The Chant of Savant

Friday 25 July 2014

Seriously, Mlevi kugombea urais

Baada ya kila msaka tonge kutangaza nia ya kugombea urais ambao unaanza kugeuka urahisi yaani ulaji rahisi, mlevi japo alishabainisha kuwa anaweza akatia timu, sasa anatangaza rasmi kuwa atagombea urais. 
Kwanini nisigombee iwapo naona watu wanaotegemea majina makubwa ya wazazi wao na umri mdogo unaoonyesha ukosefu wa uzoefu kuwania urais? 
 Kwanini nisitangaze iwapo urais umegeuzwa urahisi tena wa kuhomola na kuibia kaya? Kwanini asigombee iwapo urais ni kijiko cha kuchumia utajiri wa haraka kwa rais na ukoo na marafiki zake? 
Mlevi anapanga kufanya yafuatayo ili kuikomboa kaya toka kwenye mikono na midomo ya mafwisadi na mafisi. 
Mosi, atakuza uchumi kwa kutosafiri nje kwa vile ameishi nje sana. Hivyo, si mshamba wa pipa wala wa miji mbali mbali duniani. Nitapiga marufuku hata mawaziri wangu kupoteza fedha na muda kwenye uzururaji usio na tija kwa taifa. 
Wasaka’ per diem’ jiandaeni. Lazima niwashukie kama mwewe ashukiavyo vifaranga. Pia nitahakikisha najenga uchumi wa kizalendo unaotoa kipaumbele kwa wazawa katika uwekezaji badala ya huu uliopo ambao unapendelea wageni ukiwakomoa wazawa kutokana na kuwa wagumu kutoa ten percent. 
 Nani anataka uchumi unaoendeshwa na magabacholi kumi tu? Nitahakikisha najenga uchumi wa kutumainiwa badala ya uchuuzi na ufisadi unaoendelea ambapo kaya inasifika kwa kuwa na rasilimali nyingi lakini bado inaombaomba na kukopakopa kichizi. 
Pili, vitegemezi vyangu wala mke wangu hawataruhusiwa kujihusisha na siasa nikiwa madarakani. Hata hivyo, vilishasoma na kupata kazi vinavyoridhika nazo ughaibuni.  
Hivyo, msitegemee kuona wanangu wakijifanya marais wadogo wala mke wangu kujifanya rais wa kike kwa vile mumewe ni rais. 
Wakifanya hivyo nasweka ndani bila kuwatazama usoni. Ukitaka kuua nyani..? Nitatawala kama Mchonga kwa kuhakikisha urais haugeuki mali ya ukoo wala marafiki. 
 Urais wangu hautakuwa wa ubia kama wale waliosema kuwa urais wao si wa ubia wakimaanisha kinyume.  Kuepuka kujichanganya, lazima nitangaze mali zangu kila mwaka tena bila kukumbushwa wala kutafuta visingizio. Kutotangaza mali kwa kiongozi kama rais ni ushahidi kuwa ni mkwapuzi wa kunuka. 
Tatu, Bi mkubwa wake ni msomi wa kupigiwa mfano aliyesoma na Michelle Obama. Hivyo, hataanzisha NGO wala kugombea vyeo vidogo vidogo kwenye chama cha mlevi. Hata hivyo, nitaamuru katiba itamke wazi kuwa hakuna cha mke wala nani wa rais kutumia ofisi yake kwa namna yoyote kutengeneza njuluku. Enzi za akina Anna Tamaa na Shari zimepita. 
Nne, Mlevi ni msomi wa kupigiwa mfano ambaye hataingizwa mjini na vyuo vya kitapeli kwa kumpa shahada za uongo na ukweli halafu vije kumtembelea ili kumtoa upepo kama tulivyoshuhudia chuo kimoja cha kwa Joji Kichaka kikifanya. 
Tano, sera za mlevi ni usawa. Ndiyo maana analaani wale wanaotaka kutumia kete ya umri, jinsia, dini, maeneo ya bara au visiwani, mitandao uchwara, kujuana, kuhonga na jinai nyingine kutafuta urais. 
 Nichukue fursa hii kuwatahadharisha walevi na wapika kula. Yeyote mtakayemuona anakuja na sera za kibaguzi muogopeni kuliko ukoma. Hata kama hana mpango wa kugombea kwa sasa akijiandalia kugombea baadaye, muwekeni kwenye maweko ya kumbukumbu zenu na kuhakikisha hachaguliwi hata baada ya miaka 50. Ubaguzi ni ukaburu na anayeufanya ni kaburu mweusi anayepaswa kuzomewa hata na kunguru na wadudu. 
Sita,  kwangu urais ni utumishi wa umma na si njia yake na familia yake na marafiki zake kuuibia na kuunyonya umma kama ilivyo. 
Saba, lazima niweke wazi. Sigombei kwa vile eti kuna watu wanataka nigombee kama waongo wengi wanavyosema. Nagombea kwa vile nautaka urais ili niisafishe kaya kutoka kwenye uchafu huu na uroho wa watu kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa wala kuomba. Ukisikia mtu anasema eti ameambiwa na watu agombee jua mbea na muongo wa kupaswa kupigwa mawe hadi kufa. 
Nane, nagombea urais si kwa kutegemea mitandao ya bibi wala babu yangu. Wala sitegemei ukubwa wa jina la wazee wangu ambao bahati nzuri ni marehemu ambao walikuwa malofa wa kawaida. Nagombea kwa vile naamini walevi wanajua vitu vyangu na lazima wavikubali kwa ajili ya ukombozi wao. Mimi ndiye yule aliyetabiriwa na manabii kuwa atatokea rais ambaye hamkumtegemea na atawaweka huru. 
Tisa, kampeni zangu zitakuwa za uwazi na ukweli kwa maana kwamba walevi wasitegemee kuhongwa kanywaji kanga wala mabulungutu ya njuluku. Huku ni kuwanunua. Watakaowapa vitu kama hivyo wale na kuwaadhibu kwa kuwanyima kura.  
Kwani watu wa namna hii wanatafuta kura ya kula si kura ya kuwakomboa walevi.
Kumi,nitakamata na kusweka ndani wale wote waliouza kaya kwa wachukuaji kuanzia wale waliochukuwa Kiwila, IpTL, Richmonduli, Gesi, Tanesco, Net Group Problem, NBC, EPA, Kagodamn, Meremetuka, Mwananchi gold, SUKITA na ujambazi mwingine mwingi. 
Kumi na moja, nitahakikisha nawapa katiba mpya na safi ambayo itahakikisha kila jiwe linafunuliwa tangu kaya ipate uhuru kuhusiana na ufisadi. Hivyo, wanaozuia katiba mpya kuandikwa watakuwa wanapteza muda na kujipalia mkaa kama nitapata kuchaguliwa kuwa rais. 
Kumi na mbili, nitahakikisha urais unarejea kuwa urais badala ya kuwa urahisi kama ilivyo sasa ambapo unavutia majambazi na mafisi na mafisadi wengi ili wawaibieni wapendwa walevi wote.
Kwahereni tukutane nikianza kampeni!
CHANZO: NIPASHE 

6 comments:

Anonymous said...

Hapa tatizo la wapiga kura kuelewa maana ya kura zao na gharama zake kumpiga kura mtu asiye sahihi. Mpaka sasa wapiga kura watanzania hawajaweza kujifunza ni zaidi ya miaka sishirini imepita bado wanaendelea kuwapigia kura watu wasiokuwa wahaminifu katika ofisi za umma!

Anonymous said...

Watanzania tunapenda sana ufahari
Tangu mitandao imezuka imekuwa nongwa
Ukitaka kuwajuwa watanzania angalia glob ya mashughuli na ni mashughuli party haziendani na hali halisi wanapata wapi fedha tena cha kushangaza hata marais ,wake zao na vigogo wa serikali utawaona nao wamealikwa huko na kupiga mapicha ya pozi , Toba mungu wangu
Kweli tembo wetu watapona , sembe itaachwa kuuzika
Wameifanya pasipoti ya tanzania inanuka duniani nzima
Poleni wabongo lakini 2015 ndo uwamuzi sahihi mfifanye makosa, wapeni fundisho walipo madarakani waende shule

Anonymous said...

Mzee ruhsa rais awamu ya pili si yeye wala mkewe hana NGO yoyote
Mkapa na mkewe wote wana NGO pesa wanepata wapi watanzania tjiulize
Rais wa sasa mkwewe na NGO
Sijui naye ataanzisha ipi mwakani yetu macho
Cha kushangaza bongo bongo vioingozi wanajifanashina na viongozi wa USA au ulaya , but when its come to people hatuna pesa
Hata kusafiri kuja ulaya na dunia wanasafiri first class
Inashangaza kabisa tanzania makini wa kutupwa evn the barget 50 toka wahisani pamoja rasilimali zote
Nyerere alisema u humi tunao lakini tumeukalia
50 years bado omba omba
Wahisani haisadii tanzania ngo wanachuma uchumi wetu,
Tangu tumevumbua gesi ishakuwa nongwa
Nigeria wako wapi pamoja na kuwa produce wa mafuta no 3 in world bado masikini
Hatujifunzi bado
Tanzania need change and this should happen in 2015
Nawatakia idd njema

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon wote mmetoa mchango wa maana kazi kwa wahusika kusikia na kufahamu kuwa hila na janja yao vimegundulika na wanayofanya hawafurahishi wala kukubaliwa na wote. Nani anapenda taifa la kula kula?

Anonymous said...

Anon
Kweli tena wanasafiri na wake zao first
Haniingilii kichwani wake za marais Kuwa na walinzi
Hata mke wa waziri mkuu naye ana mlinzi
Waziri mkuu wa Tanzania hapaswi Kabisa Kuwa na ulinzi huu
Huyu ni mbunge na hakuchaguliwa na wanainchi sorry
Kwani rais atakuwa anachagua maziri wakuu wangapi
Kwa kipindi cha miaka 10
Mizigo hii hatuinoni inatughalim Watu wanaishi maisha ya akhera kwa kodi
Ukiliza tena wanajibu ya mkato hii ipo kwenye mkataba
Basi twambie au tuchieni mkataba yote ya viongozi tujue
Na nyumba za serikali kipengere kipi kilitumika wauguzi a vigogo, same fanya nini kwa Watanzania
Tunajua fika %100 ya wote waliuziwa nyumba hizi wana majumba Kila kona
Wengi wao wemeisha anza kupangisha nyumba hizo Mwakani tutatoa data zote

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemacho ni kweli. Ila kwa vile wetu ni ufalme uliojificha kwenye demokrasia kiasi cha walipa kodi kutouona, kimsingi kinachofanyika ni ujambazi na ushenzi ambao hauna mfano. Kwa Afrika wake za marais ni marais fichi wenye nguvu kwa vile wanashea kitanda na rais. Hapa hujaongelea akina Ridhiwan, Hussein Mwinyi na wengine wanaokuwa princes wazazi wao wanapochukua madaraka. Kwa ufupi kinachoitwa uongozi Afrika licha ya kuwa uongo ni ushenzi na ukoloni unaoendeshwa na genge la wakoloni weusi na watwana wao.