Kwanza, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kuumaliza mwaka pia kuuona mwingine. Wengi hawakuumaliza. Ni majaliwa na mapenzi ya Subhana. Kifupi, tunajaribu kudurusu yaliyojiri mwaka 2014 ili kujiandaa kwa ajili ya 2015. Mwaka 2014 umeweka historia kama wa hasara tokana na yaliyojiri nchini.
Januari: Sanaa zilizoishia kuwa hasara kwa taifa. Rais Jakaya Kikwete alivunja baraza la mawaziri. Aliwatema baadhi ya mawaziri na kuteua wengine. Hii ni kawaida. Tokana na sura zilizoingia au kurejeshwa bila kustahili, mwaka ulianza kwa hasara. Nani alitegemea watuhumiwa Saada Mkuya, Mary Nagu, Adam Malima, Makongoro Mahanga na Wiliam Lukuvi kueendelea kuwa mawaziri wakati wanajulikana kughushi wazi? Rejea tuhuma za Msemakweli Keinerugaba na jinsi CVs za baadhi zilivyo tata.
Feb., taarifa ya kuuawa zaidi ya tembo 10,000 yatolewa na The Mail on Sunday na kuwatuhumu wakubwa.
Machi: Jengo la ghorofa 16 la mitaa ya uhindini liliporomoka na kuua takriban watu 19. Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi profesa Anna Tibaijuka alidai angeamuru jengo dada lililojengwa kinyume cha sheria kuporomoshwa. Baadaye aliramba matapishi yake. Wenye fedha walimshinda nguvu na jengo husika likaumaliza mwaka na kuuona mwingine.
Machi 21 rais Kikwete alihutubia Bunge la Katiba na kuua rasmi rasimu ya Jaji Joseph Warioba ya wananchi na kuamuru kuandikwa rasimu fisadi ya CCM.
Aprili: Kikwete alitunukiwa tuzo ya kutia shaka na genge la matapeli wa kinigeria wamilki jarida la African Leadership kule Marekani. Tuzo hii ya aibu iliitwa Africa's Most Impactful Leader of the Year kabla ya kupewa nyingine iitwayo Icon of Democracy Septemba na tapeli wa kinigeria, Elvis Iruh hata baada ya polisi kuua waandamanaji wasio na hatia! Hasara nyingine!
Mei iliingia kwa hasara kubwa iliyotikisa taifa hadi mwisho wa mwaka. Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulilwa007Aa alifichua wizi wa sh bilioni 200 ziliongezeka na kufikia 400 kwenye akaunti ya escrow. Ufisadi ulishika kani baada ya Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Julius Kashaza kuuawa siku moja baada ya kuhojiwa na Bunge juu ya ufisadi wa sh bilioni 83. Hadi mwaka unaisha hakuna aliyeushughulikia.
Juni: Kashfa ya wabunge kuomba na kupewa fedha toka kwenye mifuko ya umma. Waliotajwa ni Job Ndugai, William Lukuvi, Angela Kairuki, Pindi Chana na wabunge Betty Machangu, Livingstone Lusinde, John Komba, Eugen Mwaiposa na Gudluck Ole Medeye (wote CCM). Wizi kwenye serikali za mitaa uliendelea.
Julai Chuo cha IMTU chatupa viungo vya waswahili kwenye mashimo ya mchanga.
Agosti: Matokeo ya kutia shaka ya kidato cha sita.
Septemba: Rasimu ya katiba feki ilipitishwa rasmi.
Oktoba: Kashfa ya miss Tanzania ambapo Sitti Mtemvu aliibuka kidedea na kunyang’anywa taji.
Novemba: Mvuragano kashfa ya escrow.
Mwaka 2014 ulishuhudia hasara nyingine. Shirika la Usafiri Dar Es Salaam (UDA) lilitwaliwa kinyemela na kifisadi huku serikali ikitoa taarifa zenye kukanganya. Rejea meneno ya Septemba 2014 ya naibu waziri wa fedha, Malima aliyekaririwa akisema, “Jiji la Dar es Salaam lina hisa 51katika UDA na serikali ina hisa 49.” Hadi mwaka unaisha, hakuna anayejua ukweli ni upi na ni lini serikali iliuza hisa zake na kwa bei gani.
Mwaka 2014 ulishuhudia vifo vya wabunge William Mgimwa (Kalenga) na Said Bwamdogo (Chalinze). Katika uchaguzi mdogo nchi ilishuhudia ufalme ukichukua nafasi ya demokrasia. Mtoto wa Mgimwa, Godfrey alichaguliwa kurithi kiti cha baba yake huku mtoto wa rais Ridhiwan Kikwete akichaguliwa mbunge wa Chalinze. Kurithishana madaraka kulianza kushika kasi. Mwana wa kigogo, January Makamba aliteuliwa waziri kutimiza utabiri wa baba yake
Pia deni la taifa lilifikia sh trilioni 27 bila maelezo huku wakubwa wakiendelea kuiba na kufuja na kuzurura ughaibuni huku kashfa ya kuficha mabilioni Uswizi ikiuawa. Mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani Jaji Fredrick Werema akimtisha balozi wa Uswizi Olivier Chave kuacha kukumbushia kashfa hii.
Nafasi haitoshi. Tunaacha mengi mengine. Mwaka 2014 uliisha kwa vituko ambapo rais alimtimua Tibaijuka aliyekatiwa sh 1.6 bilioni huku akisema eti fedha ni ya IPTL. Wengine waliotajwa kukatiwa fedha ni Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), William Ngeleja (Sh40.4 milioni), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni), Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni), Majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji Aloysius K Mujulizi (Sh40.4 milioni), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni), Emmanuel Ole Naiko (Sh40.4 milioni), Lucy Appollo (Sh80.8 milioni), Askofu Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Pia, Safari za nje kutibiwa, na baadaye kufichuka kansa ya tezi dume na baadaye kansa ya kizazi na kuachiwa huru kwa msamaha wa rais kwa mtuhumiwa wa EPA, Ajay Somai vilitawala huku watuhumiwa wakuu wa escrow wakiendelea kuwekwa “kiporo” kuonyesha hasara inavyoendelea kiasi cha mwaka 2015 kuanza kwa hasara zaidi.
Msisahau funga mwaka ya mauaji ya tembo na ndege ya rais wa China kusafirisha vipusa.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 7, 2015.
No comments:
Post a Comment