwa kuongea kimombo cha hovyo na cha kihuni. Wajua alisemaje alipotakiwa atende haki?
Alimbwatukia Daudi akisema, “Dogo, kama umem-provoke mura aka-provotika ulitegemea nini?”Sijui kama walevi walioogopa umande au kughushi wanaelewa alichomaanisha bi mkubwa huyu mwenye kutia shaka kulhali.
Sikujua kuwa kumbe na wakubwa wakati mwingine wanakuwa wahuni kiasi cha kuchonga ‘slang’ na lugha za kihuni hivi!Nilidhani lugha hizi ni za walevi hasa wanywa gongo na wavuta bangi kumbe na wakubwa wamo!
Laiti ningekuwa Daudi ningemjibu bi mkubwa, “Bibi wawashwani wakati hii kesi si yako au unataka kuni-degrade na ni-degradike hata vidosho wanidharau na kuni-look down baada ya wewe kuni-dress down kwenye knockout zako na showoffs na showdowns? In fwact umenikosea adabu.”
Wakati Goliati akijiandaa kumshushia kipigo Daudi kabla ya kumkata kichwa si akina Tyson Steve Wasssira na wengine wakaingilia kiasi cha kuvurunga pambano!
Hivyo, bila kuzungusha au kupoteza muda tunaomba msamaha kwa kuvunjika pambano ambalo bila shaka lingeleta burudani ya aina yake kwenye mjengo na kayani.
Hata hivyo, tunampongeza Daudi kwa kutomuogopa Goliati ambaye alionyesha wazi kuchemka kutokana na kuhemkwa na mihasira hovyo. Ama kweli mtu mzima hovyo! Tumalizie kwa kumshauri Goliati Were apunguze kanywaji na kama anapata ile kitu yetu aache kabisa maana ubongo wake hauwezi kuhimili. Haifai jaji kuwa jaa au junk kama siyo janga.
Hivi karibuni tutaandaa pambano baina ya Khalima Mundee na Lete sia Nyenyere inshallah kama siyo la Jiwe-lenyeuhai Lusindie na Weenjee au Pita Musigwaa na Bill Lukuvii.
CHANZO: NIPASHE Julai 5, 2014.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment