How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 3 April 2015

Rais ajaye asitokane na chochote ila….


          Harakati za kumsaka mrithi wa rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake Oktoba mwaka huu zimeiva. Tumeshuhudia na kusikia wengi wajinadi na kutangaza nia ya kuwania urais. Tumeshuhudia wanaofaa na wasiofaa wakipigana vikumbo kutangaza nia – wengine bila ya hata sera wala sifa – ili mradi kila mwenye kusaka ulaji huu wa juu na wa dezo anajitahidi kutuaminisha kuwa ndiye anafaa.
          Kutangaza nia wala kutaka kugombea urais si jambo baya ingawa kwa staili tunayokwenda nayo ambapo urais na ubunge vimegeuka biashara yenye kuingiza utajiri haraka, tunapaswa kuwa makini ten asana. Wapo wanaojinadi kwa umri wao na wengine hata mitandao yao. Kila mtu anatumiam binu yake ilmradi lake liwe hata kama hana sifa wala stahiki. Hivi karibuni rais Kikwete alitoa matamko makuu mawili yaliyowastua wengi na kuwahangaisha wachambuzi wa mambo katika kupima na kutafuta anachomaanisha au kutaka katika kinyang’anyiro cha kumsaka mrithi wake. Alikaririwa akisema, “Wapo watu wenye sifa zote za urais lakini hawajitokezi na hata wakiambiwa kuwa wanaweza husema kuwa hawajajiandaa. Hawa ndiyo tunaowahitaji kwa kuwa wanahitaji kukumbushwa.”  Kikwete aliyasema haya mjini Songea akihutubia wakati wa kilele cha maadhimisho ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutimiza miaka 38. Ni bahati mbaya kuwa rais hakuwataja hao wenye sifa wake wanaongoja kubembelezwa na kuombwa utadhani hawajui wapi zinachukuliwa fomu. Wapo waliodhani kuwa Kikwete ana mtu wake anayemuunga mkono ambaye angetaka amrithi baada ya kutoridhishwa na makada wa chama chake waliokwisha kujitokeza kutangaza nia. Kimsingi, Kikwete aliacha swali moja kuu: Nani huyo anayemtaka Kikwete na ili iweje?
          Baada ya muda kidogo, kikwete hakuishia hapo. Kwani alikaririwa akisema, “Kwangu mimi ninaamini wapo wanawake wenye sifa na uwezo mkubwa wa kuwania urais, hivi sasa wanawake mnaweza msirudi nyuma.” Aliyasema haya wakati akihutubia kilele cha maadhmisho ya siku ya wanawake mjini Morogo hivi karibuni. Kwa kiasi fulani –japo hakutaja jina –unaweza kusema kuwa anayetakiwa na Kikwete kumbe ni mwanamke. Vinginevyo, Kikwete atoe kauli nyingine ya kupingana na hili. Wachambuzi wa mambo walianza kukuna vichwa na kumsaka huyo mwanamke anayemtaka Kikwete. Kwa sifa zao sawa lakini si jinsia yao. Kwani tunatafuta rais au mchumba?
 Siku moja baada ya Kikwete kutoa tamko hili, baadhi ya magazeti yalipambwa na picha za wanawake wawili yaani Spika wa Bunge Anna Semamba Makinda na Dk Asha-Rose Migiro waziri wa Katiba na Sheria ambaye amekuwa akitajwa tajwa kuwa anaweza kuteuliwa na CCM ili kuwaengua makada wake fisadi wenye ushawishi chamani. Kama mtanzania yeyote, si vibaya kwa rais kuzungumzia mgombea ingawa hakutaja sifa wala jina la mhusika ili watanzania – hasa wapiga kura wampime kama anafaa au la.
          Kimsingi, tokana na kukithiri kwa ufisadi wa kimfumo chini ya CCM, mgombea toka CCM hafai. Kwani hana jipya. Nadhani Tanzania inataka rais mwenye sifa ya uchapakazi na usafi kimaadili na si rais atokanaye na jinsia yake. Hatutaki rais atokanaye na uke wala uume wake bali sifa nyingine za kiutendaji na kimaadili. Kwa hali iliyo sasa ambapo taifa limetekwa na ufisadi, itakuwa pigo la mwaka kwa watanzania wenye matumaini ya kubadili mfumo wa sasa kupandiziwa rais toka CCM. Kimsingi, kutokana na jinsi CCM ilivyochemsha na kuicha nchi iwe shamba la bibi, kuondokana na kadhia hii ni kupata rais toka nje ya CCM. CCM imechakaa, imechoka, imechusha na ni kama inakufa ukiachia mbali kuendelea kupumlia kwenye mashine. Kwani lazima CCM? Mbona kuna watanzania wenye sifa zote kwenye upinzani? Kwanini Tanzania iendelee kuwa taifa lenye sifa kama za jogoo ndege mjinga afugwaye anayesifika kwa kuimba wimbo mmoja ule ule miaka nenda miaka rudi? Kuna haja ya kuipumzisha CCM ili na wengine wachukue nafasi yake na kuonyesha ujuzi na uchungu wao kwa taifa. Nani anataka chama ambacho watani wake wamekipachika jina chafu la chama cha mafisadi?  Nani anataka chama kinachoonyesha wazi kupwaya kuisha na kuishiwa kulhali? Nani anataka chama kilichochoka na kutekwa na mafisadi wanaoamua ni kiasi gani kiibiwe na nani apewe mgao? Inatosha, CCM ipumzishwe lau itie adabu kama KANU, UNIP, MCC na vyama vingine vya namna hii vilivyotupwa nje ya madaraka vikafaa na kusahaulika.
          Chini ya CCM hasa baada ya kung’atuka Marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere, Tanzania iligeuka taifa la majaribio na la watu wa hovyo ambapo ufisadi, usafirishaji na uuzaji mihadarati, ujangali, ujinga, uvivu, majunga, rushwa, wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma, utoro na uzururaji wa viongozi wakuu, kulindana, kufadhiliana na kuhujumu taifa vimegeuka sera kuu ya CCM. Je chama cha namna hii – kinachotumia uwepo wake madarakani kuhudumia makada wake na marafiki na familia zao – kinahtajika kweli kuwa madarakani ili kuvurunde zaidi?  Kwa hiyo, tunaposema rais ajaye asitoke CCM tuna hoja tena yenye mashiko hasa kwa kuzingatia utendaji, historia ya CCM na hali ilivyo mbaya kwa sasa ambapo taifa letu linasifika kwa mambo ya hovyo kama vile kuombaomba na kukopakopa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ukiachia mbali madhambi yaliyotajwa hapo juu. Hata majirani zetu hawatuheshimu tena. Wengine wanadiriki hata kututukana sisi na rais wetu kwa vile wanajua tulivyo wa hovyo na tunavyofanya na kupenda mambo ya hovyo japo si wote.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

No comments: