Wakuu wa Jeshi la Polisi wakikenua baada ya kutupia cheki na fisadi Harbinder Sethi Singh mwizi wa escrow |
Tanzania sasa iko msambweni. Inatenzwa
kana kwamba haina viongozi, na kama wapo, hawaoni wala hawasikii, ukiachia
mbali kutofaa wala kujihangaisha kupambana na majanga yanayowakabili umma ambao
sasa ni yatima. Kuvamiwa kituo cha polisi cha Ikwiriri, Pwani hivi karibuni na
wanaosemekana kuwa majambazi ni kiashiria cha uoza wa mfumo fisadi. Askari
wawili wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu waliripotiwa kufa huku bunduki saba
na risasi 60 ambazo, bila shaka, madhara yake yatakuwa makubwa baadaye
zikiibiwa. Inashangaza polisi wanaopaswa kulinda usalama wetu nao si salama. Je
hapa nchi ni salama? Ajabu hata kadhia hii ilipotokea, serikali haikuja na
tamko stahiki lau kuonyesha kuwa kuna serikali. Je kuna magenge ya watu
yanayotaka kuingia msituni kama ilivyowahi kudaiwa na baadhi ya vigogo wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa bunge la katiba wakisema kuwa kama rasimu ya jaji
Warioba ingepita wangeenda msituni? Je hawa siyo sehemu nzuri ya kuanzia
upelelezi? Je kuna kitu watu hawa wamenusa kiasi cha kuanza kujiandaa au ni
matukio tofauti? Jikumbushe kauli za John Komba, mbunge wa Mbinga na William
Lukuvi (Ismani)? Ni bahati mbaya. Hata waheshimiwa hawa walipotoa madai hatari kama
haya, hawakuhojiwa kwa vile ni vigogo wa chama na serikali.
Ifahamike kuwa Ikwiriri si kituo cha
kwanza wala mwisho cha polisi kuvamiwa. Ilishatokea kule Mkamba Kimanzichana na
Bukombe Geita. Kinachogomba ni kwanini serikali, hata baada ya kuvamiwa kituo
cha kwanza, haikuchukua hatua kuzuia kurudiwa kwa jinai hii kama hakuna namna?
Unaweza kutoa hitimisho lolote hasa ukizingatia kinachofanyika kwenye
kushughulikia kashfa za wizi wa mabilioni ambapo baadhi ya wezi wanaonekana
kutoguswa hata wakitenda jinai kiasi gani. Hawa wanashindwa kuanza kuanzisha
majeshi yao?
Ukivuka mpaka ukajielekeza kwa
kinachofanyika Nigeria ambako kundi la Boko Haram linaihenyesha serikali au
Somalia ambapo al-Shabbaab wanaipa hali ngumu serikali nchini humo na nchi
jirani ya Kenya, unaweza kujua ninachomaanisha hapa. Hata haya makundi kama al-Houthi
kule Yemeni, al Qaeda Maghreb na mengine mengi yalianza hivi hivi. Je wizi huu wa silaha toka vituo vya polisi
unaashiria nini kwa taifa ambalo liko msambweni kutokana na kukosa uongozi
makini na wenye visheni?
Zama za awamu ya kwanza, kitu kama hiki
kingetokea, mipaka yote ingefungwa na wahalifu hawa wangesakwa na kutiwa adabu.
Lakini sasa nani afunge mipaka wakati watu wameziba masikio wakihangaishwa na
wizi wa fedha za umma na kuusaka ukuu bila kuwa na ajenda yoyote ya kuufayia
umma zaidi ya kuibia na kuutumia watakavyo kama ambavyo imezoeleka kuwa urais
kwa sasa ni kijiko kikubwa cha kuchotea utajiri kwa mwenye kuwa nao pamoja na
familia, marafiki, hata waramba viatu wake?
Kwa matukio haya matatu ya kuvamia,
kuua askari, kupora silaha, kuharibu mali ya umma, kuruvuga amani, kutenda
jinai, kumilki na kutumia silaha kinyume cha sheria na kutishia usalama wa
taifa, ni ushahidi kuwa taifa letu si salama tena. Kama tunashindwa na magenge
ya wahalifu wawe wanatumwa na wakubwa wanaotishia kwenye msituni au wanasukumwa
na jinai yao, je tukivamiwa na taifa jingine tutafurukuta kweli? Inakuwaje
tunapata polisi wengi wa kuwapiga wapinzani na waandamanaji lakini tunakosa
hata polisi wa kujilinda?
Uvamizi wa vituo vya polisi licha ya
kulidhalilisha jeshi la polisi, unatishia maisha ya askari wetu ambao hawakwepi
lawama kwa kujiruhusu kutumika kisiasa huku maslahi na usalama wao vikiwa
hatarini. Ili kuwa salama askari wetu
wanapaswa kuasi na kuacha kutumiwa kisiasa kama walivyofanya wenzao wa Tunisia,
Burkina Faso na kwingineko ambako serikali zilizokuwa zimelala kwenye usukani
zilifurushwa baada ya askari polisi na jeshi kukataa kutii amri za kuzuia
waandamanaji waliolenga kukomboa nchi zao.
Polisi wetu wanafanya kazi katika mazingira
magumu. Wana mishahara na marupurupu kidogo sawa na watanzania wengine
ikilinganishwa na wanasiasa. Pia wanaisha maisha ya chini sana. Ukienda kwenye Kota
zao, nyingi zinatia aibu. Wengine hata sare zao zinaonyesha ugumu na uhovyo wa
maisha wanayoishi. Hapa hujaongelea udhalilishaji na chuki wanavyopambana navyo
baada ya kutumiwa kisiasa kuwapiga na kuwaumiza watu wasio na hatia waliopaswa
kuwalinda. Je kuvamiwa kwa vituo vya polisi ni jinai ya kawaida au chuki za
wananchi dhidi yao? Tunapaswa kuzama zaidi.
Japo lolote lawezekana, mazingira ya
ukosefu wa maadili yaliyojengwa tangu kuondoka serikali ya awamu ya kwanza ni
ya kulaumiwa kwa matukio haya. Watu wanataka bunduki ili wafanya ujambazi na
kuwa matajiri wakijua fika mfumo wetu haumbani mtu kueleza alivyopata utajiri
wake. Huu ni motisha mkubwa kwa wanasiasa na wahaloifu bila shaka.
Wakati umefika wa kuwataka watawala
wetu wahakikishe usalama wa watanzania wote wakiwamo polisi wanaoshughulikia
usalama huu. Pia umefika wakati wa polisi kuuhoji mfumo na mamlaka
zinazowajengea mazingira ya kufanya kazi na kuuawa katika mazingira magumu
kirahisi hivi. Wavunje ndoa na wanasiasa
na mafisadi na kufunga ndoa na umma.Tunatuma salamu za rambirambi kwa jeshi la polisi
tukishauri IGP ajiuzulu kwa vile ameshindwa.
Chanzo; Tanzania Daima Januari 28, 2015.
No comments:
Post a Comment