Mwenzenu nina hasira kiasi cha kutamani kumyotoa mtu roho kama si kujinyotoa. Nimejaribu kupata kidogo lau hasira ziondoke bila mafanikio. Hivyo, nimeamua kutoa hasira zangu kwa kuwaasa walevi kuwa makini na baadhi ya rongorongo na matamko ya wajivuni na walevi wa ulaji wanaowafanya walevi hamnazo kama wao.
Hata kama tunalewa sana, bado tuna akili hata kama ni za kilevi. Hata hivyo, nani si mlevi katika kaya hii ambapo ulevi uwe wa mali, ngono, vitu, siasa, dini na hata bingi ni dili? Kujua tulivyo kaya ya walevi, hebu angalia tunavyowekeza kwenye baa, glosari na chap-chap Guest Houses badala ya shule kiasi cha majirani zetu kutuchuna kwa kupeleka vitegemezi vyetu kule baada ya akina dk Shchool Kawadog kudedisha ilm kayani.
Si juzi msanii mkuu akaja na mpya akisema eti urahisi ni mgumu wakati ni rahisi. Akiwa kwenye kaya ya Joji Kichaka alisema eti ulaji kwake ni kibarua kigumu. Tangu lini kupe akaona ugumu wa kumfyonza damu ng’ombe kama siyo umbea na kiherehere? Ni lini mpanda farasi akaona machungu ya farasi kama siyo umbea na unafiki wa kizamani? Kweli ukishangaa ya Mlevi utaona ya Njaa Kaya! Urahisi ungekuwa rahisi vilaza kama yule ungekaa muda wote huo?
Kweli, zama za mzee Nchonga urahisi ulikuwa mgumu kweli. Maana kuweka msingi wa kaya iliyokuwa imebanjuliwa na mkoloni wa Kitasha haikuwa kazi rahisi. Ilihitaji visheni, kujikana na uadilifu vya hali ya juu. Ila sasa –ambapo patakatifu pa patakatifu pamegeuka pango la mafisi, wezi na vinyangarika kuibia kaya –urahisi ni rahisi sana tu. Ni kula dezo. Ukiwa rahisi unahakikisha na kila kinachokuhusu kuanzia nkeo, vitegemezi, marafiki, waramba makalio hata mbwa wako nao wanakuwa marahisi kwa namna yake.
Ukiwa rahisi unahakikisha bi mkubwa anaunda kampuni yake ya ulaji na kuipa jina zuri la NGO yaani Nahomola kwa Ghamu nyinyi Ombolezeni. Vitegemezi na ndugu zako nao wanapata ulaji kwa staili kwa kutumia jina lako. Ukiwa rahisi kwa sasa unakula matunda ya mzee Nchonga bila hata kujali wala kushukuru. Unaita washikaji zako mnakula kwa mikono na miguu tena bila kunawa. You just take a dip in gravy train. Mnakula kila kitu bila kujali kama kuna kesho. Unawabinafsisha walevi na mali zao. Wakifurukuta na kutaka kubadili katiba unaipiga chini ili kesho usinonihino kwenye debe kule Ukonga au Segerea. Wakitokea wabishi kutaka kukuzuia unawatumia akina Makondakonda wawakondeshe kwa vitisho.
Ukiwa rahisi wa kaya ya vipofu, mataahira na wasahaulifu unatanua kama huna akili nzuri. Wanaishia kulalama wasichukue hatua kukubughudhi wala kukuzuia. Unaizunguka dunia hadi wanakupa jina la kireno, Vasco da Gama yule jambazi aliyeizunguka dunia akifanya uchafu wake ambao matokeo yake ni ukoloni.
Jamaa aliposema eti urahisi na ulaji ni mgumu nilitamani kumramba mlevi vibao lau atie akilini. Hata hivyo, sikuweza. Amejizungushia mabaunsa kibao ili kumlinda walevi wasimdhulu baada ya kuwadhulumu kwa mvua kumi. Unadhani urahisi ungekuwa mgumu kama wakati wa mzee Nchonga wezi wa escrow, Kagoda, Richmonduli na EpA wangeendelea kutukoga na kupiga dili? Thubutu kama Nchonga hajakusweka lupango na walaji wenzako! Jamaa alikuwa tafu. Nani angemweka mfukoni au kumtumia kama kikaragosi kama tulivyoona kwenye escrew ambapo majambazi na wahalifu wamewatumia wanene wetu kutumaliza bila hata kukaripiwa? Nani anahoji kitakachofuatia hasa baada ya kuona watuhumiwa wakuu wakiendelea kutesa huku walevi wakiteseka? Weshasahau walevi wa kaya hii ya Danganyika aka Bongolalaland. Msikwe wapi mstuke yarabi? Walevi ni watu wa ajabu hata kama hawana nkia. Unaweza kuwauza hata mamsahibs na maza wao wasikufanye kitu. Unaweza kuwatia madole machoni na kila sehemu wasistuke!
Mzee Nchonga kuachia ngazi walikuja kila aina ya vinyamkera viherehere na majambazi wakavuruga mema yake yote. Walianzisha kila aina ya ujambazi, “ruxa”, “uongo na ufichi” na “usanii na matanuzi” na kuharibu sifa njema ya kaya. We miss you mzee Nchonga. Hivi urahisi ungekuwa mgumu tungeshuhudia kila jambazi akiutaka kwa udi na uvumba? Jamaa angewachafua wenzake kwa kutumia makanjanja na nyemelezi ili aupate? Who is fooling who hither? Mijitu mingine hata haikui. Unataka kumdanganya nani unayedhani ni taahira kudai kuwa ulaji wa dezo ni mgumu?
Kwenye kaya ya walevi, mataahira na wasahaulifu hata bata anaweza kuwa rahisi akakalia kiti kitakatifu na kukinyea na asiwepo wa kumtolea uvivu na kumchinjilia mbali. Hata chizi anaweza kuwa rahisi na asifanywe kitu tokana na mfumo wa kijambazi kayani. Waulize akina Rugemalayer, Singasinga, Andy Chenga, Prof Saucepie Muongo, Anna Kajuamlo, RostaTamu la Aziz, na majambazi wengine kama urahisi ni mgumu. Wanamtumia rahisi wanafanya kila ujambazi mbuzi na hakuna anayewagusa.
Urahisi ungekuwa mgumu walevi wangeendelea kuwa watazamaji wakati kaya yao ikibakwa na kuchafuliwa na kila kinyamkera kinachotumia ukaribu wake na rahisi? Kufuru za huyu mjivuni mkuu zilinikumbusha mwenzake asifikaye kwa kuwauza walevi kwa wachukuaji aka wawekaji wakati hawaweki kitu zaidi ya kuchuku akila kitu. Hasira zinanipanda nikikumbuka marehemu NBC, Tanisco na Air Tanzia ambao waliouawa na huyu kidhabi na mjivuni. Nimekumbuka Loliyondo iliyouzwa na kidhabi aliyemtangulia chini ya ujambazi ulioitwa kula bila kunawa ruksa. Nalilia njuluku anazolipwa jambazi mmoja wa Richmonduli anayelipwa eti kwa kustaafu wakati alitimka tokana na ufisi na ufisadi. Huenda kuweza kuruhusu madudu kama haya ndiyo kulimfanya mjivuni mkuu kusema kuwa urahisi ni mgumu. Nadhani kama ni mwenye kujisuta, ugumu wa urahisi uko moyoni mwake ambapo akikumbuka madhambi aliyowatendea walevi anakosa usingizi. Huenda ugumu wake ni kupambana na magonjwa ya ajabu ajabu ambayo pamoja na kuzunguka kila mahali hayaponi. Heri Aliyejuu atulipie sisi walevi tulioshindwa kumtolea uvivu huyu kidhabi na wenzake wanaoendelea kutukoga kwa kulipana njuluku zetu.
Chanzo: Nipashe Aprili 18, 2015.
No comments:
Post a Comment