The Chant of Savant

Saturday 11 April 2015

'Ufunuo: Walevi jihadharini na wachunaji'.

Tazama naona kaya inayoliwa kama karatasi mbele ya mchwa. Naona malaika mkuu akishuka na kusema nami akinitaka nipeleke habari hii njema kwa waja wake wanaodhulumiwa na wajinga na wahalifu waliojivika vyeo vikubwa na vitukufu wakifanya ukufu na makufuru ya kuwaibia na kuwaacha makapuku. Malaika anasema nami, “Nena usiogope Nabii wa Mungu Mlevi mwana wa Mvuta Bangi mjukuu wa mzee Fyatu wa Fyatua.
Tazama naona fisi, mbweha na chui waliovaa ngozi ya kondoo wakitangaza kutenda miujiza wakati si miujiza kitu bali mazingaombwe usanii na wizi wa mchana. Naona maiti waliovishwa vito vya thamani wakisimama mimbarini na kuhubiri neno wakati nyuma yake kumjeaa meno ya kuwararua kondoo wa Bwana kwa kudai wamtolee Bwana wakati wanaotolewa si Bwana bali mbwa hawa. Naona maiti wanaonuka na kuoza wakihuburi utukufu wakati ukweli ni kwamba wao ni wafu tena waliokufa zamani nyoyo zao zikiliwa na tamaa ya utajiri na ujambazi wa mchana uitwao usanii. Nawaona wakisema uongo mchana baada ya kujipachika utafiti wakidai wamesoma hata kutunga vitabu wakati ukweli ni kwamba wametunga uongo tokana na tamaa ujinga na upogo wao. 
Malaika alinionyesha kituko. Aliniambia, “Tazama wale wajinga na wapumbavu wanavyokamuliwa na hawa kupe waliojificha nyuma ya utukufu wakati ni utukutu na usanii mtupu. Tazama wanavyoshangilia wakiamini utapeli na upuuzi kana kwamba hawana ubongo wala akili. Tazama walivyo maskini wakimtajirisha matapeli wajisifuye kuwa wanazo wakati wanawaibia kwa sababu ya utapia mlo wa vichwa na roho zao. Leo mnaambiwa mpande mbegu. Kesho wataambiwa wamtolee Bwana kana kwamba Bwana ni maskini na anahitaji madafu yao. Kesho kutwa wapumbavu na vipofu hawa wataambiwa walete minofu na mifupa ya mazeruzeru na watafanya hivyo.”
Namuuliza Malaika. “Hii maana yake nini? Anajibu. “Hii ni kaya iliyotawaliwa na ujinga, upumbavu, uroho na roho mtakakitu ambapo wataka kitu hutumia roho mtakatifu kuwaibia watakakitu kwa kuwadangaya kuwa wana roho mtakatifu. Kwa ufupi ni kwamba kinachofanyika hapa ni wafu wawili kukokotana kila mfu akidhani atafikia malengo yake kwa kumtumia mwenzake ingawa unaweza kuona nani anawatumia kwa kuwala wenzake.”
Sikumuelewa malaika. Hivyo, niliuliza, “Kama wote wameoza na wanatumiana mbona kuna anayenufaika na wapo wanaoumia?” Malaika alijibu, “Umeona na kunena vyema. Fisi anawafaidi wanakondoo walioponzwa na ukondoo na upogo wao. Wanampa fedha anawapa ahadi. Wanamsikiliza hawasikilizi. Wanamuita kiongozi na mchungaji wasijue ni mchunaji. Hivyo, katika wafu hawa wawili wanaokokotana hakuna mwenye nafuu. Huyu anayewala wenzake ataliwa siku si nyingi. Akibanwa kidogo anazimia hata kuchanganyikiwa. Je siku akifanyiwa kweli itakuwaje?”
Baada ya kumaliza kuuliza, malaika aliinua macho yake juu na kusema maneno ambayo sikuyaelewa na kusema, “Basi nenda kwambie walevi kuwa wawe macho na matapeli wanaojivisha utukufu wakati si chochote bali utukutu na uroho na uchovyo kuwaibia maskini kwa jina la Bwana. Bwana ahitaji madafu yenu. Mnaliwa kwa jina la Bwana. Hakuna cha Bwana wala Bibi bali hao matapeli wenyewe.”
 Baada ya kuyasema hayo mbingu zilifunguka nikaona wadudu wa kutisha wakitoka kwenye mwili wa yule anayewahadaa wenzake kuwa anaweza kufanya miujiza wasijue ameoza na hana lolote bali kuwachezea mahepe. Nilimuona akipewa adhabu si ya kawaida. Akiwa ameshika ukuta akipewa maagizo na shetani kuendelea kuwakamua kondoo, aliinama kwa unyenyekevu akaendelea kupokea maagizo.
Ndipo malaika mkuu akasema, “Nenda kawambie walevi waache upumbavu. Wataliwa wanajiona na fisi anayeshikishwa ukuta na kutii kila upambavu ili kutimiza kiu ya upumbavu na ujinga wake.”
Alinigeukia na kusema, “Nenda kawambie walevi hivi, wapendwa walevi, kama mtajiamini na kuchukua tahadhari hamtachunwa na mafisi na maiti waliojivisha utukufu wakiogelea kwenye ukwasi utokanao na ujinga na uvivu wenu wa kutegemea miujiza badala ya kuchapa kazi. Mnaamini rongorongo za nilifanya hiki na kile bila kutafuta ushahidi. Mtaendelea kuliwa na kugeuzwa majuha, kengeukeni kabla ya kuendelea kuingizwa mkenge.”
Tazama mbingu zinafunguka na wanatokea fisi na mbwa wanaojivisha utukufu wakijipa vyeo vitukufu. Wananuka, nyuso zao zinatisha na wakipumua inatoka harufu ya kutisha. Vifua vyao vinafunguka naona mioyo iliyooza ikitokwa na wadudu kila aina. Harufu itokayo humo inafanya nikaribie kuzimia.  Namgeukia malaika mkuu na kusema, “Nini maana ya haya?” Anasema. “Harufu ni alama ya uongo na uoza ni alama ya ufisadi.  Nyuso ni alama ya kinachowangojea siku yao ikitimu. Kutoa harufu ya kutisha nyoyo zao ni alama ya wasi wasi presha na mfadhaiko wanaoupata baada ya kutoka kwenye mimbari wakihubiri utapeli na ujinga wao.
Baada ya kujibu maswali yangu mara mbingu zinafunguka tena. Naona majina yakipita kwenye ubao mkubwa ung’aao mithili ya uso wa kompyuta.
Jina la kwanza, Jose Gwaijimama.
Jina la pili, Zek Katortoise.
Jina la tatu, Gettie Rwakatarehehehehee.
Jina la nne, Tony Lusesekesekelo.
Jina la tano, Silvessiee Gamanyanyua
Jina la sita, Chrisie Mwakasengeeee.
Majina ya mbweha wala kondoo yakiwa yanaendelea kumiminika, ghafla nilijikuta peke yangu nikitokwa na jasho.

Huo ndiyo unabii kwa walevi toka kwa nabii mwenyewe aliyesalia kuwaonya na kuwaokoa walevi waliwa, wadhalilishwa na watapeliwa. Tieni akilini mtaendela kuliwa mkijiona mkiwatajirisha matapeli huku mkiendelea kuwa makapuku. Shikeni maneno ya utabiri huu uokoke vinginevyo utapigwa.
Chanzo: Nipashe April 11, 2015.

No comments: