How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 9 July 2014

Kwanini serikali haina fedha wakati inaibiwa ikinyamaza?


          Ripoti kuwa serikali yetu imefilisika kiasi cha kushindwa kupata pesa ya bajeti yake licha ya kutisha zinaudhi sana. Wahusika wametutaarifu kuwa hakuna pesa ya kutosha lakini licha ya kutupa sababu za uongo, hawakuonyesha nia ya kutatua tatizo hili linaloanza kugeuka donda ndugu. Badala yake wameonyesha kuliendeleza kwa kufanya mambo hatari na hovyo kama matumizi mabaya, kuingia mikopo ya kiwizi na mikataba ya uwekezaji ya kijambazi ambavyo havina tija kwa taifa bali watu wachache wanaodai na kupewa cha juu almaaruf kama ten percent.
          Wahusika wamejitahidi kuficha ukweli. Walipotoa taarifa walitoa zile zinawaondolea lawama na kujitenga kabisa na kuhusika na kadhia na aibu hii. Kwanza, taarifa hizi, kwa wenye akili zinazua maswali mengi kuliko majibu. Moja ya maswali muhimu yanayoibuliwa na taarifa hizi ni kwanini hakuna pesa? Je tatizo ni nini? Kama serikali haina pesa mbona wakuu wa serikali wanatanua na kutumia kama watawala wa nchi za ghuba ya Uajemi zenye utajiri wa mafuta? Rejea wanavyotumia muda mwingi angani kwenye madege na ughaibuni bila kujali kuwa nchi inaendelea kufilisika.
          Hata hivyo, kama tutaangalia ukweli kama ulivyo, kuna sababu nyingi za kufilisika kwa serikali japo hazitajwi zote. Tunaambiwa wafadhili hawakutimiza wajibu wao na ahadi zao. Je sisi tumetimiza wajibu wetu kama serikali? Je ni wajibu wa serikali kutunza watu wetu? Je tabia zetu za kimatumizi zinaunga mkono sababu za kufilisika kwa serikali yetu? Kwanini tuwakabe wafadhili kutumiza ahadi na wajibu wao wakati sisi hatufanyi hivyo? Je tumewahi kujiuliza nini tutafanya siku wafadhili watakapogoma au kuachana na kuchangia bajeti zetu? Huwezi kuendelea kama nchi huku ukiendeleza uombaomba, matanuzi na uchuuzi wa roho za watu wasio na hatia kwa kisingizio kuwa hawasemi wala kuingia mitaani. Kuna siku watafanya hivyo yatakapowazidi.
          Japo serikali inaweza kuendelea kujidanganya kuwa wananchi hawatabadilika, ukweli ni kwamba ipo siku watasema enough is enough.  Ni jambo la kusikitisha na kufedhesha sana kugundua kuwa serikali imekuwa ikijifanya kuwa haisikii wala kuona malalamiko ya wananchi ili mambo yasahaulike kirahisi. Hili vile vile si jibu bali kuzidi kulikuza tatizo. Watanzania wanataka kujua fedha yao inakwenda wapi na kwanini?
          Wenye akili watahoji sana kiasi cha kuwaudhi wahusika wanaotaka waonekane hawahusiki na umfilisi huu. Kazi ya wenye akili ni kuhoji bila kujali wala kuogopa patilizi.  Haiwezekani nchi yenye kila aina ya raslimali iendelee kufilisika kila mwaka tena baada ya kuwa huru kwa zaidi ya miaka 50. Lazima kutakuwa na tatizo tena kubwa tu. Uzuri ni kwamba tatizo hili linajulikana na kama umma utaamua linaweza kumalizwa kwa kuwawajibisha watawala wasiojali maslahi ya wale waliowaweka madarakani. Haiwezekani nchi yenye uongozi makini unaowajibika iendelee kuombaomba na kukopa kopa mwaka nenda mwaka rudi. Lazima kutakuwapo na tatizo ambalo linatulazimu wote kama jamii kulishughulikia kabla nchi yetu haijawekwa reheni kiasi cha kutawaliwa na wakoloni upya.
          Ili kuondokana na tatizo la umfilisi wa serikali, yafuatayo yanapaswa kufanyika tena haraka na kwa makini:
          Mosi, serikali iache matumizi mabaya ya fedha mali na raslimali za umma. Lazima kuwepo na nidhamu ya matumizi ambayo inapaswa kuwekwa kwenye katiba na wakatakaokiuka wawajibishwe mara moja.
          Pili, watanzania wahakikishe wanapunguza ukubwa wa serikali ambao unasababisha sehemu kubwa ya fedha za bajeti kutumika kwenye kuihudumia badala ya kuhudumia wananchi.
          Tatu, serikali iliazimishwe kupambana na ufisadi ambao unaanza kuzoelekana kuonekana kama kitu cha kawaida na halali. Sambamba na ufisadi, serikali ikomeshe wizi wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka ambapo kikundi kidogo cha watu kinaishi kwenye pepo ya neema huku umma uliowazunguka ukiishi kwenye jehanamu na umaskini wa kutengenezwa na kikundi hiki.
          Tatu, lazima serikali itakayoingia au kuwa madarakani iwe na sera mujarabu na si ubabaishaji na bora liende.  Hatuwezi kuendelea kuendesha nchi kishikaji na kisanii huku watu wetu wakiangamia kwa majanga ya kutengenezewa kama umaskini.
Nne, serikali ilazimishwe kukusanya kodi vilivyo ukiachia mbali kuzuilikwa kutoa misamaha ya kodi ya kifisadi ambapo wahusika hutumia fursa hii kujipatia pesa ambayo ingekuwa mapato ya serikali ambayo yangetumika kuwakwamua watanzania. Si uzushi. Tanzania imegeuka shamba la bibi kwa wawekezaji ambao kimsingi ni wachukuaji wanaokuja mikono mitupu na kuondoka mabilionea kama ilivyotekea kwa makampuni kama RITES, IPTL, Richmond, Dowans na mengine mengi ambayo yametusababishia ugumu wa maisha bila ulazima. Pia makampuni mengi ya uchimbaji madini na uwekezaji katika nishati yameliibia taifa kama ilivyofichuliwa hivi karibuni ingawa wahusika wakiwakilishwa na kuwadi wao Ami Mpungwe walikanusha. Laiti Mpungwe angeeleza ni kwanini aliacha ubalozi na kujiingiza kwenye biashara ya uchimbaji wa madini, huenda wengi wangemwelewa vizuri.
          Tumalizie kwa kuwahimiza wananchi wasikubali kusikinishwa huku wanaofanya hivi wakiendelea kujitajirisha. Lazima kama jamii na taifa tusimamie maendeleo na maisha mazuri ya watu wetu. Wananchi wanapaswa kauachana na ukondoo wa kujifanya kama hayawahusu, kulalamika na badala yake wachukue hatua kuanzia sanduku la kura hadi mitaani. Hii nchi ni yetu sote na hatuna pengine pa kwenda kudai maendeleo na maisha bora. Uzuri ni kwmba serikali iliyomo madarakani ilituahidi maisha bora kwa wote ambayo, bahati mbaya, yamegeuka maisha hovyo na balaa kwa wengi huku maisha bora yakiwa ni kwa wote wale wenye kuwa madarakani na si wananchi wote.
          Tunaamini kuwa, kwa machache tokana na ufinyu wa nafasi, wahusika yaani watawala na watawaliwa wamepewa namna ya kuondokana na kadhia na aibu ya taifa kuombaomba na kuishi kwa kutegemea wafadhili kana kwamba tunaishi jangwani bila raslimali zozote. Uchumi mnao lakini mnaukalia.
Chanzo: Dira Julai, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Sifa ya Binadamu aliye hai ni kuona na kujitambua...Viongozi wetu wanauwezo wa kuona tuu na siyo kujitambua ili ndiyo tatizo kuu.

Maana wanyama wote porini wanaona kamwe hawawezi kutambua, ndiyo sababu wanaishi na mikakati ya kula na kushiba na siyo zaidi ya hapo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umetoa falsafa kubwa ambayo ikitafsiriwa vizuri inaweza kuwaweka watawala wetu kwenye kundi moja na hayawani. Ubarikiwe kwa kusema vyema.