Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Abdulrahaman Kinana huwa si mtu wa kuishiwa vituko. Wakati mwingine
akiongea mambo huwa unashindwa kuelewa kama anaelewa anachosema au wale
anawaambia kama anaamini kuwa wana akili kama yeye. Maana hujiongelea vitu
wakati mwingine kiasi cha kuacha maswali kuliko majibu.
Kwanza,
amejitahidi kujionyesha kama kiongozi tofauti na wenzake kwa kutumia muda
mwingi akitembelea mikoa na wilaya za Tanzania bila mafanikio. Anachofanya Kinana
licha ya kuwa kinyume na bosi wake yaani rais Jakaya Kikwete ni kama suto kwa
Kikwete. Wakati yeye akipenda kutumia siku nyingi vijijini mikoani, Kikwete
anatumia muda mwingi kwenye majiji makubwa ughaibuni.
Pili, Kinana huwa anatoa kauli za
kujikanganya, kukanganya na wakati mwingine hata kujisuta. Mfano juzi
alikaririwa akiwa huko wilayani Ngara akisema, “Msikubali kuyaachia mashamba
yenu kabla hamjalipwa fidia. Lazima mpewe mkono kwa mkono na siyo vinginevyo,
Serikali haiwezi kutekeleza mradi kama haina fedha za kutosha kuwalipa.” Kinana
alikuwa akijibu malalamiko ya wananchi kuhusiana na ardhi zao kutwaliwa bila
fidia wakati wa ujenzi wa miradi ya maendeleo. Inashangaza kuwa serikali
inayofanya haya ni ya chama anachokiongoza Kinana. Kama siyo kuwahadaa wananchi
–sijui wachague chama chake –ni nini wakati ana uwezo wa kwenda kuongea na
wenzake wakalipa hiyo fedha ya wananchi?
Pia Kinana akiwa wilayani Kyerwa alikaririwa
akisema, ““Hakuna haja ya kutumia ‘pasipoti’ kuhudhuria harusi au msiba wa
ndugu yako aliye nchi jirani, itoshe kutumia vitambulisho.” Je ni lini Kinana
akawa waziri wa mambo ya Ndani au ya Uhusiano wa Afrika Mashariki? Je anapotoa
amri kama hii haingilii mamlaka ya waziri mhusika ukiachia mbali kusahau kuwa
anaweza kuwahadaa wananchi asijue kuwa wengi wanajua msimamo wa Tanzania kuhusiana
na uhuria wa kuvuka mipaka yake kwa nchi jirani? Inakuwaje Kinana anapingana na
msimamo wa nchi kwa kutaka kutoa ruhusa kwa jambo ambalo bunge halijaridhia? Je
hapa Kinana alilenga kuonyesha ujinga wake au jeuri yake kama siyo kuchanganya
na kuingilia mamalaka ya wizara husika? Je Kinana aliongea haya kutafuta mtaji
wa kisiasa na kuonekana anawajali wananchi wakati matatizo yanayowahangaisha
yamesababishwa na serikali ya chama chake?
Sehemu nyingine Kinana alipoonyesha
usanii ni pale alipokaririwa akiwa wilayani Muleba akisema, “Uchangiaji wa mafuta ya Mwenge ni wa hiari, si
kuwalazimisha wananchi na kusababisha Serikali kutoaminiwa na mkichangisha
fedha hakikisha Mwenge huo unafika kwa wananchi wa eneo husika.” Kwanza,
watendaji wengi vijijini wanatumia mbio za mwenge si kuchangisha pesa ya mwenge
tu bali kujipatia chao ukiachia mbali kuwanyanyasa wananchi. Na hilo si kwamba
Kinana halijui. Analijua sema anawafanya watu wapumbavu tu. Pili, ukidurusu
kauli ya Kinana kwenye kipengele kinachosema, “mkichangisha fedha hakikisha
Mwenge huo unafika kwa wananchi wa eneo husika” haelezi utaratibu unaopaswa
kutumika kuchangisha. Na kwanini kuchangisha kana kwamba mwenge ni muhimu
hivyo? Kwa mtu ambaye angetaka kuwasaidia wananchi tokana na mateso wanayopata
na wizi wanaofanyiwa, angewakataza kuchangia mwenge. Lakini unaposema mchangishe na kuhakikisha
mwenge unafika kwa wananchi husika una maanisha nini kama hakuna shurti na
wajibu fulani?
Pamoja na Kinana kuwachukulia kama
watanzania hasa wa vijijini na mikoani ni kama hamnazo, alipata habari yake
mjini Bukoba alipotakiwa aeleze ni lini Meli ya MV Victoria meli pekee
wanayotegemea wakazi wa mkoa huo kuwaungisha na sehemu nyingine za nchi kwa
njia ya majini, alijaribu kujikanganya hadi wakamzoea. Ndipo alichukia na
kukaririwa akisema, “Suala la meli itakuja lini sijui, ila kama mnataka niseme
uongo nitasema kama hilo ndilo litanisaidia kutoka hapa salama, ila
watakapokuja wakubwa zenu waliowatuma waambieni walete hiyo meli kwa sababu
kila kitu kinakwenda kwa mipango. Rais alitamka msubiri sasa kama mmepewa elfu
kumikumi ili mje mharibu mkutano haya.” Kumbe kwa Kinana wanaompinga wamepewa
elfu kumi kuja kumpinga na si kupinga hoja zake zisizo na majibu au tuseme
mashiko kwa kero za wananchi? Je Kinana anaweza kutoa ushahidi kuwa waliomzomea
walihongwa elfu kumi? Je walihongwa na nani na kwanini linin na wapi? Je kauli
ya rejareja kama hii haimuonyeshi Kinana kama mtu anayeamini katika kutoa na
kupokea rushwa? Kama aliweza kuwaamuru wananchi waingie nchi jirani kwa
vitambulisho tofauti na sheria ya nchi, alishindwa nini kuamuru hao waliotoa,
kupokea rushwa na kutaka kuvuruga amani wachukuliwe hatua kama siyo usanii na
kuwadhalilisha wananchi?
Tutamalizia na kauli ya mwenzake,
Katibu wa Itikadi na Unenezi wa CCM taifa Nape Nnauye aliyeongea utumbo kana
kwamba wananchi ni wapumbavu wasiojua kupambanua. Alikaririwa akiwa wilayani
Ngara akisema, “Katiba ni
mradi wa wanasiasa kugawana madaraka. Ipite au isipite wakubwa hao watakuwa Dar
es Salaam wakigongeana glasi huku wewe ukishuhudia kupitia runinga. Tuwaache
wao waendelee na suala hilo na sisi tufanye ya kwetu.” Nnauye alikuwa akongelea
vurugu zilizozuka wilayani mle wakati wa kujadili katiba mpya ambayo hata hivyo
iliuawa na CCM. Ni kam alikuwa anawambia kuwa “nyinyi mlie tu” tukiamua hamna
cha kufanya bali kushuhudia tukitanua nanyi mkiendelea kuumia.
Kwa ufupi ni kwamba wapinzani
wanapaswa kuzitupia macho ziara za Kinana na Nape za mara kwa mara mikoani huku
wakichambua hoja zake kwa makini. Kwani anawanufaisha na kujibomoa bila kujua. Maana
kauli zake nyingi humuonyesha kama anayewafanya wananchi hamnazo wakati wanazo.
Chanzo: Dira Juni 25, 2015.
2 comments:
Ukitaka kujua kwamba aslimia kubwa ya wapiga kura wanamushkeli na ubongo zao angalia Lawassa wanavyompigia chapuo kwa kuanzia tuu...huo udhamini unavyoendelea.
Anon usemayo yana ukweli. Watu wetu wasipobadilika wataishia kuliwa na kulalamika kila baada ya uchaguzi mkuu.
Post a Comment