Baada ya kushuhudia mauzauza, wizi, ujambazi, ufisadi na mazabe mengi, kijiwe kimeamua kulia na kufunga kwa ajili ya wanayama wetu wanaotoroshwa kila uchao kana kwamba kaya yetu haina wa kuisimamia. Waliopewa dhamana kufanya hivyo wanajihudumia kwa kushirikiana na majambazi ya kimatifa.
Baada ya kuingia na kuamkua, Mgosi Machungi analipua bomu akisema, “Japo timekuwa tikipigia keee escoo na ujambazi mwingine, huu ujambazi wa kutolosha wanyama wetu na madini vinatisha kuiko hata huu udokozi wa mabiioni?”
“Usemayo ni kweli Mgosi. Tumekuwa tukiangalia ufisadi wa fedha na rushwa bila kuuliza maswali kuhusiana na kwa mfano kwanini lisirikali halikuwajibishwa kutokana na kutoroshwa wanyama wetu miaka mitano iliyopita,” anajibu Mipawa huku akijiweka vizuri kwenye benchi.
“Walianza meno ya tembo wakaongeza twiga na wanyama wengine. Sasa wamegeukia hata kenge! Kunani?” anshangaa Mbwamwitu.
“Mie naona heri wangeuza nyoka au hata mafisadi kama wana shida ya fedha fedheha hivyo. Maana wanivyouza raslimali zetu utadhani hakuna kesho. Utadhani watapokufa kila kitu kitaisimama au kuisha wallahi,” analalamika Mpemba huku akikatua kashata.
Kapende anamuunga mkono, “Yakhe umeniacha hoi kusema eti lau wauze mafisadi. Laiti kungekuwa na soko la watumwa na tukaondoa hawa wahalifu, ningependekeza wauzwe utumwani ili waonje adha ya utumwa waliowaweka wachovu wetu kwa miongo nenda rudi. Natamani hawa wamanga wanaoiba twiga wetu wawanunue binti zao wakawawoweee wakome.”
Mijjinga kaguswa pabaya. Anakwanyua mic na kumwaga mipwenti, “Mijitu hii mijizi sijui aliyeiroga nani! Unaruhusu wanyama hai kusafirishwa ili watu wafungue zoos waache kuja kufanya utalii kwako halafu unajiona mjanja. Jamani hawa ngurumbili mafisi na walafi na mafisadi wasipoacha jinai yao kaya itaingia kwenye machafuko. Kitanuka na wao ndiyo watakuwa wa kwanza kupoteza. Maana wachovu hawana cha kupoteza except their chains.”
“Mie sishangai kuona wanyama wetu wakiuzwa tena kwa bei ya dagaa. Kama wameuza utu wao wenyewe kiasi cha lisirikali zima kuwekwa kwenye mifuko michafu kama ya akina Rugemalayer na Harbinger unategemea nini? Ukiangalia hata fedha kiduchu wanayohongwa huku wanaowahonga wakiondoka na utajiri wa kunuka unahoji utimamu wa akili za ngurumbili hawa,” Msomi anaamua kukatua mic.
Mzee Kidevu anakwanyua mic, “Hamna haja ya kulalamika. Wameanza na tembo na baadaye kenge kesho watauza wajomba zao yaani manyani. Baada ya hapo bila shaka watawauza mama zao watake wasitake.”
“Wawauze mama zao mara ngapi? Kwani hawa akina mama wanaotumika kusafirisha miunga tena wengine kwa kubeba mimba na kuzitoa baada ya kufikisha mzigo au vyangu wanaojiuza mitaa ya Ohayo na Kinondo au wale wanaoajiriwa au kupata shahada kwa kuvua nonihino zao wana tofauti gani na mama zao? Mheshimwa Bwege anaamua kudema.
“Kama wangewauza mama zao originali na si watu wetu mie lisingenihangaisha. Nina usongo kuona mama zao nao wakifanya hii biashara na udhalilishaji wanaowafanyia mama zetu. Sijui kama watoto wa wakubwa nao wanavuliwa nonihino kupata shahada au kazi kama akina Kajamba nani.” Anauliza Mchunguliaji aliyekuwa akimaliza kusoma gazeti la Udhuru Leo.
Sofia Lion Kanungaembe anaamua kujibu mapigo tena kwa nyodo, “Jaribuni kuheshimu akina mama. Kwanini kuuza iwe ni mama zao na si baba zao?”
Msomi anakwanyua mic, “Sofi usemacho ni kweli. Leo umeongea pwenti kwa mara ya kwanza hasa kulingania usawa wa kijinsia. Unataka wawauze baba zao mara ngapi iwapo mibaba mizima inabebeshwa mimba za unga? Unataka wawauze mara ngapi iwapo mibaba mizima inaendeshwa na mafisadi? Sema wameishajiuza hata wao. Utawaona wakati wa kuelekea kwenye kampeni watakavyo kuwa wakihaha kwenye majumba ya magabacholi na mafisadi kutafuta mabwana wa kuwafadhili kwenye kampeni zao.”
Kanji anamkata jicho Msomi na kuamua kuingia kifua mbele akidema, “Somi pana changia vatu vote. Sasa fisadi na hindi vapi na vapi dugu yangu? Kama Harbinda moja naiba siyo hindi yote baba yangu. Kama vana siasa nataka hindi saidia fedha kidogo hapana iko baya.”
Mgosi Machungi haridhiki, anaamua kutia guu tena, “Kanji acha ongo yako dugu yangu. Kwanini siku zote juuku toka kwa hindi na si Swahili?”
Mipawa naye anaamua kutia guu tena, “Kanji hajakosea. Hivi kwa mfano kama yule Kamlaani Ahmed aliyetorosha wanyama wetu mwaka 2010 akiamua kuwasaidia waliomwezesha kufanikisha dili utamlaumu au walioamua kujirahisisha akawatumia? Mbona huko nyuma hawakuwa hivyo?”
“Mie sijali hata wakishikishwa ukuta au kutwaliwa na Popobawa kwa sababu ya upogo na tamaa zao za kula bure. Kiniogomba ni sisi kuwa mashahidi wa wizi wa raslimali hata kura zetu. Kuna haja ya kubadilika. Maana hii sasa ni too much.”Mpemba anazoza.
“Na tutakuwa mashahidi zaidi.Huoni akina Muongo na wezi wenzake wanavyozidi kutesa huku tukiteseka baada ya kulindana na wanaopaswa kuondoa balaa hili kujifanya hamnazo wala hayawahusu? Heri wauzane wenyewe kwa wenye ili waliwe wakijiona,” anajisemea Kapende huku akionyesha ishara mbaya ya dole.
Kijiwe kikiwa kinanoga likapita shangingi la yule aliyekuwa katibu wa wizara ya wanyama aliyekula dili na ponjoro na baadaye kuteliwa ubalozi kwa M7 Ladisilasi Kombha. Acha tumfukuze ili tumtie adabu!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 14, 2015.
No comments:
Post a Comment