The Chant of Savant

Friday 17 April 2015

Kwanini Kinana anaendelea kuhadaa umma?




  
       Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana ni kiongozi mwenye kutatanisha tokana na matamshi yake na mapenzi ya kupigwa picha kwa kila anachofanya hata kama ni cha kawaida. Siku hizi imekuwa kama fasheni kumuona Kinana kwenye picha akijionyesha kama kiongozi aliyeko karibu na wananchi na mwenye uchungu na hamasa ya kujenga taifa. Hata hivyo, wengi wanashangaa na kuuliza: Ni kwanini sasa kuelekea uchaguzi? Kadhalika Kinana si mtu wa kuishiwa vituko, mizengwe hata vitu ambavyo kidogo huwa vigumu kuviamini achilia mbali kuvielewa.

Hivi karibuni Kinana alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Wananchi wanakaa na hofu kwa muda wote wakati serikali haiwalipi haki zao wala kuwapelekea maendeleo na matokeo yake wanaishia kudhulumiwa.” Kinana alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Ngaramtoni Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha.  Inashangaza sana kuona Kinana ambaye chama chake ndicho tawala akisema vitu hivi kwa wananchi badala ya kumwambia rais au watendaji wengine katika serikali yao. Anachofanya Kinana ni sawa na mtu kujisuta asijue anafanya hivyo. Mbona ana nafasi ya kuonana na rais kila mara? Je huku si kuwahadaa wananchi wamuone kama anawajali wakati anawachuuza na kuwageuza majuha? Kwani huyo aliyechelewesha fidia ya hao wananchi ni nani zaidi ya serikali ya CCM?
Kwa maneno rahisi, kauli ya Kinana licha ya kuonyesha kushindwa kwa serikali yake ni ushahidi wa kushindwa tena vibaya sana. Litakuwa jambo la ajabu kama wananchi watamwamini badala ya kumshuku hata kumhoji alikuwa wapi wakati serikali yake ikiwatosa. Kama analenga kuwahadaa wapigie kura chama chake wajue fika uchaguzi ukiisha nao wamekwisha hadi miaka mitano ijayo. Ni juu yao kuchagua kuingia mkenge au kukengeuka.

Kinana alifichua sura yake halisi alipoonyesha wazi kuunga mkono mauji ambayo yamekuwa yakitekelezwa na jeshi la polisi kutokana na maagizo ya serikali yake. Alisema, “Mkishaanza kupigwa wanawakimbia, hata ukiangalia katika orodha ya waliouawa au kuumizwa majina ya familia zao hayapo.” Hapa aliwalenga viongozi wa upinzani. Kumbe Kinana alitaka viongozi wadhurike au ndiyo walikuwa walengwa wakuu? Hii inakatisha tamaa na kuudhi sana. Badala ya Kinana kuongelea haki za binadamu, utawala wa sheria, matumizi ya sheria kwa usawa anakuwa kama mwenzake waziri mkuu Mizengo Pinda aliyetoa amri kwa polisi wapige na kuumiza watu na wakafanya hivyo hadi kuua. Kwa matamshi kama haya Kinana na wenzake wanaonyesha fika wanavyoshabikia, kuamuru na kuchochea vurugu na uvunjaji wa sheria na haki za binadamu. Wengi wanashangaa. Wanawezaje kuongea sana bila hata kufikiria wala kuona aibu?  Hivi Kinana hajui kuwa polisi kupiga watu wanaotekeleza haki yao ya kikatiba ni kuvunja sheria na katiba au anahitaji asomeshwe hili?Alichosema Kinana ni matusi ya nguoni kwa watu waliofiwa na ndugu zao kwenye mauaji yaliyotekelezwa na polisi tokana na maagizo ya serikali ya CCM kutaka kuuzima na kuutisha upinzani bila mafanikio.

Kuonyesha viongozi wa CCM walivyo janga kwa taifa, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Onesmo Nangole ambaye wahanga wengi walitoka mkoani mwake akimpongeza Kinana badala ya kutetea haki za watu wake. Hata hivyo, atawateteaje wakati hawakuwa wana CCM? Nangole alisema, “Nakupongeza Katibu Mkuu, endelea kuibana serikali kwa sababu viongozi wamejisahau, kero ni nyingi zinahitaji ufumbuzi wa haraka. Vile vile ndani ya Chama kulikuwa na vurugu viongozi wa juu katika mikoa hawakuelewana ndiyo maana katika baadhi ya chaguzi tulianguka, lakini yote yamezikwa kutokana na ziara zako.” Nangole na Kinana ni wasanii wa kawaida. Kinana anaibana serikali gani wakati anatetea ukiukwaji wa haki za binadamu? Anaibanaje serikali wakati anaonyesha ubaguzi wa wazi utokanao na itikadi ya mtu? Kwake wapinzani hawana haki ya kufaidi haki za binadamu wala thamani. Kinana anaongea utadhani chama chake kinatawala nchi iliyofeli kama Somalia. Inasikitisha kuwa na viongozi kama hawa kwenye madaraka. Viongozi wabaguzi na wauaji tena wenye kupongezana kwenye jinai hii. Kuna haya ya wananchi kuwatolea uvivu viongozi wanaowachezea na kuwageuza majuha. Wanapaswa wasishikilie uanachama bali matatizo yanayowakumba bila kujali dini wala itikadi.

Viongozi wanaotumia ubaguzi wa kidini kutaka kuwavutia wananchi wanapaswa kuogopwa kama ukoma au magaidi. Wananachi wanapokumbwa na matatizo kama mfumko wa bei, ughali wa maisha, ukosefu wa usalama, tishio la mashambulizi ya kigaidi na umaskini wanaathirika kwa pamoja bila kujali itikadi. Hata matajiri wanapokuwa wakifaidi fedha zao wakisafiri kwa madege na kupeleka watoto wao nje kupata elimu nzuri ambayo CCM iliwanyima huwa hawajali itikadi bali uwezo wa kifedha. Hata watoto wao hucheza pamoja na kushirikiana bila kujali itikadi wala dini ya mtu. Ndiyo maana kwenye maeneo ya matajiri ya jiji la Dar es Salaam wanakoishi akina Kinana hakuna matawi ya wakereketwa wala vikundi vya vijana vinavyoomba omba msaada au kuhitaji kusaidiwa. Hawa si wenzao japa wanaweza kujifanya wenzao wakati huu wa kuelekea uchaguzi.

Wakati umefika wa kuwaonya akina Kinana wasichochee fujo kwani kuna maisha baada ya kuondoka madarakani. Hata kama wanataka kura, kwanini wasizitafute kwa kufuata kanuni na kusema ukweli. Heri ya kunyamaza kuliko kuchochea vurugu. Ni vizuri akina Kinana wakafahamu kuwa watanzania wa sasa siyo wale wa mwaka 47. Je kwanini Kinana anaendelea kuuhadaa umma?
Chanzo; Dira ya Mtanzania.

No comments: