Hivi karibuni waziri mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara ya kikazi nchini Qatar na kutangaza “neema” kwa watanzania. Pinda alikaririwa akisema kuwa watanzania watanufaika na ajira nchini Qatar japo hili linatia shaka. Je hawa watanzania anaosema watafaidika wameandaliwa vya kutosha kielimu? Wanao ujuzi unaouzika kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa Qatar inavutia watu toka India, China na hata ulaya tena wenye sifa na ujuzi wa juu zaidi? Je watanzania wanakwenda kufanya vibarua au kuajiriwa kama anavyodai waziri mkuu?
Pinda alikaririwa akisema
Pinda aliongeza “La kwanza ni Kilimo. Hapa Qatar ni jangwa kila mahali. Wamekubali kuja kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi kwa sababu sisi tuko karibu nao zaidi kuliko Marekani au Brazil.” Japo ni kweli kuwa Qatar wanahitaji mazao tajwa hapo juu, kwanini kuwaruhusu kuja kujilimia badala ya sisi kuwahimiza wakulima wetu walime na kuwauzia hawa Qatar ambao wakiruhusiwa kulima, licha ya kuua soko la wakulima wetu, watazalisha na kwenda na kusindika kwao na kuuza nje? Kwa tunaoishi nje tunashuhudia mfano bidhaa nyingi za mboga zikotoka uarabuni na kuuzwa huku wakati tukijua wazi kuwa hawa jamaa hawalimi vitu hivi zaidi ya kununua kwingine na kusindika na kuuza. Kwanini tusianzishe viwanda vya kusindika mazao haya na kuwauzia yakiwa yamesindikwa badala ya kuwaruhusu waje watwae ardhi na kujilimia huku wakiua masoko yetu? Ni kwanini serikali yetu inakuwa sahaulifi kirahisi hivi? Rejea uzembe iliofanya na inaoendelea kuufanya kwa kuuza korosha mbichi India huku India nao wakiipanda na kutokea kuwa wazalishaji wakubwa wa korosho kuliko sisi tuliowauzia.
Pinda aliendelea kusema,“Wanaweza kupata mchele, matunda, nyama kwa maana ya machinjio na viwanda vya kusindika nyama lakini pia katika uvuvi wa samaki. Tunayo bahari ila mitaji yetu ni midogo. Kwa hiyo wamekubali kuangalia eneo hilo pia.” Huu ni upungufu mwingine. Kwanini kuruhusu watu kuja kuvua nchini wakati tunao uwezo wa kuwawezesha wavuvi watu wakazalisha samaki na kuwauzia hawa Qatar? Nijuacho ni kwamba kama biashara hii kichaa itafanikiwa, samaki wetu wengi wataibiwa kama ilivyotokea kwa wanyama wetu waliosafirishwa hai na kwenda kuwekwa kwenye zoo huko Qatar jambo ambalo linatunyima watalii. Mfano mtu anayetaka kuja kuona twiga au nguchiro ana shida gani ya kuja tena Tanzania wakati twiga wamepelekwa kule na kutumiwa kwenye utalii wakati sisi tukiendelea na biashara kichaa? Kimsingi, hii naona kama nadharia tamu iliyokosa vitendo hasa kama maswali muhimu hapo juu hayatajibiwa kikamilifu.
Hata hili debe linalopigwa kuhusiana na ajira Qatar lina walakini hasa ikizingatiwa kuwa wenzetu waliotangulia kupeleka watu wao kufanya kazi za ndani hata vibarua kama anavyotetea Pinda kama vile Kenya na Uganda wanajutia kufanya hivyo hasa baaada ya wengi wa watu wao kurejeshwa kwenye majeneza baada ya kuuawa na wengine kutoroka tokana na kufanyiwa ukatili wa kutisha. Si siri. Nchi nyingi za ghuba zina ubaguzi wa kunuka hasa kwa waafrika. Hivyo, Pinda badala ya kutegemea kupeleka watanzania kuajiriwa Qatar atumie fursa ya uhusiano uliopo kuwashawishi kuja kununua bidhaa hapa nchini. Kama serikali itapata masoko ya mazao kama aliyotaja Pinda halafu ikatekeleza ngonjera yake ya “Kilimo Kwanza” uwezekano wa kutengeneza ajira hapa nchini ni mkubwa kuliko kupeleka watu wetu utumwani.
Inashangaza kwa Pinda kuaminishwa kuwa watanzania watapata ajira Qatar wakati hawajui kiarabu. Kama wanahitaji watu anaosema Pinda basi nchi za Sudan, Chad na Mauritania zinaweza kutosheleza soko la Qatar. Isitoshe, hata wahindi wameishajaa Qatar ukiachia mbali wachina na wazungu. Kwanini Pinda hakutambua kuwa kazi alizoahidiwa si chochote bali kazi za majumbani ambazo adha yake ni kubwa hasa kutokana na unyanyasaji, ubaguzi, unyonyaji n ahata mauaji?
Hata kama aliyoahdiwa Pinda yangekuwa ya kweli, kupeleka watanzania nje kupata ajira bila kutengeneza ajira hapa nchini ni kujidanganya hasa ikizingatiwa kuwa tuna wahitimu wengi. Nadhani serikali badala ya kuhangaika na kutafuta vibarua kwa watu wake ingeenda kule kujifunza jinsi nchi za kiarabu zilivyonufaika kutokana na utajiri wa mafuta na gesi. Sisi tumegundua mafuta. Mikataba yake imegeuka siri ya mafisadi wachache huku watu wetu wasijue wala kuona faida ya ugunduzi huu. Nadhani kinachojionyesha hapa ni sawa na kile kinachoendelea nchini Nigeria ambapo serikali inaagiza mafuta nje kwa bei mbaya wakati inazalisha mafuta. Pia wanigeria wengi, sawa na watanzania, hawaoni faidi ya kugunduliwa mafuta nchini mwao wala hawana ajira.
Kukaribisha wageni waje kulima na kupeleka chakula kwao huku wakiajiri watu wetu kama vibarua kutaleta balaa badala ya neema. Maana hata hawa wakulima wanaolima kidogo cha kujilisha watakimbilia kwenye ajira za wakulima wa kigeni na kuishia kuishi kwa kununua chakula badala ya kukizalisha. Kwanini hatujifunzi kutokana na kuletewa mazao ya kikoloni tuliyoita cash crops yaliyowateka watu wetu wakaishia kuyazalisha kwa wingi wakati bei zake zikiporomoka wakaishia kuyauza na kutumia fedha chache wapatayo kununulia chakula? Kimsingi, Afrika imekuwa ngumu kujifunza. Uongozi wetu unaendelea kurudia makosa. Kwanini tunasahau kirahisi kuwa marehemu Thomas Sankara rais wa zamani wa Burkina Faso alisifika tena kwa muda mfupi aliotawala kwa kuikomboa nchi hiyo kutokana na kuhimiza wananchi wazalishe chakula cha kuwatosha kabla ya kufikiria mengine? Maana ukiangalia tatizo kubwa la Afrika ni kushindwa kujilisha kiasi cha kutegemea vyakula feki toka nje. Leo ukienda madukani kwenye nchi nyingi za kiafrika unauziwa matunda ya makopo kutoka nje. Wakati hayo yakifanyika, kwenye nchi hizo matunda ya wakulima wa mashambani yanaoza tokana na kukosekana wanunuzi. Hii imesambaa hata kwenye uzalishaji wa sukari na bidhaa nyingine ambapo wakubwa uhongwa na wafanyabiashara na kuingiza bidhaa hafifu zinazoua mazao ya wananchi wao. Tumeona hili halitoshi. Sasa tunakaribisha wageni waje kutulimia kana kwamba hatuna mikono wala akili. Je hii ni biashara au biashara kichaa?
Chanzo: Dira
2 comments:
Hi Nkwazi, I having been looking for your contact details but see none. Please let me know how I can get in touch with you. dearafricaproject.wordpress.com -> That's me.
Hello Kellz,
My email is nkwazigatsha@yahoo.com.
Thanks and welcome
Post a Comment