Rais Jakaya Kikwete karibuni atatundika jezi kama rais wa nchi baada ya kuitawala Tanzania kwa vipi viwili vyenye utata. Hata hivyo, atakumbukwa kwa hisia tofauti kulingana na anayemtathimini alivyouona utawala wake. Kwa waliofaidika na utawala wake –hasa mafisadi –Kikwete atakumbukwa kama rais aliyewakomboa. Kwa wananchi wa kawaida maskini wanaoendelea kuumizwa na ufisadi na kuparaganyika kwa uchumi, watamkumbaka Kikwete kama rais wa hovyo aliyewazamisha zaidi kwenye mateso na mahangaiko bila sababu za msingi. Rejea kunyamazia ufisadi wa kutisha kama vile escrow ukiachia mbali kutumia fedha za umma vibaya kwa kuizunguka dunia akiandamana na kila watu wenye kutia shaka ambao mara nyingi walifanywa siri.
Pia Kikwete atakumbukwa kama rais ambaye angeweza kujisemea lolote bila kujali athari zake. Rejea alivyosema kuwa wanafunzi wa kike wanaopachikwa mimba ni kwa sababu ya kiherehere chao. Sijui binti zake wangekuwa waathirika kama angeyasema haya.
Nadhani seriali yake itaingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama rais aliyesimamia ufisadi wa kutisha mwingine akituhumiwa moja kwa moja kuushiriki bila kutoa maelezo au kukanusha. Rejea kashfa ya EPA ambayo inasemekana fedha zake ndizo zilimuwezesha kuwashinda wapinzani wake na kuingia madarakani akaendeleza mchezo ule ule. Rejea kashfa ya hivi karibuni ya escrow ambapo watuhumiwa wakubwa licha ya kuwa nje wakitanua, wengine wamesafishwa na ikulu ya Kikwete huyu huyu.
Kikwete atakumbukwa kama bingwa wa kutoa ahadi lukuki za kila aina asizitekeleze. Yako wapi maisha bora kwa wote yaliyogeuka bora maisha kwa wengi hasa ambao hawako karibu naye wala kuwa kwenye utawala wake.
Moja ya mambo ambayo atakumbukwa kwayo Kikwete ni kashfa zilizamisha mabilioni ya shilingi. Kashfa inayovuma kwa sasa –kama ilivyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni ya serikali kuendelea kuwalipia maafisa wake walioko ughaibuni hata baada ya kustaafu. Je kwanini serikali ilifanya hivyo na kwa faida gani kama hakuna namna?
Kimsingi, hawa ni wahalifu wanaopaswa kufungwa kwa kuhujumu taifa. Na isitoshe, wengi wa waliofichwa huko ughaibuni ni ndugu, jamaa au watoto wa wakubwa ndiyo maana serikali inatenda jinai hii kwa umma maskini wa watanzania. Wengi wameteuliwa kwa vigezo vya ajabu ukiachilia mbali kwa kificho kikubwa. Hivi watoto kama wa Edward Lowassa, Pius Msekwa, kweli wameteuliwa kwa vigezo gani zaidi ya majina ya wazazi na mitandao ya wazazi wao?
Kichekesho ni pale waziri anayesimamia wizara hii Bernard Membe kuutaka urais wakati anasimamia na kubariki ufisadi. Kama ameshindwa kusimamia wizara moja ataiweza nchi? Nadhani hiki ni kigezo kuwa Membe hafai kabisa kuwa rais kwa vile ameonyesha wazi anavyoshabikia ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma. Taarifa ya CAG inabainisha kuwa jumla ya Sh 543.7 milioni zilitumika kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani. Balozi ziliozoongoza kwa wizi huu ni zile za Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani). Ajabu ya maajabu, aliyekuwa balozi wa Tanzania Washington Liberata Mulamula alipandishwa cheo hivi karibuni na kuwa katibu wa wizara pamoja na kutajwa kwenye kashfa hii moja kwa moja. Kesho utasikia Shamim Nyanduga (Maputo) na Hemed Mgaza (Kinshasa) wamepandishwa vyeo. Kwa ubalozi wa Ottawa wengi walishuku pale alipoteuliwa mtuhumiwa wa utesajiwa Dk. Steve Ulimboka Jack Zoka.
Nadhani yote haya ni matunda ya uteuzi wa kujuana na kulipana fadhila ambao kimsingi, unadhoofisha uchumi wa taifa bila sababu za msingi. Kwa sasa Tanzania chini ya Kikwete inajiendesha au tuseme inaendeshwa kihovyohovyo na umma haustuki na kuchukua hatua.
Kikwete atakumbukwa kama rais aliyetamka wazi wazi kuwa ana orodha za wahalifu mbali mbali kuanzia mafisadi, wauza unga, majambazi lakini akasita kuwachukulia hatua pamoja na kupewa majina yao. Kwanini na ana faida gani nao? Nani anajua? Hakuna sehemu aliponiacha hoi Kikwete kama mkuteua Hilda Gondwe kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wakati mhusika anatuhumiwa kujipatia gari la serikali aina aina ya Toyota Land Cruiser VX iliyokuwa imenunuliwa miaka mitatu kabla kwa shilingi 155,000,000 kwa shilingi milioni moja na nusu tu huku akiusababishia umma hasara ya shilingi 149,000,000. Hata angekuwa Obama rais wa taifa tajiri asingemteua mtu huyu licha ya kutokumfikisha mahakamani. Huyu ana maadili gani wakati ni bingwa wa kupiga madili? Inaonekana hii ndiyo aina ya watu anayoitaka Kikwete kwa sababu anazojua mwenyewe.
Kitu kingine ambacho Kikwete atakumbukwa kwacho ni kujenga barabara ambazo hata hivyo hazikidhi viwango wala kulingana na kiwango cha fedha kilichotumika kuzijenga.
Pia Kikwete atakumbukwa kama rais ambaye serikali yake ililitumia vibaya jeshi la polisi kiasi cha kusababisha vifo na mateso ya watu wengi. Rejea mauaji ya mwanahabari Daud Mwangosi na kuteswa kwa daktari Ulimboka na mwandishi wa habari Absalom Kibanda.
Pia Kikwete atakumbukwa kwa kuwa rais wa kwanza kuamuru katiba aindikwe upya lakini akaisaliti na kutaka kupandikiza yake yenye kulinda mafisadi huku akipuuzia mawazo na maoni ya wananchi ukiachia mbali kutumia wahuni kumtisha aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni, jaji Joseph Warioba.
Si rahisi kuorodhesha mambo mengi ya hovyo ambayo Kikwete atakumbukwa kwayo. Hata hivyo, kuna funzo toka kwenye utawala wa Kikwete kuu likiwa ni kwamba watanzania wasirudie makosa kuchagua mtu kwa kuangalia sura, ahadi na ubobeaji wake katika usanii wa kisiasa.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 27, 2015.
5 comments:
kazi kweli!
LONGA LONGA ZA BURE NDUGU. LAIS NI LOWASA WAZIRI MKUU RUSTAM AZIZI
VIJANA SONGA MBELE HAYA NI MMAMUZI YANGU
LONGA LONGA ZA BURE NDUGU. LAIS NI LOWASA WAZIRI MKUU RUSTAM AZIZI
VIJANA SONGA MBELE HAYA NI MMAMUZI YANGU
Salaam,Mwalimu Mhango,
Makala yako hii Mwalimu Mhango,naona utawakasirisha wachache au umeshawakasirisha tayari wale ambao katika utawala huu wa awamu ya nne ya Rais Kikwete wanaona kama sio kweli kwamba Rais huyo kamaliza muda wake wa madaraka,wachahche hawa ambao wanatamani kama kungekuwa na uwezekano wa kubadilishwa hata kwa katiba ambayo ingeweza kumpa nafasi nyingine Rais huyu wa awamu ya nne aendelee kuitawala nchi.Wachache hawa hawaamini akili zao kwamba Rais huyu ambaye alikuwa anawalinda,anawakinga na kuwatetea katika ufisadi,ufisadi ambao yeye ndie alikuwa kinara cha ufisadi huo,amemaliza muda wake.Wachache hao ambao wameingiwa na woga wa aina moja au nyingine kwamba uwenda wanaweza kujikuta sehemu mbaya endapo Rais ajaye atawasimamia kidete, na tunatamani iwe hivyo.Rais Kikwete ataingia katika historia ya Tanzania na dunia kwamba ni mmoja wa marais mafisadi duniani mwenye kuupigania na kuutetea ufisadi wa kila aina na wa kila njia,Rais ambae ataingia katika historia ya Tanzania kama Rais muongo,msanii,mnafiki,kigeugeu,mwenye kujionyesha(show off)panapostahiki na pasipostahiki na hata ukimtia katika chupa atadiriki kutoa kidole chake na kusema nioneni nipo hapa!Rais ambaye hakuwa na haiba yoyote ile kulingana na cheo cha urais kilivyo.Kwa hiyo kuondoka kwa Rais huyu ni kama nchi ya Tanzania imeamka kutoka katika jinamizi na kabusi ambalo limeishi nalo kwa miaka yote hii kumi ya utawala wake.
Mwalimu,Muhango,kila mwanandamu huwa anapigania nafasi yake ya kutaka kujua kwa nini amekuwepo hapa duniani na mchango wake ni nini katika dunia hii,na hata akiondoka duniani ameacha urithi (legacy)gani katika dunia hii.Inapotokea kwamba huyu ni mwanadamu wa kawaida ambaye anapigania hivyo ,je na tujiulize iwapo mwanadamu huyu amepewa jukumu na watu wake la kuwaongoza na hakuja madarakani kwa mabavu,iweje leo mwanadamu kama huyu asifikirie kuacha urithi(legacy)ambao atakuwa anakumbukwa na kuingia katika historia kwa milango yake mipana na yenye mwangaza wa kutosha?Na hatimae mwanadamu huyu aliefikia cheo cha juu kabisa na cha mwisho katika nchi anapigania kuacha urithi(legacy)ambao kila akikumbukwa utakuwa unanuka tu,kutopendwa wala kuheshimiwa na wananchi wake na hatimae kuingia katika pipa la takataka ya historia?Mwalimu Mhango,je udhani kwamba huyu Kikwete kukipata hiki cheo cha uraisi ilikuwa ni bahati tu au tuseme bahati mbaya(coincidental)?Au tukimchambua kisaikolojia udhani kwamba kulikuwa na mapungufu katika utoto wake mpaka ujana wake wa kuishi na kujihisi upungufu(inferiority complex)Kwamba ameupata uraisi kwa bahati au kwa bahati mbaya inabidi afanye madudu yote aliyoyafanya?Mana hata kupenda kwake kusafiri (Vasco da gama wa afrika kama ulivyomwita katika safari zake)bila ya ulazima wowote kwa masilahi ya nchi unaashiria hali hiyo,hata kupiga piga picha na wanamichezo wa nje,kutembelea vilabu na viwanja vya mpira vya nje,kuwapokea wasanii wa nje ikulu,kupokea zawadi za ajabu ajabu pia unaashiria hali hiyo!
Mwalimu Mhango,Tumshukuru Mungu kwamba Tanzania imeamka katika usingizi wa miaka kumi na kugundua na kuona kwamba kumbe lilikuwa ni jinamizi na kabusi tu la miaka kumi ya Kikwete,wache tuone asubuhi mpya,mwangaza mpya,matumaini mapya na tuwe na matumaini kwamba yoyote yule tutakaemchagua asaidie kutusahulisha na hili jinamizi na kabusi la miaka yote hiyo ambao hatukupata usingizi mzuri.Ahsante kwa makala yako hii uzidi kubarikiwa.
Anon kwanza nashukuru kwa mchango wako pevu. Nitajitahidi kujibu maswali yako makuu mawili kuhusu Kikwete "kuukwaa" rais ambao aliugeuza urahisi na nafasi ya kula bila kunawa, kuzurura huku akiwaalika kila aina ya jamaa zake na vinyangarika kuja kuhomola. Kama ulivyobainisha, walaji wa Kikwete wote hawaamini kuwa miaka kumi imetimu na anatimka kwenda kwenye sahau. Je Kikwete aliupata urahisi kwa bahati au bahati mbaya? Tokana na mfumo mbovu uliokuwa umeanzishwa na Mwinyi ambaye kimsingi ndiye alimtengeneza Kikwete kwa ushawishi wa Kighoma Malima, yoyote angeweza kuwa rais hasa baada ya Mkapa aliyemrithi Mwinyi kugeuzwa fisadi la kunuka na mkewe ambaye hupenda kumuita Anna Tamaa. Hivyo, kosa la kwanza ni la kimfumo na pia la chama chao ambacho hata hivyo kilikuwa kimechafua kiasi cha wote walioutaka urais kuwa wachafu hasa baada ya wapambe wa Kikwete kuwachafua vibaya sana.
Suala jingine uliloongelea ni kwanini Kikwete ameashindwa kuacha legacy ya maana. Sidhani kama asiyejua maana huambiwa maana na kama mtu wa hovyo anaweza kuacha legacy ya maana zaidi ya hovyo kama yeye.
Kwa ufupi ni kwamba Kikwete anaingia kwenye vitabu vya historia si kama rais fisadi, muongo, kegeugeu,mlipiza visasi, malaya wala mnafiki tu bali ajali ya kisiasa kwa taifa letu. Naona niishie hapa.,
Post a Comment