Baada ya
wimbi la ufisadi kutikisa taifa letu, kumeanza kujitokeza dalili za woga
miongoni mwetu. Hii ni baada ya kuwepo manung’uniko mengi toka kwa wananchi
wanaoona kama mambo yanakwenda ndiyo siyo. Rejea mfano, vijana toka Geita
walioamua kutembea kilometa yapata 1,000 kwenda ikulu kumwambia rais
awawajibishe watuhumiwa wa ufisadi ikiwa ni pamoja na kumtaka apambane na
ufisadi kwa vitendo. Japo polisi walifanikiwa kuwazuia vijana hawa bila kosa
lolote, ukweli ni kwamba hali ya taifa letu si nzuri.
Baada ya
nyufa, tena nyingi, kujitokeza, wapo walioanza kutafuta jinsi ya kupata adui wa
kumtupia lawama. Mmojawapo wa walioonyesha wasi wasi huu dhahiri ni shehe muu Issa
Shabaan Simba aliyekaririwa akizituhumu nchi za magharibi wakati akihutubia
mkesha wa Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W)
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mazoezi, Korogwe. Shehe mkuu
aliwaasa watanzania kuwa makini na uchonganishi wa nchi za magharibi akidai
zinafanya hivyo ili ziweze kuuza silaha.
Ni bahati
mbaya kuwa shehe mkuu hakutoa mifano ya nchi ambako nchi hizi zimefanya hivyo
na lini zimeanza kufanya hivyo. Japo ni kweli kuna baadhi ya nchi za kiafrika
zimegeuzwa soko la silaha na wizi wa raslimali zake kama DRC, hali kwa Tanzania
ni tofauti. Tanzania hakuna cha uchonganishi wala nini zaidi ya uongozi mbovu
na ufisadi. Hata hivyo, wanaodhani kuwa amani inaweza kutoweka tokana na
uchonganishi wanashindwa kuona ukweli wa kadhia hii. Kwa mfano, huwezi kudai
eti nchi za magharibi zinatuchonganisha kana kwamba sisi ni taifa la mataahira
wanaoweza kuambiwa gombaneni bila sababu tukafanya hivyo. Hii haingii akilini
hata kidogo.
Nadhani kama tutagombana si kwa sababu ya
kuchonganishwa bali kuchoshwa na mfumo wa kujihudumia ambapo wachache
wanawatumia wengi kujineemesha wakati wengi wakiendelea kuwa maskini bila
sababu ya msingi. Nchi yetu ina raslimali ambazo zinachezewa na watawala wetu. Rejea
mfano kutoroshwa wanyama wengi tu hapo Oktoba 26, 2010 kupitia uwanja wa ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Tangu ufiadi huu kufanyika serikali imekaa kimya
kana kwamba hakuna kilichofanyika. Baya zaidi, hata hawa wanyama walkioibiwa
hawakupelekwa kwenye nchi za magharibi bali Qatar. Mtuhumiwa wa jinai hii ni
raia wa Pakistani aliyeshirikiana na watawala wetu wanaojifanya kutojua lolote
kuhusiana na kadhia hii.
Ni bahati
mbaya hata viongozi wakubwa wa dini wanaliona hili na kulifumbia macho
wakitengeneza maadui bandia ili kuwaaminisha wananchi na kuwanusuru watawala
marafiki zao. Hapa hatujaongelea madai kuwa ndege ya rais wa China iliondoka na
shehena kubwa ya pembe za ndovu. Hili lilipotokea, wakubwa zetu walitoa majibu
ya kitoto yasiyoingia akilini na wakanyamaza. Mchezo kwisha. Kwa sasa tuna
wananchi wengi wa China wakifanya magendo ya vipusa na biashara ya kimachinga
huku wamachinga wetu wakipigwa, kufukuzwa na kunyang’anywa mali zao kila uchao.
Hawa hakika, ndiyo watakaotuchonganisha kwa vile wanaziba maslahi ya watu wetu
waliokatishwa tamaa na uongozi fisadi na mbovu.
Hawa wanaosema eti nchi za magharibi
zinatuchonganisha ili amani itoweke wauze silaha wanashindwa kutwambia ni
kwanini nchi hizi hizi za magharibi zinapotoa fedha ya kuendesha serikali yetu
kwa zaidi ya aslimia 40 hauwi uchonganishi.Wakitupa fedha ya kuendesha serikali
yetu fisadi hatulalamiki
Kama hatutaki
uhusiano nao basi tujitegemee.
Pia wanashindwa kusema kama hizi nchi
ambazo si za kimagharibi hazituchonganishi. Bahati mbaya hazichangii hata
bajeti ya serikali yetu mzigo
China
wanatuibia hata pembe za ndovu na kutujazia wasaka riziki. Hata wanyama wetu
waliopotoroshwa kwenda kwenye nchi za kiarabu hakuna aliyeliona hili na
kulipigia kelele. Tunajenga tabaka la viongozi wa aina gani ambao wanataka
kutumanisha katika uongo ili tusiuone na kuufanyia kazi ukweli? Ni bahati mbaya
sana walipoimbiwa wanyama wetu hakuna hata moja iliyopinga ujambazi huu.
Kwanini
tunakubali kuchonganishwa? Je tunachonganishwa au tunajichonganisha,
kuchonganishana wenyewe na kutafuta maadui wa bandia ili kupata namna ya kuzoa
wafuasi?
Nadhani
hakuna kitu kinatuchonganisha na kitatuchonganisha sana kama taifa kama ufisadi
ambapo kikundi kidogo cha watu kinawaibia wengi na kutajirika huku wao wakiendelea
kuwa maskini wa kutupa. Bila kuwabana hawa na kuwawajibisha, hizi mbinu zote za
kutaka kutengeneza maadui wa bandia hazitafuta dafu. Tunachonganishana sisi kwa
sisi yaani baina ya mafisadi na waathirika wa ufisadi. Hili ndilo tatizo na
sababu itakayoondoa amani ambayo nayo si amani chochote kwa vile hakuna haki. Huwezi
kuwa na amani bila kuwa na haki. Huwezi kuwa na amani sambamba na ufisadi. Lazima
uchague moja, amani au vurugu tokana na kushindwa kupambana na ufisadi. Haiwezekani
wezi wanaoibuliwa kila siku waendelee kutanua wakitukoga na kutufungulia kesi
kila siku nchi ikawa na amani. Ni bahati mbaya sana kuwa hata wakubwa zetu wa
kiroho hawakemei zaidi yaw engine kuwa washirika wakubwa wa mafisadi kama
ilivyogundulika kuwa maaskofu wawili waandamizi walikatiwa fedha ya escrow.
Cha msingi
kwa viongozi wetu wa kiroho ni kuacha kulala kitanda kimoja na viongozi
mafisadi. Kwanini kuweka nchi zote
kwenye kapu moja kama si ujinga? Hivi kitendo cha Uswizi kutuambia kuwa kuna
wakubwa zetu mafisadi, wezi, wachoyo na wenye roho mbaya walioiba fedha yetu na
kuificha huko serikali ikajifanya haisikii ili watu wake wasiumbuke nacho ni
uchonganishi? Kama ni uchonganishi basi ni mzuri.
Tumalizie kwa
kuwataka wote wanaoamini kuwa tunachonganishwa na nchi za magharibi ambazo
zimekuwa zikifadhili serikali yetu wawe wakweli na kuliangalia tatizo halisi
badala ya kutengeneza maadui bandia. Nchi za magharibi zikiacha kuifadhili
serikali yetu nchi haitakarika. Kama huu ni uchonganishi basi ni mzuri.
Chanzo: Dira
No comments:
Post a Comment