How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 12 January 2015

Kwa ufisadi huu amani itatoweka haraka


          Pamoja na kwamba ufisadi umeanza kuzoeleka nchini, madhara yake yanaanza kujitokeza japo kwa kiwango cha chini na kidogo. Japo watawala wetu wamejiridhisha wakiimba wimbo wa amani, mambo si shwari. Vikundi vya vijana waliokata tamaa vimeanza kujitokeza na kuiweka amani yetu kwenye mtihani. Polisi waliokata tamaa tokana na kulipwa mishahara kidogo wameanza kuonyesha hasira zao kwa kutowashughulikia wanaovunja amani.
          Matukio ya hivi karibuni ya vijana waitwao Panya Road kuvamia mitaa, kunyang’anya na kufanya vurugu bila kuzuiliwa haraka ni ushahidi kuwa walio nacho wachache tena wanaoibia umma kwa kubariki ufaidi, hawatafaidi walicho nacho. Amani itatoweka haraka kama wimbi la ufisadi litaendelea bila kuzuiliwa. Japo hii inaweza kuonekana kama kuongeza chumvi kwenye hali, utegemezi wa mtutu wa bunduki kuhimili vitendo vya uvunjaji amani vitokanavyo na ugumu wa maisha si jambo la kutegemewa sana. Bila haki kutendeka kwa wananchi wote, amani ambayo watawala wetu wamekuwa wakiimba na kukariri kama kasuku ni ukungu tu. Itatoweka na wote tutaumia. Hakuna atakayekuwa salama. Kwa vile tunaishi kwa kutegemeana. Walio nacho wanawategemea zaidi wasio nacho kuliko wao wanavyowatagemea. Matajiri wanawahitaji maskini kuliko maskini wanavyowahitaji matajiri.
          Hivi karibuni vyombo vya habari vimeripoti kutokea kwa uporaji wa halaiki katika mitaa ya Tabata, Magomeni Kagera, Sinza, Mwananyamala, Kinondoni, Kijitonyama, Manzese, Kigogo na Buguruni ilionja joto la ugumu wa maisha ya vijana hawa almaarufu kama Panya Road.
          Hili si jambo la kawaida wala la kuchkuliwa kama la kihalifu tu. Ni kiashiria kuwa vijana wamechoka kufa njaa wakati wakiwaona wenzao walizaliwa kwenye familia tukufu wakiukata na kutakata. Vijana wanaona na kujua kinachoendelea. Wanaonekana kuhamasika kuonyesha hasira zao. Japo tunaweza kuwahita wahalifu kirahisi, hebu sisi wenye fursa na ukwasi kwenye jamii tujiweke kwenye viatu vyao. Tushukuru Mungu imechukua muda mrefu kwa hasira za vijana kujionyesha tokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutosha. Sasa vijana wameelimika. Wahitimu wa vyuo hawana kazi. Wanaishi ima kwa kutegemea jamaa zao au kubangaiza. Je hii itaendelea lini? Je jeshi kama hili la wasio na kazi laweza kuishi sambamba na ufisadi wa kunuka na amani ikaendelea kuwapo?
          Vijana wa sasa si wajinga. Wakisikia kikundi fulani kimeiba mabilioni kwenye kashfa ya escrow hata trilioni kama ilivyodaiwa juzi kwenye kashfa ya ujenzi wa bomba la mafuta toka Mtwara kwenda Dar es Salaam wanajua ukubwa wa fedha hii. Vijana wanajua kupambanua. Wanajua fedha inayoibiwa na wakubwa wachache na washirika zao toka nje inaweza kuwafanyia nini kubadili maisha yao. Wanawajua, tena kwa sura, wote wanaowaibia. Wanawajua wote wanaokufuru kuita mamilioni na mabilioni ya shilingi vijisenti na fedha ya ugolo. Wanawajua hata wale wanaowatetea. Wanawafahamu fika wabaya na wazuri wao katika jamii.
          Kwenye zama za maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano, vijana wanapata habari karibu kutoka kila pembe ya dunia. Hata hivyo, walichelewa kutokana na wengi kuzuzuliwa na nyenzo za mawasiliano kwa kupendelea miziki na filamu wasijue huwezi kupata vitu hivi bila kipato. Wengi wana simu lakini hawana uwezo wa kulipia line au internet ili wafaidi maisha. Wakubwa zetu wamewekeza kwenye imani kuwa vijana wataendelea kutumia mitandao kutafuta mambo ya upuuzi wasijue kuwa wanapokosa fedha ya kuishi kisasa lazima watahoji ni kwanini iwapo nchi yao imejaliwa raslimali na utajiri lukuki. Watahoji kwanini wengine tena wachache wanakula na kusaza hata kutapanya wakati wao wanaishi maisha ya kijungujiko. Tutake tusitake wanahoji tena zaidi ya tunavyodhani. Vijana wa sasa si wa mwaka 47.
          Vijana wanajua kuwa umoja wao ni nguvu na ndiyo silaha pekee inayoweza kuwaondoa kwenye maisha magumu. Wanajua ukubwa wa nguvu yao. Leo wanaitumia kama Panya Road kumalizia hasira kwa wananchi wasio na hatia. Kesho wataenda ikulu liwalo na liwe. Ni suala la wakati tu hata hawa machinga wanaofukuzana na migambo ya jiji watasimama na kupambana nao huku wakivamia maduka ambayo mengi yanamilkiwa na wageni. Kwanini wao wawe wageni nchini mwao na wageni wawe wenyeji nchini mwao?
          Nani alitegemea kuwa vijana wangejitoa mhanga kutembea kilometa 1,000 toka Geita kwenda ikulu Dar es Salaam kumwambia rais kuwa ufisadi umekithiri nchini? Japo vijana waliofanya hivyo wamebatizwa jina la vijana wa CHADEMA, hata kama ni kweli, hawa hawana tofauti na wale vijana waliowasoma kwenye historia waliotembea mwendo mrefu hadi wengine wakapoteza maisha ili kuunga mkono Azimio la Arusha lililokuwa limeahidi kubadilisha maisha yao. Hata kama limeuawa, Azimio la Arusha bado linajulikana sana hasa wakati huu ambapo vijana wameonja machungu ya ufisi, ufisadi, ubepari na uroho vinavyoonekana kuwa matokeo ya siasa za kiliberali za kisasa zinazowageuza kuwa wanasesere wasijue shida itawaamsha. Wanasikia yaliyofanywa na wenzao wa Burkina Faso. Wanaona maandamano yasiyo kwisha kule Ugiriki ambapo wenzao wanataka ajira. Wengine walikuwa kule wakaondoka baada ya maisha kuwa magumu au kuanza kuonekana kama ndiyo chanzo cha matatizo. Wengine wamejaribu kuuza unga na kuishia magerezani. Wamezamia meli na kugundua kuwa hakuna maisha tena ughaibuni. Wanajua kuwa ni nyumbani pekee wanaweza kuishi kama watu.
          Tumalizie kwa kuwashauri viongozi wetu waachane na fikra za kizamani kuwa vijana wataendelea kuogopa mitutu ya polisi. Wanaogopa njaa kuliko mitutu kwa vile wakijaribu kuleta mabadiliko wanategemea kusonga mbele badala ya kuendelea na woga ambao si jibu. Hivyo, hawa wanaojitahidi kurithisha ulaji kwa watoto na jamaa zao wanapaswa kujua kinachowangoja. Hizi nchi tunazotolea mifano kama zenye machafuko zilipitia huku tulipo. Tieni akili. Bila kupambana na ufisadi, tujue tunaifukuza amani taratibu. Itatoweka tu. Haiwezekani wachache wakala na kusaza wakati wengi wakifa njaa au kuishi maisha magumu wakati hii nchi ni mali yao wote.
Chanzo: Dira.

No comments: