The Chant of Savant

Tuesday 21 April 2015

Kama mali za Gwajima ni halali, anahofu nini?

          Askofu wa kujipachika Josephat Gwajima amevutia vyombo vya habari kwa siku za karibuni. Ni baada ya kwanza, kushutumiwa kumchukua mwimbaji wa nyimbo za injili Flora Mbasha ambaye mumewe wa zamani Emanuel Mbasha anamtuhumu Gwajima kumwiba mkewe. Kabla ya hili kupoa lilizuka jingine la Gwajima kumrushia matusi Askofu mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Polycarp Pengo kiasi cha kuitwa polisi kutoa maelezo. Kana kwamba hii haitoshi, Gwajima alipofika polisi akitegemea kutoa maelezo juu ya kashfa na matusi, alijikuta akitakiwa kueleza alivyochuma utajiri wake wenye kutia shaka na wa haraka.
Tokana na na kutakiwa kueleza utajiri wake alivyoupata, Gwajima anaona kama anaonewa wivu tu akidai yeye ni “maskini” ingawa si maskini wa kawaida. Alikaririwa hivi karibuni akisema, “Wanaodai mimi ni tajiri wana wivu tu na wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini kama walivyo masikini wengine. Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu wakiwa matajiri, siwezi kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini, nitatajirika pamoja nao.”
Je ni kweli kuwa Gwajima si tajiri kwa kiwango chochote hata kwa nchi tajiri duniani kama Marekani? Jibu linapatikana tokana na utajiri anaosema ni umaskini alio nao Gwajima. Alikaririwa akisema, “Wanaodai mimi ni tajiri wana wivu tu na wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini kama walivyo masikini wengine. Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu wakiwa matajiri, siwezi kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini, nitatajirika pamoja nao.”
Je mtu mwenye kuweza kuwanunulia wenzake magari yapatayo 40 kweli ni maskini huyu? Je kama ameweza kuwanunulia wenzake magari yeye amejibakizia utajiri kiasi gani na ameupata vipi na kwa muda gani? Jibu utalipata tokana na utajiri wa Gwajima ambao umetajwa kuwa ni majumba, magari ya starehe na juu ya yote helkopta. Kwa Tanzania na afrika, kwa mtu mwenye kumilki helkopta si tajiri tu bali tajiri wa kutisha. Kuwa tajiri si dhambi kama mhusika amepata utajiri wake kihalali. Hata hivyo, inatia shaka tokana na kazi anayofanya Gwajima ambayo kimsingi, si ya kuzalisha bali kutoa huduma. Hata yule anayesema kumhubiri, Yesu Kristo hakuwa tajiri na aliuchukia utajiri. Methali 28:20 imeweka wazi kukwa “Mtu mwaminifu atapata baraka tele, lakini mwenye pupa ya kuwa tajiri hataepa adhabu.” Je utajiri wa Gwajima ameupata baada ya muda gani na kwa kufanya nini? Na kwanini anapoulizwa siri ya utajiri wake anang’aka kama hakuna namna? Ni muhimu kumshauri Gwajima kuwa asipoteze muda kutunishiana misuli na serikali hadi kumpa shinikizo rais kuwazuia polisi kufanya kazi yao. Mtu wa namna hii anaonekana kutojua afanyacho hasa ikizingatiwa kuwa, japo serikali imemnyazia kwa muda mrefu, si kwamba haijui mchezo wake.
Kwa mtu ambaye hana wasi wasi na utajiri wake na jinsi ulivyopatikana, alipoitwa na polisi alipaswa kutoa maelezo na vielelezo na kuruhusiwa kwenda nyumbani badala ya kusimama mimbarini na kuanza kutishia na kulaumu watu wanaotekeleza wajibu wao. Tanzania haiwezi kuendelea kuwa shamba la bibi ambapo wachumia tumbo wachache wanawaibia watu wetu kwa kuwadanganya na miujizi na ujinga mwingine. Serikali inapaswa kuwachukulia wote wanaotia shaka hasa wachungaji na maaskofu wa kujipachika vyeo ili kuwaibia wajinga na maskini kama ilivyoanza kuzoeleka. Hatuwezi kuendelea na jinai kama hii. Huu nao ni ufisadi wa kutumia dini kuwaibia wajinga na maskini waliokata tamaa nchini. Serikali inapaswa kuingilia kati kupambana na wachungaji wachunaji ambao hawana tofauti na matapeli na waganga wa kienyeji wanaopotosha na kuiibia jamii. Hakuna miujiza katika kufanikiwa au kutatua matatizo yoyote yawayo. Ni wajinga waliokata tamaa wanaoweza kuendelea kugeuzwa mabunga kwa kushawishika kutoa kidogo walicho nacho kuwapa matapeli wanaochezea akili zao. Kazi ya serikali ni kuhakikisha hakuna mtu anayemnyonya mwenzie hata kama mnyonywaji ameihiari tokana na ujinga na kukata tamaa kwake.
Kuna haja ya kuwachunguza hawa viongozi wa kiroho wanaojipachika vyeo vikubwa kama askofu, mitume na wachungaji wakati hawana sifa zaidi ya kusaka fedha. Mwishoni mwa mwaka jana nchini Kenya aligundulika tapeli wa namna hii aliyejipa uchungaji, uaskofu, utume na udaktari aitwaye Victor Kanyari ambaye alikuwa akitumia radio na runinga kulaghai watu kuwa anatenda miujiza wakati waliokuwa wakitoa ushuhuda walikuwa matapeli wenzake wa kupanga. Hali imekithiri nchini Nigeria na hata Zimbabwe ambapo matapeli wenye majoho wameweza kuwaibia waumini wao huku wakikwepa kulipa kodi na kutokea kuwa matajiri wa kutisha ndani ya muda mfupi. Hii ni aina mpya ya wizi inayoshika kasi barani Afrika ambapo watu wengi licha ya kuwa wajinga, wamekata tamaa kiasi cha kupwakia kila uongo kwa imani kuwa wanaweza kuboresha maisha yao.
Tumalizie kwa kuzitaka mamlaka kumbana Gwajima aeleze alivyopata utajiri wake kwa haraka hivi. Si yeye tu bali wote wenye utajiri wa kutia shaka ilmradi wasifanye hivyo kumkomesha kwa sababu za kisiasa. Akishindwa kufanya hivyo, ataifishwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ili liwe somo kwa wengine wanaotumia ujinga na umaskini wa watu wetu kujitajirisha kinyume cha sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 22, 2015.

3 comments:

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,Bwana Mola azidi kukulinda kwani kalmu yako imekua ni silaha ya kuwatetetea wanyonge daima,lakini tatizo kubwa ni ni kuingiliana kwa maradhi sugu katika jamii ya ulimwengu watu hususa Sub Sahara Afrika ambapo kila aina ya maradhi ya kumfanya mwanadamu adumae kiakili yanazidi kujizatiti nakusudia hapa UMASIKINI na UJINGA na kama ujuavyo umasikini na ujinga ndio mama wa mabalaa yote ya maradhi ya kijamii katika jamii yoyote ile ile duniani na wakati mwingine uwezi kuamini kwa vile maradhi haya yamejikita basi hata wale wenye elimu ya aina moja au nyingine utakutwa wamedhurika na maradhi hayo ebu angalia hawa waumini ambao wanaowatajirisha hawa mbwa mwitu ambao wamevaa ngozi ya kondoo,utawakuta ni wenye elimu zao na vyeo vyao katika serikali na sekta binafsi ambao wanakuja na mavazi ya fahari,magari makubwa makubwa ya fahari na hata michango yao ni mikubwa mikubwa wakiamini kwamba watakuwa na sehemu kubwa katika maisha ya mbinguni.
Kama tulikoloniwa kwa sababu ya ujinga wetu,umasikini wetu na ukarimu wetu leo hii tnakoloniwa na hawa matapeli wanaodai wana miujiza ya kuwafanyia waumini wao ambao wengi wao ni masikini kuliko maelezo.
Mwalimu Mhango tuna safari ndefu sana ya kuweza kupambana na maradhi haya ya kijamii na watu wa aina hii ambao wametoa makucha yao na bila ya huruma kuwaparura wafuasi wao bila ya kujali muda wa kudumu tu wao wanafaidika na wanazidi kufaidika.
NI kweli kabisa kama ulivyoandika kwamba..."Hakuna miujiza katika kufanikiwa au kutatua matatizo yoyote yawayo"maelezo yako haya ni ya kielimu(sayansi) lakini katika jamii ambayo imetawaliwa na ujinga,umasikini na uchawi maelezo haya yanakosa maana kabisa.kwa nini wajanja hawa wategemee katika mahubiri yao au dini yao miiujiza?kwa nini wasiende makaburini kuwafufua wafu arudi duniani na kwenda makanisani mwao ili kuwahakikishia waumini kwamba haya wanayohubiri hawa matapeli ni ukweli mtupu?Bwana Yesu alikuwa anafufua wafu.Kwa nini wasiende katika hospitali za ukoma wakawaponya watagonjwa kama alivyokuwa akifanya Bwana Yesu?kwa nini wasiende shule za vipofu viziwi na mabubu wakawafanye miujiza huko kama alivyokuwa akifanya Bwana yesu?Bwana Yesu alikuwa asubiri kuifanya miujiza yake katika kanisa japo yeye alikua akihubiri na kusali katika nyumba ya kiibada ya kiyahudi (synagogue)Bwana Yesu popote pale ilpohitajika au kuhitajika kufanya miujiza yeye aliwajibika tu bila ya lkusita,lakini hawa matapeli na utapeli wao upo wazi wanafanya miujiza yao makanisani mwao kwa kutumia uchawi,kupanga watu ambao wanakula na kanisa na viini macho.
Mwalimu Mhango sisi bado tupo katika stage ya jamii ya ki primitive na mihimili muhimu ya jamii hiyo ni uchawi,wachawi makuhani,na watu wa dini na kwa bahati mbaya hali hiyo bado inaendelea na itaendelea afrika mpaka dunia kwisha.
Msemo wa Karl Marx hapa una uzito wake "Religion is the opium of the masses."
Mwalimu Mhango ni serikali gani hiyo ambayo unayoikusudia kuwachukulia hatua watu wapuuzi kama hawa?ikiwa serikali inashindwa au inakataa kwa makusudi kuwachukulia hatua viongozi ambao wamebobea katika machafu ya ufisadi unaonuka kaya nzima leo itawachukulia hatua matapeli wa kiroho?Unajua nini nachoongea hapa Mwalimu Mhango.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon nimevutiwa na mchango wako hadi kuutundika kama post ili wengi wasome na kunufaika kama ambavyo nimenufaika. Karibu tena na tena na uje na michango minono na tekenyeshi kama hiyo.

Anonymous said...

Tupo pamoja Mwalimu Mhango,najuwa wazi kwamba tuna safari ndefu lakini wahenga walisema safari ndefu huwazwa na hatua moja,na wewe umeshaanza hatua hiyo.Mwalimu Mhango tunahitaji watu kama nyinyi katika jamii yetu ambayo wapo tayari kujitolea muhanga wa maisha yao na bila kuogopa lawama za wapiga madebe ambao hawalali mchango wako ni mkubwa sana na utabaki kwa kizazi kijacho kuchota kwa kiu kikubwa kusaidia muelekeo wao na maendeleo yao ya maisha.amini usiamini mwalimu Mhango kuna wengine wanakutamani kwamba ungejiunga nao katika ufisadi na kufisidisha kuliko kupoteza wakati wako kwa kuwaelimisha ambao wasiostahiki kuelimishwa amini usiamini lkn hiyo ndo dhana yangu nzito.Bwana Mungu akulinde daima.