How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 28 April 2015

Mauaji ya albino tuige mfano wa Malawi


        Hivi karibuni serikali nchini Malawi imetangaza hatua za kimapinduzi dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Baada ya kukamatwa wahalifu wenye viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi, serikali imeamuru jeshi la polisi nchini mle kuwapiga risasi watakaokutwa na viungo vya binadamu. Japa wengi wanaweza kuona kuwa hatua hii ni ukiukwaji mkubwa wa haki za bindamu, inabidi wajiulize. Ni binadamu yupi anastahili haki za binadamu kati ya wahanga na wahalifu wanaowawinda na kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi.
Kimsingi, mtu anayewinda, kuua, kumilki, kusafirisha, kuuza na kununua viungo vya binadamu mwenzake si binadamu tena. Hivyo, jinai hii inamuondolea haki za binadamu kutokana na kutenda kinyume na ubinadamu. Siku zote haki huandamana na wajibu. Yeyote anaposhindwa kutimiza wajibu wa kibinadamu, anaondokewa na haki ya kuwa au kufaidi haki za binadamu.
Tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Malawi si kubwa kama ilivyo Tanzania ambayo inasifika kuwa chanzo cha kadhia hii ya kishenzi na kinyama. Pamoja na udogo wa tatizo, mamlaka nchini Malawi zimeonyesha nia na utashi wa kupambana na tatizo hili hasa kulikomesha. Hii maana yake ni kwamba sisi Tanzania tumezembea. Je kwanini Malawi wamechukua hatua hii ambayo kwa serikali huwa mara nyingi si rahisi kuichukua tena ndani ya muda mfupi?
Kwanza, wanajali haki za binadamu ambapo uhai ni haki kubwa ya binadamu kuliko zote. Pili, wanawajali raia wao kiasi cha kuwa tayari kujiweka kwenye nafasi ya kulaumiwa kwa kuchukua hatua kali hivyo. Tatu wanajua madhara kwa watu binafsi na taifa yatokanayo na mauaji haya ya kinyama na kishenzi yatokanayo na ujinga, roho mbaya, ushirikina na tamaa ya utajiri wa haraka tena bila kutumia maarifa wala kufanya kazi halali. Nne, wanajua madhara ya kadhia hii kwa sifa ya taifa. Malawi ina mottoisemayo kuwa Malawi is warm heart of Africa. hawapendi sifa hii ichafuliwe na yeyote. Na anayejaribu kuichafua havumiliki na serikali itatumia mbinu na sheria yoyote kuhakikisha hili halifanyiki. Je Tanzania sisi motto yetu ni ipi? Kusema ukweli sijui kama tuna kauli mbiu au motto ya kutangaza taifa letu ambalo limegeuka kusanyiko la watu wa hovyo, mafisadi, wezi, majambazi, wauaji, waongo, wanafiki na wababaishaji.
Maana ukiangalia tangu mauaji haya yaanze na hatua ambazo serikali ya Tanzania imechukua, unagundua uhovyo na ukatili wetu kitaifa na sasa kimataifa kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kusambaa nchi jirani. Malawi ni taifa la pili jinai kukumbwa na kashfa hii ya “kitanzania”. Nchini Burundi vimewahi kuripotiwa vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Shirika la habari la Reuters likikariri taarifa ya Umoja wa mataifa limeripoti kuwa watu wapatao 15 ima wameuawa au kushambuliwa ndani ya  mitatu katika nchi za Burundi, Malawi na Tanzania. Hii si idadi ndogo hata kama ingekuwa ya faru au tembo. Hii si idadi ya watu tu bali watu waliopoteza maisha kwenye mikono ya wanyama waitwao binadamu wenye tamaa ya kutajirika hata kwa kukatiza uhai wa wenzao bila hatia. Malawi imeamua kupambana na tatizo bila kusita wala kificho kwa kuutangazia ulimwengu kuwa itawapiga risasi watakaokutikana na hatia hii ya kuua, kumilki, kusafirisha, kuuuza na kununua viungu vya binadamu. Mkuu wa jeshi la polisi nchini Malawi, Lexen Kachama alikaririwa akitoa amri kuwa askari, “wapige risasi, wahalifu hatari watakapobainika kuwateka watu wenye ulemavu wa ngozi.” Reuters inaripoti kuwa tangu mwaka huu kuanza, watu wenye ulemavu wa ngozi wapatao 10 wameishauawa nchini Malawi. Kachama aliongeza kusema, “Hatuwezi kuangalia tu wakati rafiki zetu wenye ulemavu wa ngozi wakiuawa. Tumegudua kuwa wahalifu hawa ni katili na hawana huruma hivyo washughulikiwe hivyo hivyo.” Kwa maana nyingine, Malawi imeamua kutumia sheria ya jino kwa jino na dawa ya moto ni moto. Wakati mwingine tunahitaji kukabili baadhi ya matatizo kulingana na uhalisia wake. Waingereza husema, “Extraordinary problems need extraordinary solutions” yaani matatizo yasiyo ya kawaida uhitaji suluhu zisizo za kawaida.
Kama tutakuwa makini na wakweli kama taifa, basi mauaji katili na ya kinyama ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi yanapaswa kushughulikiwa bila huruma kama ilivyotangazwa nchini Malawi. Hatua iliyochukuliwa na Malawi –pamoja na utata wake kwenye macho ya watetezi wa haki za binadamu –ni ya kuigwa hasa ikizingatiwa kuwa wauawaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi ni katili na wasio na utu. Hivyo, tunapowashughulikia tunapaswa kuweka utu pembeni.
Tumalizie kwa kuitaka serikali ya Tanzania ichukue hatua kama hizi ambazo zinaonekana na kuingia akilini badala ya siasa na usanii wa kuwaita viongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi ikulu na kupiga picha nao huku wakiendelea kuangamia. Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanahitaji ujasiri na utashi wa hali ya juu unaozingatia thamani na haki za binadamu. Tanzania isipobadili mbinu yake ya kupambana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, basi wana harakati za haki za binadamu waifungulie mashtaka kwenye mahakama ya jinai ya kimataifa ili iweze kuwajibishwa iwalinde raia wake dhidi ya wauaji wasio na huruma wala utu.
 chanzo: Tanzania Daima Aprili 29, 2015.

4 comments:

Anonymous said...

Wateja ni nani? Je wateja wanaweza kushughulikiwa?

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon swali lako zuri. Wateja wanashughulikiwa maana wote wanavunja sheria. Hata hivyo kama ni wazito serikalini ambao wanaaminika kwa ushirikina wao itakuwa vigumu kidogo.

Anonymous said...

Kwa msingi huo biashara hiyo hawezi kufa kwa sababu wateja wanayo pesa haramu kwa kufanya vitendo haramu pia vya kishetani na huku wakiwa wanapindisha sheria kujilinda hivyo ni sawa kuchimba kisima na kuhamisha maji bahari yote kwa kutumia kisima ulichochimba huku nchi kavu!!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemayo ni kweli. Nadhani unaweza kupata jibu sahihi tokana na madai ya rais Kikwete kuwa ana orodha ya mafisadi, wauza unga, majambazi na wahalifu wengine. Je ni kitu gani kimefanya asiwashughulikie? Wenzetu wa Malawi wako wazi kuwa mauaji ya mazeruzeru hayakubaliki. Finish.Piga risasi yoyote utakayemkamata na ushahidi wa kutosha ili asipoteze muda wa magereza, mahakama, fedha za walipa kodi na upuuzi mwingine. Je Kikwete alifanyaje? Waite ikulu upige nao picha wakitoka nje waendelee kuteketezwa. Isitoshe anajulikana kwa usanii wake. Anasema hili anafanya lile. Waingereza husema you preach water and drink wine.