How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 15 July 2014

Kijiwe chalaani serikali na milipuko ya Arusha

BAADA ya kupata taarifa za kuhuzunisha kuhusu shambulio jingine jijini Arusha, kijiwe licha ya kutoa salamu kwa wahanga, kinalaani ushenzi huu unaopaswa kukomeshwa badala ya kuzoeleka.
Pamoja na maswali mengine mengi, kijiwe kinauliza: Je, ni magaidi au washenzi fulani wanaotaka kutuchonganisha na magaidi ili tuwapige tafu kwenye ugomvi wao?
Leo Mijjinga ndiye analianzisha: “Jamani sasa haya yameanza kuwa mazoea. Yaani Arusha inashambuliwa mara tatu na hakuna anayenyea debe. Kunani hapa? Lazima watueleze hawa wanaotuhadaa kuwa wanahakikisha usalama wetu.”
“Yakhe hili la Arusha latisha na kuhuzunisha. Ila hili la kuhakikishiwa usalama sahau. Usalama gani wakati twaibiwa kila uchao na sasa twashambuliwa na mabomu kila uchao? Walianza Zanzibar na sasa wemefanya Arusha kuwa uwanja wao wa kujidai. Iko wapi sirikali na majeshi na ndata zake?” anauliza Mpemba kwa hasira.
Kapende hangoji. Anakwanyua mic. “Kuna jamaa yangu wa intelligence kanitonya kuwa kinachoendelea Arusha ukiachia mbali lile shambulio la kwanza la kisiasa kwenye mkutano wa Chakudema ni baadhi ya maadui wetu wanaotaka kutuchonganisha na Al Shubuub ili tuingie kwenye vita yao na kupoteza muda na njuluku badala ya kufanya mambo mengine ya maana.”
Msomi Mkatatamaa akionyesha dalili zote za kuudhika na kukasirika kwa pamoja anazoza: “Lolote linawezekana usawa huu hasa ikizingatiwa kuwa vita ni gharama na isitoshe kaya yetu haina uongozi zaidi ya uongo uliofichwa nyuma ya uongozi uchwara. Isitoshe, wale tuliwakung’uta kule kwa mzee Kabila, nadhani, hawafurahi kuona tunaendelea kujiimarisha kijeshi bila kutupa homework ya kutu-keep busy hata kupunguza nguvu ya majeshi yetu. Hivyo, kitaalumu tunashauri wahusika wasikurupuke na kunyooshea Al Shabuub vidole. Badala yake wachunguze other leads and possibilities on unexpected angles. We’ve to expect the unexpected in this matter.”
Mipawa aliyekuwa akimalizia kipisi chake cha sigara kali anaamua kutia guu. “Je, mageshi yanafanya kazi gani mbona kila mara Arusha inashambuliwa?”
“Umeuliza swali zuri tu. Sijui kama mageshi yetu yana muda na mambo kama haya iwapo wakuu wake wanasifika kwa kuwatisha wapinzani, lakini wakajisahau kuwa kulinda kaya ni zaidi ya kutisha wapinzani na wachovu. Umesahau kilichofanyika hivi karibuni kwenye sherehe uchwara za muunganiko ambako bosi wao alisema wazi wazi kuwa zililenga kuwatisha wachovu?”
Bwege anachomekea: “Hapa bila shaka Mzee wa Misiba na wakubwa wenzake wanajiandaa kwenda kule kujipitisha wakiwahadaa wachovu kuwa wanajali wakati wanapoteza fedha na muda kwenye mambo ya hovyo kiasi cha kuacha kaya bila ulinzi hadi ishambuliwe kila mara.”
Sofi Lion Kanungaembe hakawii. Kwa usongo wa wazi anasema: “Ulitaka aende Mafia? Kama kiongozi wa kaya lazima aende kuwafariji watu wake. Jamani hata kama mnachukia jamaa mbakizie na utu.”
Baada ya Sofi kufoka, Kanji naye kapata stimu. Anakula mic: “Iko Hindi katwa guu vunjika kono. Balaa kuba sana dugu nyingi napoteza ungo.”
Mgosi Machungi aliyekuwa anasinzia sinzia anaamua kutia timu. “Ndata badaa ya kuimaisha ulinzi kayani wako bize kukimbizana na wapingaji kiasi cha kuruhusu maadui washambulia kaya. Sijui kwanini tinawalipa njuuku zetu wakati hawafanyi kazi.”
Mzee Maneno anajibu haraka: “Wewe, ndata haendi mahali ambapo hakuna mshiko. Tena wakikusikia unataka waende kwenye mibomu badala ya dili watakubambikizia kesi ya ugaidi huu huu wa Arusha.
Au tupeleke mgambo wa jiji wakateketee huko. Maana ukiona wanavyokimbizana na wamachinga utadhani ni maadui wa kaya. Kama nyie warume basi nendeni mkapambane na mibomu kama hamjatolewa utumbo wana izaya nyie.”
“Usemayo ni kweli mtu wangu. Sina shaka Bwana Misiba atajihimu kwenda kule. Mbona walipopigwa mibomu na kuuawa wanachama wa Chakudema hatukuwaona wote wakikimbilia Arusha au ni yale yale ya mkuki kwa nguruwe?” anauliza mzee Ndomo ambaye mara nyingi huwa hapendi kuchangia.
“Yakhe hapa untoboa. Kweli, mbona walipouawaa wapenzi wa Chakudema hatukuona mzee Njaa Kaya, Mizengwe Pinder na wengine wakimiminika kule au kwa vile walioshambuliwa ni wageni?”
“Nyie mnaishi dunia gani. Mbona Mkuu alikwenda Arusha kuhani misiba ya wahanga wa shambulizi la kanisa kule Olasiti?” anarejea Sofi Kanungaembe.
Mijjinga hamkawizi: “Umeambiwa wafuasi wa Chakudema na si waumini wa Olasiti.”
Sofi akiwa anajiandaa kujibu Msomi anakula mic.
Baada ya kuona lawama zinaanza kutawala busara utadhani ugomvi wa Kafulilaa na Weremaa, Msomi anaamua kutumia usomi na busara zake kuepusha kuachana na mada.
Anasema: “Jamani, hata kama wakubwa zetu wamekuwa wazembe au wakishabikia baadhi ya ndugu zetu kuuawa na hata kuteswa na ndata, huu si wakati wa kulaumiana zaidi ya kusaka jibu hasa nani amefanya mashambulizi haya na ni kwanini. Hivyo, nashauri wachangiaji waachane na hasira na lawama.”
Kanji anamuunga mkono Msomi: “Wambie somi. Sisi nalia dugu zetu umia yeye naleta lawama. Kwanini hapana laani hii crime? Sasa naambia rahisi akamate yote naua dugu yetu Arusha mara moja.”
“Tiwe wakwei jamani. Hatiwezi kunyamaza wakati ndugu zetu wa Chakudema waliuawa na hawa hawakwenda. Kanji kwa vile waiouawa ni dugu zako azima uonje joto ya jiwe kuwa hata wae wa Chakudema walikuwa dugu zetu sisi.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Andaaman Kinamna. Kabla ya kujua ni yeye tulidhani ni jamaa wa Al Shubuub. Acha tulitoe mkuku. Kama si jamaa kusimamisha gari na kujitambulisha mbona tungemchoma moto.
Chanzo: Tanzania Daima

3 comments:

Anonymous said...

Milipuko ya Arusha jirani huyo
Ana wivu kwani watalii wote wanakuja kwetu
Wakenya wao

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, japo sitaki kulenga vidole, kuna ukweli katika uoni wako wa mbali.

Anonymous said...

Sababu za kitentejinsia mikutano ya kisiasa.Sasa matokeo yake panya nae kaingilia sasa maofisa wa sababu kitelejinsia wanapwaya.!