The Chant of Savant

Wednesday 30 July 2014

UKAWA wasibebeshwe zigo la Kikwete na CCM


          Kwa hali inayoendelea kuhusiana na majaliwa ya katiba mpya, kama busara haitatumika, yako mashakani. Kama ujanja ujanja, ubabaishaji, visingizio na urushi, kusukumiziana na kubebeshana lawana vinavyoendelea visipoachwa, kinachoonekana kama jitihada za kupata katiba mpya kitabakia kuwa kiini macho. Je nani alaumiwe kwa zengwe na mkwamo huu?
          Historia ya uandikaji katiba nchini inaanza pale rais Jakaya Kikwete alipounda Tume ya kukusanya maoni iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba. Tume hii ilipewa jukumu la kuandika kielelezo katiba (Draft constitution) ambacho kingejadiliwa na bunge la katiba (Constitutional Assembly) na kupitishwa kisha kupelekwa bungeni na kujadiliwa kama mswaada na hatimaye kupelekwa kwa rais kuusaini kuwa sheria. Mwanzoni, Kikwete, kabla ya kulishwa maneno na wahalifu fulani wenye woga kuwa katiba mpya ingefichua maovu yao, alikuwa kwenye mstari.
          Kama ilivyodaiwa mara nyingi bila kukanushwa na wahusika, inasemekana kuwa Kikwete aliitwa na watangulizi wake wakamtisha, wakamwongopea na kumshawishi hadi akaamua kuanza kujipinga na kuvuruga kazi njema iliyokuwa ikiendelea vizuri.  Hakika ni aibu.
          Mwanzoni Kikwete akiwaaminisha watanzania kuwa moja ya watakayomkumbuka kwayo ni kuwapatia katiba mpya itokanayo na wananchi na si watawala kama iliyopo.  Hata hivyo, tarehe 21/3/ 2014 itaingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama siku ya kiza ambapo Kikwete, kwa makusudi mazima na kinyume cha taratibu, alilihutubia bunge maalum baada ya jaji Warioba kufanya hivyo na kuamua kuvuruga kazi ya tume. Alichofanya Kikwete ni kuonyesha wazi mkengeuko uliojitokeza kwa kutoa msimamo wa chama chake. Heri angeishia hapo. Kwani, alikwenda mbele akaishambulia, kuizushia na kuidhalilisha tume aliyoiteua mwenyewe bila kulazimishwa wala kushawishiwa. Wengi walipigwa na butwaa na kujawa na simanzi wakijiuliza: Kulikoni, kipi kimemsibu rais? Tangu siku hiyo ya kiza Kikwete hakurudi nyuma. Ameendelea na mbinu za kichinichini kuhakikisha inaandikwa katiba aitakayo na si itakiwayo na wananchi.
          Hivi karibuni, Kikwete na CCM waligundua kuwa umma umestukia janja yao.  Hivyo, waliamua wakuwatwisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) lawama wanazopaswa kutwishwa CCM na Kikwete. Badala ya kukubali kuwa kitendo rais cha kumvizia jaji Warioba, kumshambulia, kutoa msimamo wa chama chake na kutokuwa tayari kukiri kuwa alikosea na kuomba msamaha, ndicho chanzo cha yote, wameanza kulalamikia UKAWA ili uonekane ndicho chanzo cha mkwamo wakati siyo. Je watanzania watakuwa wajinga na wasahaulifu kiasi hiki kukubali matusi ya nguoni kama haya? Je Kikwete na CCM watafanikiwa katika kutapatapa kwao hadi wakafikia kutoa vitisho kuwa kama UKAWA hawatarejea bungeni watabadili katiba waendele? Bahati nzuri, tofauti na Kikwete aliyetishwa na woga wa kuwajibishwa, UKAWA wameshikilia msimamo wao. Wamesema wazi hawako tayari kurejea bungeni na kujidhalilisha. Huu ni msimamo safi wa kupigiwa mfano unaoweza kusaidia kufanikisha mambo kadhaa muhimu.
          Mosi, kuinyima CCM fursa ya kuwatumia kuandika katiba chafu itakayoendeleza matakwa yake machafu.
Pili, kuzidi kuanika unafiki na kigeugeu cha Kikwete kiasi cha kumweka kwenye hatima ya kuweza kuachia ngazi akiwa na rekodi ya kuvuruga mchakato wa katiba mpya na kutumia vibaya fedha za umma na ofisi ya rais.
Tatu, umma kutopata katiba chafu na hivyo kuwa na hasira na wale waliozuia kupatikana kwa katiba wanayoitaka wenyewe iwatawale.
Nne, kuchochea hamu na hamasa ya kutaka katiba mpya baada ya Kikwete kuondoka ili itumike kufumua yote yaliyomsababishia kujipiga kujipinga asijue kesho hayo yatakuwa kichocheo cha kutekeleza kile alichotaka kukiepuka.
Tano, msimamo wa UKAWA utadhihirisha busara au ukosefu wa busara wa CCM na Kikwete kutokana na watakavyoamua kulimaliza tatizo hili. Baadhi ya wana CCM tena wasomi wa sheria kama Spika wa bunge maalum Samuel Sitta na waziri mkuu Mizengo Pinda wameishaonyesha uhovyo wao kwa kutishia eti kubadili sheria na kupitisha katiba chafu.
Sita, kuzidi kuichanganya CCM ikitaptatapa na kufichua ubovu zaidi ambao wananchi hasa upinzani unaweza kutumia kuunyesha umma wa wapiga kura jinsi ilivyoisha na kuishiwa.
Saba, CCM itazidi kuumbuka kwa hofu kuwa katiba isiyoitaka inaweza kupita. Hivyo, wahusika watatumia muda mwingi ima kujaribu kuficha madhambi yao au kutafuta nguvu ya kuendelea kuwa madarakani kwa gharama zozote. Hapa lazima tutegemee wizi wa fedha za umma kuongezeka kama tulivyoshuhudia wizi wa ESCROW hivi karibuni uliowachanganya CCM kiasi cha makada wao kujifichua walikokuwa wamejificha na kutaka kuzipiga bungeni.
Nane, mwitikio wa hovyo wa CCM utazidi kuwapa UKAWA hoja na hamasa ya kuhakikisha ufisadi huu wa kimawazo unakomeshwa.
Tisa. UKAWA watazidi kuona faida ya kuungana kama upinzani jambo ambalo wakiliendeleza hadi kwenye uchaguzi ni mwanzo wa kuizika CCM.
Mwisho, tutoa ushauri kuwa kadri CCM na Kikwete wanavyozidi kutumia mbinu za mwituni, wanazidi kufanya mambo kuwa magumu kwao.  Watumie busara ya kukubali kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Hivyo, hata wangewatishwa UKAWA lawama na zigo lao vipi, hawatafanikiwa kwa vile watanzania si majuha na mataahira kama wanavyowachukulia. Hakika, huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM. UKAWA lazima wajue hili na kushikilia msimamo wao ili kuwaumbua wanafiki na mafisadi wanaotaka kuhujumu na kuzuia kupatikana kwa katiba mpya.
Chanzo: Tanzania Daima Julai, 2014.

5 comments:

Anonymous said...

Wabunge Wapiga usingizi Bungeni ndiyo tatizo kuu ndiyo tunategemea pia kupata Katiba kutoka wabunge mihuri. Mimi nashangaa sana katika nchi maskingi kama hii, yenye changamoto lukuki. Mmbunge anakaa Bungeni mika ishirini au zaidi hawajwahi kuuliza hata swali moja.Aingii akilini!!!!!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hata wabunge wasingelala tusingepata katiba hasa ikizingatiwa kuwa Kikwete alipotishwa akina Mwinyi na Mkapa kutokana na madhambi yao aliamua kuiua katiba. Hata wafanyeje kuna siku tutapata katiba mpya.

Anonymous said...

Zigo analo kikwete kwa uvivu na woga wa kuchagua

Anonymous said...

Mimi si mtanzania lakini nasema kwa mungu gaa ya Watanzania ni serikali moja
Sitaki mbili wala Tatu

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umenena. Kama si upuuzi wa CCM nadhani Tanzania inahitaji serikali moja ili kuonyesha muungano wa dhati badala ya woga na madai ya kitoto kwa baadhi ya sehemu za muungano.