Pamoja na kwamba ndata huwa
wanatughasi hata kutubambikizia kesi wanapotudaka, hatuna kinyongo nao zaidi ya
kuwaonea huruma kwa wanavyotumiwa wakijiona hadi kuhatarisha maisha yao. Baada
ya kutokea mashambulio mengi kubwa likiwa la hivi karibuni pale Ikwiriri,
kijiwe kimekaa kama kamati kutoa rambirambi na tamko. Kinatoa shule kwa ndata
wajitambue na kuchukua hatua kabla hawajamalizwa.
Mgosi Machungi
siku hizi anajilawa kweli kweli. Leo kamuwahi hata muuza kahawa utadhani kuna
upupu kitandani mwake. Nani anajua? Huenda bi mkubwa kamwekea mgomo. Hayo tuyaache.
Mgosi baada
ya kuridhika kuwa yakama au korum
imetimia, anatafuna mic, “Tilishawambia kuwa wanatumika kishiasha lakini
walitidhaau. Unaona sasa majambazi yanawaua kama swaa na kuchukua vya moto vyao
kiahisi kana kwamba ni vichanga?”
“Mgosi nawe
kwa kuanzia stori katikati huna mfano! Kumbe unaongelea mauaji ya ndata kule
Ikwiriri siyo?” anauliza Mchunguliaji huku akijiweka vizuri kwenye benchi.
Mpemba aliyekuwa
ndiyo amemaliza kuagiza kahawa anakwea mic “Yakhe hii yantisha sana hadi nataka
nirejee zangu Pemba. Yawezekanaje hawa wanioitwa majambazi wavamia vituo na
kupora silaha kirahisi hivi kama hakuna namna hata baada ya kuwa hii ishatokea kule
Mwanza na kwingineko?”
Kapende
hangoji Mpemba aendelee. Anakula mic kinomi, “Kwani ukienda Pemba unadhani
utanusurika wakati kaya ni moja Ami? Hapa dawa si kufanya kama akina Kanji
ambao wakisikia tatizo hukimbilia kaya jirani hadi mambo yapoe. Tunapaswa
kusimama na kuwatetea hawa jamaa wanaoonekana kushindwa kujitetea hata
wanapohujumiwa kwa kutumiwa vibaya na watafuta ulaji,” Kanji anamkata jicho la
hasira kusikia akitaja magabacholi lakini hasemi kitu.
Mijjinga huku
akiweka vizuri mavazi yake tokana na kupenda kuulamba na kuonekana kama
Peedeejee, anapoka mic, “Hivi kama hawawezi kujilinda wataweza kutulinda kweli
au ni kutumia kodi zetu kuwaneemesha wakati tukihangaishwa na wahalifu?”
“Kumbe wewe
huwa wanakulinda! Kama kuna wanachonifanyia sikingine bali kutudunda
tunapoandamana kupinga ujambazi uwe wa bunduki au kalamu. Kwa vile umewalenga,
huenda wakaelewa somo,” Mipawa anajibu huku akitabasamu.
“Usemayo ni
kweli. Wenye kulindwa ni wanono wanaoweza kuamuru ndata hata kuwakomesha wabaya
wao binafsi. Mnaojidanganya kulindwa mmeliwa na mtaliwa sana,” Mbwamwitu
anachomekea huku akimtazama Mgosi kwa chati akijua fika asivyopenda neno
kuliwa.
Mzee Maneno
anaamua kumpa sapoti Mbwamwitu japo huwa wanakosana mara kwa mara kutokana na
maneno yake ya kufyatua. Anasema, “Kweli, wangekuwa wanatulinda si
wangewakamata majizi na mafisadi yanayotuibia kila uchao. Si wangewakamata hata
hawa wadokozi wa kura zetu wachakachuaji.”
“Yakhe
usemayo nkweli. Wangekuwa wanatulinda si wengeenda kamata wale walokataa hata
kuapisha viongozi kwa vile eti waloshinda upinzani.”
“Wankamate
nani wakati wote chama moja dugu yangu. Usinikumbushe nshike nshike wa Segerea
wa kuapishana kwa kutumia mawakili baada ya wachakachuaji kuzidiwa ujanja na
people power,” Anachomekea Kapende.
Mheshimiwa Bwege
anaamua kutia guu,“Hapa halindwi mtu. Tunalindwa na Mungu vinginevyo, naona
ndata kama wanyanyasaji wanaotumiwa na wanono, finish. Nadhani hawana haja ya
kunung’unika wala kuonewa huruma hasa ikizingatiwa kuwa wao ndiyo wamewalea
majambazi n ahata wengine kushirikiana nao wasijue hawa jama hawana dini.”
Baada ya
Msomi Mkatatamaa kumaliza kusoma gazeti lake la kitasha anaamua kutia guu huku
kila mtu akiwa na hamu ya kusikia atasemaje. Anakohoa kidogo na kubwia kahawa
yake na kusema, “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hawa ndata waliwalea majambazi
hata baadhi yao kufikia kushirikiana nao wasijue kuwa hawa hawana dini kama
alivyosema msemaji mmoja aliyepita. Kimsingi, huu si wakati wa kuwalaumu ndata
bali kuwasikitikia na kuwapa darasa wajue kuwa nao wanaliwa kama wale
wanaodhani wananyanyasa kwa vipigo kila siku.”
Anabwia kahawa
na kuendelea, “Kwa waliosoma mambo ya kiutawala tunajua fika nani wa kulaumiwa.
Ulitegemea nini kwenye kaya ambapo kila mtu
anaruhusiwa kujiibia bila kushughulikiwa? Unategemea nini kwenye kaya
ambapo kila mja anaruhusiwa kutajirika bila kutoa maelezo ya alivyopata huo
ukwasi? Kama kuna kitachowamaliza ndata si kingine ni hiki. Pia kile kitendo
cha kujiruhusu kutumika kuwa kikwazo cha ukombozi lazima kitawagharimu hata
maisha yao kama ilivyotokea. Na huu si mwisho wa filamu yenyewe. Watanyotolewa roho
wengi tu.”
“Kumbe tatizo
ni kubwa kuiko tinavyoiona!” anashangaa Mgosi Machungi.
Msomi anaendelea
kudema, “Hivi mlitegemea nini wanene kufunga ndoa na mafisadi na wezi? Kufanya hivi
ni kuweka kaya kwenye autopilot. Kwa wale tuliopanda ndege autopilot ni mfumo
wa kuendesha ndege bila rubani au rubani kuifanya ndege ijiendeshe yenyewe.”
Kabla ya
kuendelea, Sofia Lion Kanungaembe anauliza, “Kweli ndege inaweza kupaa bila
rubani jamani?”
Msomi anajibu,
“Nilitegemea swali hilo. Usingeuliza ningeshangaa. Ukweli ni kwamba si ndege
tu. Siku hizi kuna hata magari yanaweza kukatisha mitaa bila dereva. Hilo si
muhimu leo. Muhimu ni kwamba tangu wanene walipojiingiza kwenye mashindano ya
kuibia kaya, basi imebaki kama haina mwenyewe. Kwanini majambazi wa mitutu wasiichukue
iwapo wanaona wenzao wa kalamu wameishafanya hivyo? Umemsikia mnene akilaani
jinai hii au kueleza atakavyopambana nayo? Kimsingi, ndata wasipogutuka
watatolewa kafara na wataliwa wakijiona kama wale wanaowanyanyasa.”
Kijiwe kikiwa
kinanoga si mvua ikaaza kunyesha!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 28, 2015.
No comments:
Post a Comment