How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 22 July 2014

January Makamba na falsafa ya ujana katika chama kizee

BAADA ya January Makamba kulianzisha akaungwa mkono na Jaji Joseph Warioba kuwa rais ajaye lazima awe kijana, wengi tumejiuliza mantiki ya vijana kutaka kuingia madarakani kwa kutumia chama kizee. Kwanini isiwe shehe mpya kanzu mpya?
Hivyo, bila kuzungusha, kitendo cha Makamba na wengine wenye mawazo na mipango kama yake kutaka kutumia vyama vizee kinawatoa kwenye ulingo hata kabla hawajaingia.
Huu ni ushahidi kuwa hawana maandalizi wala sera na mipango ya maana yoyote. Baya zaidi, kinachowapiga chenga ni ile hali ya kujifananisha na Rais Barack Obama wa Marekani ambaye hakuingia kwa ujana bali umakini na mchango wake katika chama chake na taifa lake.
Hata kauli ya Obama ya ‘Yes, We Can’ ilijengwa kwenye ‘Hope and Change’ yaani matumaini na mabadiliko. Obama alijikita katika kujenga hoja zinazoingia akilini na kuzitetea na zikaeleweka.
Mfano, aliahidi kurejesha majeshi ya Marekani kutoka Iraq jambo ambalo liliwavutia wapiga kura wengi waliokuwa wamechoka na utawala wa mtoto wa kigogo George Bush ambaye hana tofauti na January Makamba. Hivyo, kudai kuwa Obama aliingia kwa kete ya ujana ni upotoshaji na uongo wa makusudi. Hii si tabia ya kisomi.
Pia ifahamike, kudandia ujana ni ukosefu wa sera. Watanzania wanahitaji sera na mawazo mbadala hata yakitolewa na mzee wa miaka elfu moja. Nani anajali kama wewe ni kijana?
Hii inatukumbusha maneno ya baba wa taifa, Mwl. Julius Nyerere alipoambiwa eti Jakaya Kikwete alikuwa na sura nzuri. Alijibu tena kwa kukereka; “Kwani tunatafuta mchumba?” Sambamba na hili la kina Makamba, “kwani tunatafuta mchezaji mpira au rais?”
Pia kina Makamba wanapaswa kufahamu kuwa hao wazee wanaowaponda walikuwa vijana waliotumia ujana wao kujiandalia wanachotaka. Na isitoshe, ni hao hao wazee waliowazaa na kuwaandaa kina Makamba wanaojisahau hadi kuwabagua hao hao waliowaumba kimwili na kisiasa.
Ajabu vijana hao hao waliopendelewa na kubebwa kwa kutumia nyadhifa za wazee wao ndio wanaoanza ubaguzi.
Japo ni kweli tunahitaji uongozi mpya wenye sera na mawazo na staili mpya ya kufanya mambo, lakini hautokani na ujana bali sifa zaidi ya hiyo.
Makamba hawezi kuwa makini. Kama yuko makini, basi uwezo wake wa kufikiri unatia shaka. Huwezi kutaka mambo mapya kwa kutumia chama kizee kilichochoka na kuishiwa dira.
Ukiachia ujana, Makamba na wenye mawazo ya kibaguzi kama yake wana nini kipya zaidi ya utimbakwiri? Makamba amebebwa na jina la baba yake. Ndiyo sifa pekee iliyomfikisha hapo alipo.
Makamba kujilinganisha na Obama ni tusi la nguoni. Obama hakubebwa na baba yake wala vigogo kama anavyofanya yeye. Nadhani kama kuna matusi CCM imewahi kutukanwa mojawapo ni hili la Makamba kutaka urais kupitia mgongo wa ubaguzi na kubebwa na marafiki wa baba yake.
Kimsingi, akichaguliwa atakayekuwa akiongoza nchi ni Yusuf Makamba na si January Makamba. Nani anataka George Bush Jr Tanzania ambaye anaweza kuendeshwa kama Joyce Wowowo (Kikaragosi) na kina Donald Rumsfeld wa Kitanzania?
Taifa letu halijafilisika kifikra na kisiasa kiasi hiki. Eti anasema wana mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya. Si kweli. Kama wana mawazo mapya basi ni ya kutumiwa na kujificha nyuma ya ubaguzi wa kiumri na majina ya wazazi wao. Makamba na wenzake ni wa kuogopwa kuliko hata ukoma.
Mbona haongelei uzoefu ili walau tumlinganishe na Obama ambaye alikuwa na uzoefu wa muda mrefu akilinganishwa na Makamba anayetaka kumtumia kutuingiza mkenge? Makamba anaweza kusema ana maarifa mapya. Je ameyapata kihalali? Mbona hataki kuongelea kutuhumiwa kughushi kuingia kidato cha tano?
Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, aliwahi kusema; ”Kuna vijana wenye mawazo ya kizee na wazee wenye mawazo mapya.” Hivyo, ujana tu si kigezo tosha wala cha kutuhangaisha kumsaka rais.
Tuna vijana wengi kwenye viwanja vyetu vya ndege wanaoruhusu mihadarati kupita na kuingia. Je, hawa ujana na maarifa yao ya jinai vinalisaidia nini taifa? Nadhani kwa sasa ukitaka kukosana na Watanzania, uje na ndoto na ngonjera za upya.
Jakaya Kikwete aliingia na gea hii hii ya ujana japo alikuwa mtu mzima na falsafa ya Ari mpya, Kasi Mpya, Nguvu mpya vyote vikiashiria ujana, lakini baada ya kuingia madarakani alivurunda kuliko wazee kama Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa ambao nao walivurunda, lakini ikilinganishwa na Kikwete wana nafuu.
Nani anataka fikra mpya za kifisadi, kasi mpya ya kuingia madarakani kutuibia na nguvu mpya ya kutegemea majina na mitandao ya wazazi? Si kwa sasa ambapo taifa letu limezamishwa kwenye umaskini na uongozi wa kujuana na kufadhiliana. Hatuhitaji rais atokanaye na ubaguzi uwe wa umri au jinsia.
Makamba na wasaka tonge wenzake wanajua wanachofanya wanapoongelea ujana na upya bila kuweka uzoefu. Wanashindwa kuelewa mazingira ya Tanzania ambapo mtu anapoomba kazi, mojawapo ya sifa anazotakiwa kuwa nazo ni angalau uzoefu na si upya wala ujana na ndoto zake.
Tulishaambiwa na wahenga kuwa ujana ni maji ya moto. Leo Makamba ana miaka 40. Mwakani atakuwa na miaka 41 ambayo inamtoa kwenye kundi la vijana na kumuingiza kwenye uzee. Makamba anaongelea ujana bila hata kufikiri kuwa anaweza akatokea kijana wa miaka 30 akamwambia, “mzee January hebu tuachie sie vijana” akaishia kukaangwa kwa dhambi hii hii anayoianzisha kwa tamaa ya ulaji. Ni kichekesho cha aina yake kijana kukana uzee akategemea kutumia chama kizee!
Chanzo:Tanzania Daima Julai 23, 2014.

4 comments:

Anonymous said...

Semesemi tujuwe mengi Nani anatufaa Kuwa rais. Tanzania sisi wapiga kura

Anonymous said...

Sifa ya mgombea urahisi
1. Hajawahi kushika uongozi wowote katika chama cha mapinduzi(Chukua chako Mapema) C.C.M wala kuwahi kuwa mwanachama hichi chama.

2. Anatakiwa kuwa mzalendo wa kweli na siyo wa porojo kama hawa sasa.

3. Anayetambua uongozi ni dhamana na siyo mali yake bianfsi.

4. Anayefahamu maana ya cheo cha Rais ni nini na yeye anawezaje kuchangilia maendeleo ya maisha na uchumi yanayofaidisha jamii yote ya Tanzania.

5. Anatakiwa hana mahusiano ya aina yoyote yale na viongozi wote wa zamani na waliopo sasa.

6. Anatakiwa Rais atayeweza kuwasulubu na kuwaburuta kwenye mkond wa sheria wale wote wezi wa mchana wa mali umma bila mipaka wala upendeleo.

7. Anatakiwa Rais mwenye mawazo na maarifa muda mfupi na mrefu pia.

Ukiangalia vizuri hapo utaona utaona hakuna neno ujana, wala jinsia ya kike wala kiume. Hivyo iwapo January anategemea kuwa rais basi anatakiwa kujipima hapo kama iwapo ana fuzu kutokana na hizi sifa zilizotajwa.

Kimsingi iwapo kiongozi atatoka ndani mfumo sasa hadithi porojo itaendelea pasipo shaka kabisa. Hivyo kama kweli tupo makini basi tuangalia hizo sifa ndiyo tunaweza kupata kiongozi sahihi katika wadhifa wa Urais.

Kuna Baadhi ya watu wanadanganywa kwamba Rais ni lazima anatakuwa kuwa na uzoefu wa uongozi. Unaposema. Nachoelewa mimi Uongozi una miiko na taratibu na siyo uzoefu.

Hivyo unapapata kiongozi aliye-nje mkondo wa uwozo yeye kuwa rahisi kufuata taratibu na miiko kuliko hawa wanaojitangaza kutaka kugombea wadhifa huu.

Ingawa ukweli wamekuwa katika uongozi wa serikali muda mrefu tena wakiona kila kitu kwa macho na matendo na wakiwayafurahia yanayoendelea kudidimiza nchi na maendeleo

Anonymous said...

Sifa ya mgombea wadhifa wa cheo cha Urais Tanzania 2015

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hapo juu nawashukuruni kwa mawazo yenu pevu ambayo bila shaka yatatusogeza mbele katika harakati za kumsaka rais ajaye.